UMRA

 

Kuoga kwa ajili ya ihramu na kutawadha, na yote ni katika yanayopendelewa.

Kusali rakaa mbili za sunna ya kuhirimia; ama ikiwa sala ya fardhi imewadia basi itatosheleza.

Kutamka talbia:

"لبيك اللهم لبيك، لبيك لا شريك لك لبيك إن الحمد والنعمة لك والملك لا شريك لك"

“Labbayka-LLahumma labbayk. Labbayka laa shariika laka labbayk. Innal-`hamda, wan-ni`imata laka wal mulk. Laa shariika lak”

(Nakuitika tena na tena ewe Allah. Nakuitika tena na tena, huna mshirika, nakuitika tena na tena. Hakika shukrani na neema ni Zako pamoja na ufalme; huna mshirika)

Na baadhi ya wakati utaongeza:

"لبيك بعمرة"

“Labbayka bi`umrah”

(Nakuitika tena na tena kwa umra)

Utaendelea na talbia hii mpaka uingie Al-Masjid Al-Haraam (Msikiti Mtakatifu wa Maka), na inapendelewa uingie kwa Mlango wa Salaam (Baabu-ssalaam) na useme:

"اللهم أنت السلام ومنك السلام وإليك يرجع السلام فحينا ربنا بالسلام وأدخلنا الجنة دار السلام تباركت ربنا يا ذا الجلال والإكرام"

“Allahumma Antas-salaam, wa minkas-salaam, wa ilayka yarji`us-salaam, fa`hayyinaa Rabbanaa bis-salaam, wa adkhilnal-jannata daaras-salaam, tabaarakta Rabbanaa yaa Dhal-jalaali wal ikraam”

(Ewe Allah! Wewe ndiye Uliyesalimika [na kasoro], na kwako Wewe hupatikana salama, na kwako Wewe ni marejeo ya salama, basi tuamkie Mola wetu kwa salama, na utuingize Peponi - Nyumba ya salama; umetukuka Mola wetu, ewe Mwenye utukufu na ukarimu)

 Utakapoiona Nyumba Takatifu sema:

"اللهم زد بيتك هذا شرفا وتعظيما وبرا وتكريما وزد من حجه أو اعتمره هداية وفضلا وبرا وتقوى"

“Allahumma zid baytaka haadha sharafan wata`adhiimaa, wa birran wa takriimaa, wa zid man hajjahu au i`itamarahu hidaayatan wa fadhlaa, wa birran wa taqwaa”

(Ewe Allah! Izidishie Nyumba Yako hii utukufu na uadhimisho, na ihsani na kuhishimika, na mzidishie mwenye kuihiji au kuifanyia umra uongofu na fadhila, na wema na ucha-Mungu)

Tawafu: ukianzia kwa kulibusu Jiwe Jeusi ukiweza; usipoweza utaligusa na kubusu mkono wako baada ya kuligusa, na isipowezekana utaliashiria kwa mkono wako. Kisha utatufu ukiijaalia Nyumba Takatifu kushotoni kwako, na utasoma ‘Albaaqiyaatu Assaalihaatu’ (yaani: “SubhaanaLLah walhamduliLLah, walaa ilaaha illa-LLah waLLahu akbar”) na kuomba utakayo.

Unapofika sawa na Pembe ya Yamani utaigusa ikiwezekana na kusema:

"ربنا آتنا في الدنيا حسنة وفي الآخرة حسنة وقنا عذاب النار"

“Rabbanaa aatinaa fid-dun`ya `hasanatan wa fil aakhirati `hasanatan wa qinaa `adhaaban-naar”

(Ewe Mola wetu! Tupe duniani mema, na akhera mema, na tukinge adhabu ya Moto)

Utaendelea kutufu hivi hivi mpaka tawafu itimie kwa mizunguko saba.

Kusali nyuma ya Maqamu ya Ibrahiim rakaa mbili na kuomba utakayo.

       Kunywa maji ya Zamzam na kujirushia usoni na kichwani.

Kisha unaondoka kuelekea kwenye Safa. Ukishapanda juu ya Safa utakabir mara tatu au mara saba na utasema:

"لا إله إلا الله وحده لا شريك له الملك وله الحمد وهو على كل شيء قدير، لا إله إلا الله وحده أنجز وعده ونصر عبده وهزم الأحزاب وحده"

“Laa ilaaha il-la-llaahu wa`hdahu laa shariika lahu, lahul-mulku walahul-`hamdu wa huwa `alaa kulli shay’in Qadiir. Laa ilaaha il-la-llaahu wa`hdah, anjaza wa`adah, wa nasara `abdah, wa hazamal-a`hzaaba wa`hdah”

(Hapana anayestahiki kuabudiwa ila Allah peke Yake hana mshirika. Ufalme ni wake na Yeye ndiye wa kushukuriwa na Muweza juu ya kila kitu. Hapana anayestahiki kuabudiwa ila Allah peke Yake. Ametimiza ahadi Yake, akamnusuru mja Wake na akayashinda makundi ya washirikina peke Yake).

Na utamsalia Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie - na kuomba utakavyoweza.

Kisha utateremka utembee na huku unasema:

"اللهم اجعل هذا المشي كفارة لكل مشي كرهته مني ولم ترضه مني"

“Allahumma ij`al haadhal-mashya kaffaaratan likulli mashyin karihtahu minniy walam tardhahu minniy”

(Ewe Allah! jaalia mwendo huu uwe wenye kufuta makosa ya kila mwendo uliouchukia kutoka kwangu na usiouridhia kwangu)

Na utaomba utakayo.

  Ukifika kwenye alama ya taa za rangi ya kijani utatembea kwa mwendo wa kasi mpaka ufike kwenye alama ya pili nawe unasema:

"رب اغفر وارحم وتجاوز عما تعلم إنك أنت العلي الأعلى وأنت الأكرم وأنت الرب وأنت الحكم"

“Rabbi-ghfir war-`ham, watajaawaz `amma ta`alam, innaka Antal-`aliyyul-a`alaa wa Antal-akram wa Antal-`hakam”

(Mola wangu samehe na urehemu, na usiyahisabu unayoyajua; hakika Wewe ndiye Mtukufu wa juu kabisa, na Wewe ndiye Mkarimu wa wakarimu, na Wewe ndiye Mola na Wewe ndiye Hakimu)

Baada ya alama ya pili utatembea mwendo wa kawaida mpaka ufike Marwa na utafanya juu yake kama ulivyofanya juu ya Safa. Kisha utarudia hivyo hivyo baina ya Safa na Marwa mpaka itimie mizunguko saba.

   Kisha kutokana na ihramu, kwa kunyoa au kupunguza nywele.

MAZINGATIO

Umra ni wajibu (fardhi) kutokana na kauli Yake Aliyetukuka:

)وَأَتِمُّواْ الْحَجَّ وَالْعُمْرَةَ لِلّهِ(

{Na timizeni hija na umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu} [Albaqara, 196], vilevile kutokana na hadithi ambazo zimetaja kwa uwazi kuwa umra ni fardhi kama hija.

_ Mwenye kukusudia umra baada ya hija asifanye umra siku za tashriq (tarehe 11, 12, na 13 Dhul-hija), bali afanye siku ya terehe 14 Dhul-hija.

_ Kufanya umra hakuwezi kuwa badala ya hija ya fardhi hata kukikaririwa; mtu hana budi kutekeleza fardhi ya hija.

_ Inajuzu kukariri umra isipokuwa katika miezi ya hija.

 

Copyright ©2005  uislamu.net