|

Miongoni mwa Masuala yanayohusu Saumu
Inamjuzia
mfungaji kuonja chakula kwa ulimi wake ili ajue uzuri na ubaya wake
(kwa mfano mpisi), kisha akiteme; kwani linalokatazwa ni kukiingiza
kooni.
Atakaekula kwa kudhani kungali usiku,
kumbe alfajiri imeshachomoza, kuna kauli kuwa anawajibika kuilipa
siku yake hiyo, na kuna kauli kuwa hawajibiki kuilipa na hii ndiyo
inayotumika.
Aliyekula
au kunywa akidhania kuwa jua limeshazama, kisha akagundua kuwa bado
halijazama, inamlazimu ailipe siku hiyo.
Atakaechelewesha kulipa saumu mpaka
ikafika Ramadhani nyengine, anatakiwa afunge Ramadhani iliyofika
kisha alipe siku alizokuwa akidaiwa, na anatakiwa kwa mujibu wa
baadhi katika wenye ilmu alishe maskini mmoja kwa kila siku
aliyochelewesha kuilipa mpaka ikaingia Ramadhani nyengine bila
dharura au sahau.
Kuingiza dawa kwa tupu ya nyuma k.m.
sindano ya nyuma hutengua saumu.
Kupiga sindano sehemu nyengine
hakufungulishi, ila ikiwa inatia chakula mwilini (vitamin).
Kutia
dawa ya maji jichoni kunafungulisha ikiwa itafika kooni, na wengine
wamesema hakufungulishi. Ama kutia dawa ya maji sikioni
hakufungulishi.
Kutia
marham au wanja machoni hakufungulishi, kwani si katika
vinavyochuruzika; na kisichochuruzika hakipenyi jichoni kikafika
kooni.
Dawa
ya kupuliza anayoitumia mwenye pumu, aki ihitajia mgonjwa katika
mchana wa Ramadhani ataitumia kisha atailipa siku hiyo, lakini
atajizuia na kula muda uliobaki katika siku aliyotumia dawa. Kulipa
kwake ni kuondoa wasiwasi, kwani maulamaa kadha wamemruhusu mfungaji
kuitumia bila kulipa saumu yake. Hukumu hii ikiwa dawa hiyo
haihitajii kila siku. Ama akiwa hawezi kuikosa, kila siku lazima
aitumie, basi na alishe maskini kwa kila siku ya saumu na
anasameheka kufunga.
Dawa
anayofanyiwa mgonjwa wa mafigo (kuosha figo) hufungulisha na
analazimika kulipa funga yake baadae.
Kupimwa
damu na kutoa mchango wa damu hakufungulishi.
Kunyoa
nywele za utupuni na kwapani hakufungulishi.
Mwenye
kufunga anaweza kutumia mafuta mazuri.
Kusati
(kuingiza dawa ya mafuta kichwani kupitia puani ili kutibu maradhi
ya kichwa n.k.) mchana wa Ramadhani kunahisabiwa katika
yanayofunguza; anatakiwa mwenye kufunga aliepuke hilo mchana wa
saumu, ila kwa dharura kubwa.
Kutoka damu mdomoni kwa sababu ya kun’goa jino n.k.
hakumfungulishi mfungaji ila akiimeza; na kama kumeza huko si kwa
makusudi na bila hiari basi hapana neno juu yake na hakutengui
saumu.
Aliyefunga akapata mtihani wa kumsaidia mtu
asiyejiweza, ikabidi kumuona utupu wake, basi saumu yake haina neno.
Kwani hajakusudia.
Atakaemeza makohozi bila kukusudia basi saumu yake
haina neno, na atakaeyameza makusudi saumu yake hutenguka.
Moshi wa kujifukiza haufungulishi kuutumia, ila
anatakiwa mwenye kufunga auepushe na uso wake, kwani ukiingia kooni
kwa makusudi utapelekea kutengua saumu yake.
Atakaemeza maji anapotia udhu bila kukusudia
haharibikiwi na saumu.
Haikatazwi kupiga mswaki mchana wa Ramadhani, bali
kunapendelewa, na mfungaji anatakiwa asitumie dawa ya meno isije
ikamtangulia kooni.
Mwanamke
anakatazwa kutumia dawa za kuzuia damu ya hedhi ili aweze kufunga;
kwani kufanya hivyo si dharura wakati Mwenyezi Mungu amemwekea
badala ya kulipa siku za hedhi.
Kumeza
kisicholiwa kunafunguza,
ila kukiwa bila hiari.
Atakaefungua
katika Ramadhani kwa udhuru
kama maradhi au
hedhi au nifasi, anaamrishwa azilipe siku alizokula kwa mfululizo
hata kama alifungua katika siku mbali mbali.
|