VIPI KUHIRIMIA

 

    Inapendelewa ajinadhifishe kwa kuondoa msokotano wa nywele, kunyoa nywele za siri, kukata kucha, kunyonyoa kwapa, kupunguza sharubu na kuondoa manukato, kwa ambaye bado hajafanya hayo.

§    Inapendelewa kuoga na kutawadha kabla kuhirimia kwa kila anayekusudia kuhirimia hata mwenye hedhi au nifasi.[1]

§    Mwanamme avue nguo zilizoshonwa na za kujivika[2] na avae kikoi, shuka ya kujifunika mabegani na viatu vya ndara; kutokana na kauli yake - rehema za Allah na amani zimshukie: “Na ahirimie kila mmoja wenu katika kikoi, shuka na viatu vya ndara.” Ameipokea Ahmed.

§    Ama mwanamke, kuhirimia kwake ni usoni; haimjuzii kufunika uso wake ila akiogopa kushawishi wanaume ndipo atauteremshia nguo uso wake bila kuigusanisha nao. Yeye anaruhusiwa kuvaa nguo iliyoshonwa, lakini aepuke kila ambayo ina mapambo, na anakatazwa kuvaa glavu, kama ilivyokuja kwenye hadithi: “Mwanamke mwenye kuhirimia asijifunge nikabu wala asivae glavu.” Imepokewa na Bukhari na wengineo.

   Asali rakaa mbili za ihramu kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni baada ya kuoga. Iwapo umefika wakati wa sala ya fardhi basi bora ahirimie baada ya sala hii na atamke

§    talbia baada yake moja kwa moja, na kuna kauli atamke talbia akishapanda kipando cha safari yake.

§    Anuie ibada anayokusudia (hija au umra) kama ilivyotangulia katika mlango wa namna za kuhiji na afanye talbia kwa kuainisha namna ya kuhiji anayokusudia. Akishakuwa juu ya kipando chake atanyanyua sauti kwa talbia.

§    Atakithirisha kutamka talbia hususan zinapobadilika hali na nyakati, k.m. akipanda kilima au akiteremka bonde na wakati wa kupanda kipando na wa kushuka, na kila baada ya sala; kwani talbia inaushughulisha wakati kwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Imepokewa kwa Sahlu bin Saad kuwa Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie - amesema: “Hatamki talbia Muislamu ye yote ila vitatamka nae talbia viliopo kuliani na kushotoni kwake vikiwa mawe au miti au udongo mpaka mwisho wa ardhi kwa upande huu na upande huu.” Imepokewa na Ibnu Majah, Baihaqiy, Tirmidhiy na Haakim akaisahihisha.

 

[1]- Kumekuja katika hilo baadhi ya mapokezi yaliyonasibishwa na Mtume na kumekuwa na hitilafu katika kuyasahihisha au kuyadhoofisha, isipokuwa yaliyopokewa na Muslim kwa njia ya Bibi Aisha - Mwenyezi Mungu amridhie - amesema: “Alijifungua Asma bint Umais Muhammad bin Abi Bakr penye mti (katika eneo la Dhul-hulaifa), Mtume S.A.W. akamuamuru Abu Bakr amuamuru aoge kisha ahirimie.” Kuna riwaya nyingine imemalizikia kwa Ibnu Umar amesema: ‘Ni katika sunna mtu aoge akitaka kuhirimia na akitaka kuingia Makka.” Ameisimulia Bazzaar na Daaraqutniy na Tabaraaniy kwenye ‘alkabiir’ na Haakim akaisahihisha.

[2]- Nguo zinazouzunguka mwili au baadhi yake kwa kushonwa au vinginevyo.

MAZINGATIO

§    Mwenye kusafiri kwa ndege atahirimia toka uwanja wa mwisho anaopandia ndege ili kuchukua hadhari asije akavuka miiqati ila amehirimia, na hapana ubaya kwake akitamka talbia baada ya kuondoka na ndege; muhimu ahirimie kabla ya kuvuka miiqati.

§    Inamjuzia muhrimu kuoga na kubadili nguo za ihramu alizovaa kwa nguo nyingine za ihramu akiepuka yaliyozuiwa katika ihram.

§    Inachukiwa kuifunga ihramu kwa pini kwa kuwa hilo linafanana na nguo iliyoshonwa.

§   Kuhirimia na kuvaa ihramu hakumlazimu mwenye kuingia Makka kama hajakusudia kufanya umra au hija.

§    Mwenye kuhirimia hija katika miezi isiyo ya hija ihramu yake hugeuka ya umra, na kuna kauli kwamba hubatilika.

§    Hakuna nia ya matamshi inayomlazimu mwenye kuhiji au mwenye kufanya umra anapohirimia, lakini inamlazimu kufanya talbia kwa kutamka na sio kwa kuileta moyoni.

§    Muhrimu asivae ukanda ila kwa dharura ya kufunga shuka aliyovaa na kuhifadhi pesa zake, na la hadhari zaidi ni kutovaa saa.

§    Kauli inayofuatwa kwetu na madhehebu nyingi ni kwamba manukato kabla ya kuhirimia hayakatazwi ikiwa yataoshwa.

§    Muhrimu inamharamikia kujitia manukato akiwa katika ihramu.

§    Muhrimu haruhusiwi kuondoa vinavyokamata taka mwilini kama kunyoa nywele, kukata kucha, kunyonyoa kwapa, kunyoa nywele za siri na nyinginezo, isipokuwa kwa dharura ya ugonjwa n.k.

§   Ni haramu kwa muhrimu maingiliano ya kijinsia baina mume na mke na kushikana kwa matamanio k.m. kulala pamoja katika nguo moja, kubusiana n.k.

§    Muhrimu hafungi ndoa wala hafungishi ndoa kutokana na kauli yake - rehema za Allah na amani zimshukie: “Muhrimu hafungi ndoa wala hafungishi ndoa wala haposi.” Imepokewa na Rabiu na Muslim.

§  Ni haramu kwa muhrimu kuwinda kiwindo cha nchi-kavu kutokana na kauli Yake Aliyetukuka:

) وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُماً(

   {Na mumeharamishiwa viwindo vya nchi-kavu maadamu mumo kwenye ihramu} [Al-maida 96]. Ama viwindo vya bahari havikatazwi.

§    Muhrimu hafuniki kichwa chake kwa cho chote ila kwa dharura kama matibabu, joto au baridi, ambapo itamwajibikia fidya.

§ Muhrimu anakatazwa kubishana kunakosababisha ghadhabu, kutokana na kauli Yake Aliyetukuka:

) الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلاَ رَفَثَ وَلاَ فُسُوقَ وَلاَ جِدَالَ فِي الْحَجِّ(

{Hija ni miezi maalumu; anayekusudia katika miezi hiyo kufanya hija basi hakuna kusema maneno machafu wala kufanya maasi wala kubishana katika hija} [Albaqarah 197].

§     Hakatazwi muhrimu kupiga msuwaki hata kama utakifanya kinywa chake kitoke damu.

§    Mwanamme atakayerefusha shuka yake zaidi ya vifundo vya miguu akiwa katika ihramu itamlazimu kuchinja.

§   Maneno machafu yanapingana na tabia za muislamu, na katika ihramu huwa yanachusha zaidi.

 

Copyright ©2004  Uislam.net