التقوّل على الله بغير علم

HATARI YA KUMZUSHIA ALLAH MAMBO YASIYO  NA UKWELI

بسم الله الرحمن الرحيم

Baada ya kumshukuru ALLAH kama anavyostahiki kushukuriwa sala na salamu zimfikie Mjumbe wake Sayyidna Muhammad s.a.w. pamoja na sahaba zake na kila anayefuata njia yake .

Umma wa Kiislamu:

Ninakuusiyeni na kuiusiya nafsi yangu kumcha ALLAH na kumtii Mtume wake aliyeletwa na kuhukumiana kwa kitabu chake kilioteremshwa na kujiepusha na tamaa za uongo na badala yake tujiandae kwa maneno ya kweli na vitendo vya ikhlasi , anasema ALLAH Mtukufu :

يا أيّها النّاس إنّ وعد الله حقّ فلا تغرّنّكم الحياة الدنيا ولا يغرّنّكم بالله الغرور ، إنّ الشّيطان لكم عدوّ فاتّخذوه عدوّا إنّما يدعو حزبه ليكونوا من أصحاب السّعير . / سورة فاطر : 5-6

Enyi watu! Bila shaka ahadi ya ALLAH ni haki . Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia , wala yule mdanganyaji mkubwa (Iblisi) asikudanganyeni juu ya ALLAH . Kwa yakini shetani ni adui yenu , basi nanyi mfanyeni adui yenu kwani analita kundi lake liwe katika watu wa motoni .

Na tambueni ya kwamba ALLAH ametutakia dini iliyosawa mila ya baba yetu Ibrahim na wala hakuwa katika washirikina , dini hii ALLAH amejitolea kulihifadhi chimbuko lake pale aliposema :

إنّا نحن نزّلنا الذّكر وإنّا له لحافظون . / الحجر : 9

Hakika sisi ndio tulioteremsha mawaidha (hii Qur-ani) na hakika sisi ndio tutakayoyalinda .

Na ameamua kuidhihirisha dini hii juu ya dini zote , kwa kusema:

هو الّذي أرسل رسوله بالهدى ودين الحقّ ليظهره على الدّين كلّه ولو كره المشركون . الصف : 9

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake (Nabii Muhammad) kwa uongofu na kwa dini ya haki ili kuifanya ishinde dini zote , ijapokuwa makafiri watachukiwa .

Kwa hivyo dini hii ya kiislamu pamoja na sheria zake na mafundisho yake ndiyo yenye kuleta manufaa pahala popote na nyakati zote kwa maslahi ya mwanadamu , kwani humuongoza mwanadamu katika njia iliyonyooka na humpatia ufumbuzi wa matatizo yake kwa njia nzuri kabisa .

Na kwa wingi wa ukarimu na fadhila , pale ALLAH alipojaaliya kuwepo watakoikinga sheria yake na kuwepo walinganiaji wa dini yake , huwafungua watu macho yao na akili zao ili wafuate yale yatakayowaongoza vizuri katika dini na dunia na akhera yao na watu wa namna hiyo ALLAH amewatunukia elimu na hikma na nuru ya uongofu , kama alivyonena Mjumbe wa ALLAH kwa kusema :

يحمل هذا العلم من كلّ خلف عدوله ، ينفون عنه تحريف الغالين ، وانتحال المبطلين وتأويل الجاهلين

Wataibeba elimu hii waadifu watakaokuja baadaye , watayakataa mabadiliko ya wanaopenda kubadilisha mambo katika dini na uzushi wa waovu na fikra za wajinga .

Kwa hivyo ndio maana akatuamrisha ALLAH kuwauliza hao wanavyuoni watendao amali njema kwa kusema :

فاسألوا أهل الذكر إن كنتم لا تعلمون .

Waulizeni wenye elimu ikiwa nyinyi hamjui.

Na ALLAH Mtukufu ametukataza kuwauliza wale wanaowapoteza watu kwa kutojua kwao mambo ya dini kwa sababu wanatoa fatwa za dini bila ya kuwa na elimu na hupelekea kumzushia ALLAH mambo asiyoyasema .

Ndugu Waislamu:

Hakika kusema maneno juu ya ALLAH bila ya kuwa na elimu nayo ni katika madhambi makuu ambayo pindi mwanadamu akiitumbukiza nafsi yake katika jambo hili huwa ameangamia na kuwaangamiza wengine , kwani ALLAH anasema katika kitabu chake :

ولا تقولوا لما تصف ألسنتكم الكذب هذا حلال وهذا حرام لتفتروا على الله الكذب إنّ الذين يفترون على الله الكذب لا يفلحون . / النحل : 116

Wala msiseme kwa sababu ya uongo usemao ndimi zenu “Hili ni halali na hili ni haramu” msije mkamzulia uwongo ALLAH . Hakika wale wamzuliao uwongo ALLAH hawatafaulu.

Na imekuja katika hadithi ya Mtume s.a.w. haya yafuatayo:

إنّ كذبا عليّ ليس ككذب على غيري ، فمن كذب عليّ متعمّدا فليتبوّأ مقعده من النّار .

