أثر الطّلاق على المجتمع
|
Baada ya kumshukuru Allah kama anavyostahiki kushukuriwa , sala na salamu zimfikie Mjumbe wake Sayyidna Muhammad s.a.w. pamoja na sahaba zake na kila anayefuata njia yake . Umma wa Kiislamu: Hakika Allah Mtukufu amekufaradhishieni mambo ya fardhi basi msiyawache, na amekuwekeeni mipaka na wala msiipindukie, na amekukatazeni baadhi ya mambo basi jiepusheni nayo . Na Tambueni ya kwamba mfungamano uliopo baina ya mume na mke ni mfungamano madhubuti, na ahadi iliyopo baina yao ni ahadi nzito, kwa hivyo usivunjike uhusiano wao kwa sababu za kipuuzi au zisizokuwa na msingi. Bali Allah mtukufu ameamrisha kuhifadhiwa uhusiano wa ndoa, ili utekeleze kazi yake na kuhakikisha lengo lake , na ulete furaha katika majumba na jamii na umma kwa ujumla, anasema Allah Mtukufu : ومن آياته أن خلق لكم من أنفسكم أزواجا لتسكنوا إليها وجعل بينكم مودّة ورحمة . / الروم 21Na katika ishara zake (za kuonyesha ihsani zake juu yenu) ni kuwa amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu kwao, naye amejaaliya mapenzi na huruma baina yenu. Na ilivyokuwa kulingana tabia ni jambo adhimu na kupatikana kwake si jambo rahisi, basi huwa hapanabudi kutokea matatizo katika maisha ya ndoa, na kuchafua mandhari yake, na kuwepo majonzi yanayokata furaha yake, na huwenda matatizo hayo yakatokana na mume au kwa upande wa mke, kwa hivyo pakazuka matatizo na kuzidi ukali wake, na shetani akaingia upande wake, ili kuzidi kuwasha moto wa fitna na kupandikiza chuki baina yao, na hatimaye maisha yakabadilika, na hapo ndipo watu wanapotafuta dawa ya kutatua matatizo, na kuulizia njia ya kutoka katika matatizo hayo. Na katika hali hii ngumu hutafautiana mitazamo ya watu, kuna watu hutumia akili zao na kuyapima mambo kwa mizani ya haki na uadilifu, na wakawa wanajua haki na wajibu wao, na watu kama hawa ndiyo waliowafikishwa katika mtazamo wao. Na kuna watu wengine wanafuata ghadhabu zao na kujisalimisha kwa nafsi zao, na wakati huo huwa hawasikii nasaha ya anayewanasihi wala mawaidha ya anayewaaidhi, basi mara mtu kama huyu huanza kumfokea mkewe na kumwambia : Nimekuwacha talaka tatu. Kwa hakika hili neno ni moja, lakini huvunja ukoo na huchafua maisha ya watoto na huyumbisha maisha kwa ujumla, kwani watoto wangapi wamekosa mapenzi ya mama zao, na kukosa malezi ya baba zao, maisha yao yamo katika dhiki na taabu, yote haya kwa sababu ya neno moja alilolitamka mtu pasi na kujali hatari yake , na bila ya kupima mambo kwa akili yake. Enyi Watu: Hakika imeenea talaka miongoni mwa watu kwa hali inayotisha, na utafiti wa suala hili unathibitisha hayo, jambo ambalo imekuwa ni wajibu kwa kila mtu kuwa na jukumu la kuiokoa hali hii na kuziba pengo hili , ili nyumba zirejee katika utulivu wake na nafsi zipate kupumua. Na huwa ni makosa makubwa pale mtu anapodhani kuwa hapana ufumbuzi ila kwa talaka, na hapana dawa ila kufarikiana, au hapana utulivu ila kwa kutengana, bali inatakiwa ieleweke kwamba talaka haihitajiki ila katika hatua za mwisho na inapokosekana njia kabisa, kwa hivyo huwa si hekima kuweka mambo sio pahala pake, na pupa mara nyingi huleta matatizo, na akili ndiyo kitu pekee kinachomsaidia mtu katika nyakati ngumu na kumfanya kuwa na uwezo wa kuimiliki nafsi yake, kwani huwenda mtu akafanya jambo bila ya kuzingatia akajuta maisha yake, na lau ingelikuwa watu wanalitilia maanani jambo hili, basi wasingeliikimbilia