UDH`HIYA

 

  Asiyekuwa kwenye hija atachinja anachotaka kati ya wanyama wa kuchunga wa miguu mine ili kujikurubisha kwa Allah Aliyetukuka siku ya kuchinja (tarehe 10 Dhul-hija). Imepokewa kwa Bibi Aisha – Mwenyezi Mungu amridhie – kwamba Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie - amesema: “Hatafanya mwanaadamu siku ya kuchinja amali yo yote itakayopendeza mno kwa Allah kuliko kumwaga damu.” Imepokewa na Tirmidhiy.

 

  Kuchinja siku hiyo ni sunna iliyotiliwa nguvu; inachukiwa kuiacha pakiwa na uwezo. Dalili ya kusuniwa ni hadithi aliyoisimulia Muslim kwa sanadi yake kutoka kwa Ummu Salamah kwamba Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie - amesema: “Mtakapouona mwezi muandamo wa Dhul-hija, akataka mmoja wenu kuchinja basi asikate nywele zake na kucha zake (mpaka achinje).” Imepokewa na Muslim. Kauli yake [akataka kuchinja] ni dalili ya kusuniwa na sio kuwajibishwa.

 

YANAYOSHURUTISHWA ILI UDH`HIYA IWE SAHIHI:

 

Mnyama anayechinjwa kutokuwa na ila ya kuchukiza k.m.: chongo wa kubainika, mgonjwa wa kubainika, na kilema wa kubainika.

Awe kati ya wanyama wa kuchunga wa miguu mine (ngamia, n`gombe, mbuzi na kondoo).

Achinjwe baada ya sala ya Idi kwa dalili ya hadithi ya Al-Barau – Allah amridhie – kutoka kwa Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie - amesema: “La kwanza tunaloanzia katika siku yetu hii ni tusali kisha turejee tukachinje; atakayefanya hivyo ameipata sunna yetu; na atakayechinja kabla basi hiyo ni nyama tu amewaletea watu wa nyumbani kwake, haimo kabisa katika ibada ya kuchinja.” Imepokewa na Bukhari na Muslim.

Awe amefikia umri unaokubalika kisharia kama ilivyotangulia kutajwa kwa mnyama wa  hadyi.

 

MAZINGATIO

  Mtu akichinja kondoo au mbuzi mmoja atamtosheleza yeye na watu wa nyumbani kwake. Dalili ni hadithi ya Atau bin Yasaar amesema: “Nimemuuliza Abu Ayoub Ansaari vipi zilikuwa udh`hiya katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema za Allah na amani zimshukie, akasema: ‘Mtu alikuwa akichinja kondoo au mbuzi mmoja kwa niaba yake na watu wa nyumbani kwake na wakimla na wakilisha, mpaka watu waliposhindana kwa ufakhari ndio yakawa kama uonavyo’.” Imepokewa na Tirmidhiy na akasema ni hadithi sahihi, vilevile imepokewa na Malik na Ibnu Maajah.

  N`gombe au ngamia mmoja hutesheleza kwa watu saba. Imepokewa kwa Jabir amesema: “Tumechinja pamoja na Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie - ngamia mmoja kwa niaba ya watu saba au n`gombe mmoja kwa niaba ya watu saba.” Imepokewa na Muslim, Abu Daud na Tirmidhiy.

 

    - Inapendelewa katika mnyama uliyechinja kula, kutoa sadaka, na kuweka akiba, kutokana na hadithi: “Kuleni na mulishe na muweke akiba.” Imepokewa na Muslim.

   - Inasuniwa kwa mwenye kujua kuchinja achinje udh`hiya yake kwa mkono wake mwenyewe, na aseme: “Bismi-LLahi waLLahu Akbar, Allahumma haadha an fulaan – ajitaje; kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu alichinja kondoo na akasema: “Bismi-LLahi waLLahu Akbar, Allahumma haadha `anniy, wa `an man lam yudhah`hi min ummatiy.” (Ewe Allah! kuchinja huku ni kwa niaba yangu na kwa niaba ya wasiochinja kati ya umma wangu). Imepokewa na Tirmidhiy na Abu Daud.

    Katika adabu za udh`hiya, mwenye kutaka kuchinja asiondoe kitu kati ya nywele zake wala ngozi yake wala kucha zake likiingia kumi la mwanzo la mwezi wa Dhul-hija mpaka achinje. Dalili ya hayo ni hadithi ya Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie - aliposema: “Likiingia kumi la mwanzo, na ye yote kati yenu akataka kuchinja, basi asitoe kitu katika nywele zake wala katika kucha zake mpaka achinje.” Imepokewa na Muslim; na katika riwaya moja “wala katika ngozi yake” yaani kwa kunyoa nywele zake za chini au za kwapani.

     Ngozi ya mnyama wa udh`hiya haiuzwi, lakini inajuzu kuitoa sadaka.

     Mchinjaji hapewi sehemu ya nyama ya udh`hiya iwe ujira, lakini inajuzu kupewa katika nyama hiyo zawadi, kisha mwenye udh`hiya anaweza kumlipa kwa kazi yake ujira maalumu, kwa dalili ya hadithi: “Ameniamuru Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema za Allah na amani zimshukie - nisimamie ngamia na nitoe sadaka nyama na ngozi yake … na nisimpe mchinjaji kitu kati yake.” Imepokewa na Bukhari.

     Mnyama wa udh`hiya ambae baada kununuliwa amepata ila inayomfanya asifae kw

    udh`hiya, ikiwa mwenyewe ana uwezo wa kununua mwengine basi ambadilishe; ama akiwa hawezi basi huyo hutosheleza.

    Haitolewi sadaka thamani ya mnyama wa udh`hiya badala ya kuchinja udh`hiya kwasababu hilo ni kinyume na sharia. Amesema Aliyetukuka:

)فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ(

{Basi sali kwa ajili ya Mola wako na uchinje} [Al-kawthar, 2].

 

FIDYA

Mwenye kufanya umra akiona damu kwenye nguo yake baada ya kutokana na ihramu na hajui wakati gani imeingia hapana kitu juu yake.

Mwenye kulazimika kuchinja kwa ajili ya fidya asile kitu katika mnyama huyo; akila atachinja tena.

Atakayevaa nguo iliyoshonwa au kufunika kichwa chake kabla ya kunyoa au kupunguza nywele kwa kusahau atalazimika kuchinja kwa ajili ya fidya iwapo atabaki katika hali hio tangu usiku hadi mchana au tangu mchana hadi usiku. Vilevile iwapo ataendelea kuvaa baada ya kukumbuka na hakukimbilia kuvua; ama akikimbilia kuvua basi hapana kitu juu yake.

Mwenye kuacha kulala Muzdalafa itamlazimu kuchinja, ila ikiwa alibaki Muzdalafa mpaka kuzama kwa mwezi usiku wa kuamkia siku ya kuchinja.

Mwenye kuacha kulipiga Jamra la Aqaba atalazimika kuchinja.

Mwenye kujitoa manii wakati yumo katika ihramu kwa makusudi au amemuingilia mkewe hija yake au umra yake itaharibika na itamlazimu kuchinja ngamia au n`gombe.

Mwenye kuacha sai baina Safa na Marwa baada kutufu tawafu ya Ifadha itamlazimu kuchinja.

     Mwenye kuondoka Mina kabla ya kupindukia jua (adhuhuri) katika siku ya mwanzo ya kuondoka au ya pili itamlazimu kuchinja.

 

 

Copyright ©2004  uislamu.net