Hakika uwongo usemwao juu yangu si kama uwongo usemwao kwa asiye kuwa mimi kwani atakayenizushia uwongo kwa makusudi basi ayaandaliye makalio yake katika moto .

Na miongoni mwa yaliyokuja katika tafsiri ya kauli ya ALLAH isemayo:

ويوم القيامة ترى الذّين كذبوا على الله وجوههم مسودّة . / الزمر : 60

Na siku ya kiama utawaona wale waliomsingizia uwongo ALLAH nyuso zao zimekuwa nyeusi .

Basi wamesema wenye elimu kuhusu Aya hii : Hapana shaka kwamba kusema uwongo juu ya ALLAH na Mtume wake katika kuhalalisha haramu na kuharamisha halali ni kufuru .

Na Bani Israil walitumbukia katika shari hii kubwa , pale walipokuwa wakisema wasiyoyajua na mwisho wao ukawa m-baya , na ALLAH ametuelezea habari zao kwa kutuonya ili tusije tukawafuata , na yakatufika kama yaliyowafika , anasema ALLAH

ها أنتم هؤلاء حاججتم فيما لكم به علم فلم تحاجّون فيما ليس لكم به علم والله يعلم وأنتم لا تعلمون . / آل عمران : 66

Angalieni , Nyinyi mlibishana katika yale mliyoyajua .Mbona (sasa) mnabishana katika yale msiyoyajua ? Na ALLAH ndiye ajuaye , nyinyi hamjui kitu.

Na jambo muhimu linalotufahamisha kuwa kumzushia ALLAH uwongo ni dhambi kubwa , kauli ya ALLAH :

قل إنّما حرّم ربّي الفواحش ما ظهر منها وما بطن والإثم والبغي بغير الحقّ وأن تشركوا بالله ما لم ينزّل به سلطانا وأن تقولوا على الله ما لا تعلمون . / الأعراف : 33

Sema (uwaambie) “Mola wangu ameharamisha mambo machafu , yaliyodhihirika na yaliyojificha na ni dhambi kutoka katika taa (ya wakubwa pasipo haki) na kumshirikisha ALLAH na ambacho hajakiteremshia dalili na ameharamisha kusema juu ya ALLAH msiyoyajua .

Na hapa tunaona namna ALLAH alivyoambatanisha baina ya kumzushia yeye uwongo na kumshirikisha jambo ambalo hapana ubaya zaidi yake na dhambi kuliko hili .

Kwa kutokana na haya inakatazwa kufanya maskhara na mchezo katika kauli za kifiqhi bali na kutoa fatwa kwa njia ya maskhara , kwani mwanadamu hana ruhusa ya kuyafanyia mchezo mambo haya na kumsingizia uwongo ALLAH .

Ndugu Waislamu:

Anasema ALLAH Mtukufu:

يا أيّها النّاس كلوا ممّا في الأرض حلالا طيّبا ولا تتّبعوا خطوات الشيطان إنّه لكم عدوّ مبين ، إنّما يأمركم بالسّوء والفحشاء وأن تقولوا على الله ما لا تعلمون . / البقرة : 168 169

Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi , halali na vizuri , wala msifuate nyayo za shetani , bila shaka yeye kwenu ni adui dhahiri . Yeye anakuamrisheni kufanya mambo mabaya na machafu , na mumsingizie ALLAH msiyoyajua.

Basi tazameni ndugu waislamu namna gani shetani anavyoamrisha watu na nini anachowaamrisha ? anawaamrisha katika njia ya kuwatia wasiwasi na kuwapotosha na wamzushie ALLAH uwongo , basi kafanya yote haya kwa lengo la kuwafanya watu wamuasi mola wao kisha yawe makazi yao motoni tena wakae humo milele .

Kwa hivyo wajibu wetu ni kujiepusha na kusema tusiyoyajua kwa ujumla na kutosema kabisa katika mambo ya sheria bila ya elimu , kwani kusema hili ni haramu na hili ni halali bila ya kuwa na elimu humuingiza mtu katika maangamizo na hata ikitokezea kuwa  amesibu jawabu sahihi . Imepokewa kutoka kwa Mtume s.a.w. kwa mapokezi ya Imam Al Rabii kwamba amesema Mtume s.a.w. :

من أفتى مسألة أو فسّر رؤيا بغير علم كان كمن وقع من السّماء إلى الأرض فصادف بئرا لا قعر له ولو أنّه أصاب الحقّ .

Anayefutu mas-ala au kufasiri ndoto bila ya ujuzi huwa ni sawa (katika upotofu) na anayeanguka kutoka mbinguni mpaka ardhini kisha akatumbukia ndani ya shimo lisilokuwa na mwisho na hata ikiwa atasibu haki.

Basi ndugu waislamu jambo hili ni kubwa na hatari , kwa hivyo inatupasa kutafuta kauli ya kweli na rai iliyosawa na tujiepushe na yale yote yanayopelekea kumuudhi ALLAH na huwenda Mola wetu akatuingiza katika waja wema .

والسلام عليكم ورحمة الله وبركاته .