talaka, anasema Mtume s.a.w. : استوصوا بالنّساء خيرا ، فإنّكم أخذتموهنّ بأمانة الله واستحللتم فروجهنّ بكلمة الله . Wausieni wanawake mambo ya kheri, kwani nyinyi mumewachukua kwa amana ya Allah, na mumezihalalisha tupu zao kwa neno la Allah. Waja wa Allah: Hakika talaka sio silaha anayoichukua mwanamme mkononi mwake, wala sio njia ya kutishia na kuitumia pindi akihamaki, na wala sio zana ya ukandamizaji pale mwanamke anapokataa kutekeleza amri yake, bali talaka ni njia ya mwisho ambayo hutumiwa pale zinaposhindikana njia zote, na ikawa pahana tena maisha mazuri baina ya mke na mume , basi hapo ndipo talaka inatumika. Na dalili ya kuthibitisha haya, ni kwamba Allah Mtukufu hakuifanya talaka kuwa ndiyo tiba ya kwanza inayompasa mume kuitumia pale yakiwepo matatizo katika ndoa yao, bali zipo njia nyingi za kuondosha matatizo hayo bila ya kutumia talaka bali hata kuifikiria, anasema Allah : فالصّالحات قانتات حافظات للغيب بما حفظ الله ، والّلاتي تخافون نشوزهنّ فعظوهنّ واهجروهنّ في المضاجع واضربوهنّ فإن أطعنكم فلا تبغوا عليهنّ سبيلا إنّ الله كان عليّا كبيرا ، وإن خفتم شقاق بينهما فابعثوا حكما من أهله وحكما من أهلها إن يريدا إصلاحا يوفّق الله بينهما إنّ الله كان عليما خبيرا . / النساء 34-35 Basi wanawake wema ni wale wenye kutii, wanaojihifadhi hata wasipokuwepo waume zao, kwa kuwa Allah amewaamrisha wajihifadhi. Na wanawake ambao mnaona uasi wao kwenu waonyeni na waacheni peke yao katika vitanda na wapigeni. Na kama wanakutiini basi msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure. Hakika Allah ndiye aliye juu na mkuu. Na kama mkijua kuwa kuna ugomvi baina ya mke na mume basi pelekeni mwamuzi mmoja katika jamaa za mwanamme na mmoja katika jamaa za mwanamke. Kama wakitaka mapatano Allah atawawezesha. Hakika Allah ni mjuzi wa habari za siri na habari za dhahiri. Kwa kutokana na miongozo hii ya kisheria huweza kutatuliwa matatizo ya ndoa, na mwanzo wake ni kumpa mwanamke mawaidha laini ambayo yatamkumbusha kurudi kwa mola wake na kuchunga haki za mumewe, na yatamkumbusha kuhusu hatima ya watoto itakuwaje, na ikiwa mawaidha hayakufaa basi itafuatia hatua ya pili nayo ni kumuacha peke yake kitandani ili afahamu kwamba ipo haja ya kukaa na mumewe kwa vizuri, na ikiwa njia hii pia haikufaa basi na ampige pigo lisiloacha alama. Na ikiwa njia zote hazikufaa basi itafuata njia nyengine nayo ni kuhukumiana mbele ya wazee na kutaka ushauri wao juu ya kutatua matatizo yao, kwa hivyo mpaka hapa bado ingali talaka haikutajwa madhali hali inakubali kurekebishwa . Isipokuwa wapo baadhi ya waislamu ambao hawamuogopi Allah si katika kuowa wala katika kuacha , utamkuta mtu ameingia kwa mkewe na akaona jambo la upuuzi ambalo hakulipenda, au pakazuka malumbano kuhusu matumizi basi mara hupandwa na hamaki na kuanza kuapa kuwa amemuacha, kwa hivyo mambo kama haya hayafai, imepokelewa kutoka kwa Mtume s.a.w. kwamba amesema : من كان حالفا فليحلف بالله أو ليصمت . Anayetaka kuapa basi aape kwa ajili ya Allah au anyamaze kimya. Ndugu Waislamu: Tambueni ya kwamba maisha mazuri na mapenzi yaliyokamilika katika nyumba, hayapatikani isipokuwa pawepo na mafahamiano baina ya mume na mke, na ipatikane sharti ya kuridhiana tangu wakati wa kuoana . Na mwenye kuzingatia katika hali nyingi za talaka, atakuta kuwa haraka katika uamuzi pasi na kufikiria ndiyo sababu kubwa inayopelekea hayo , kwa hivyo ndoa sio jambo jepesi na kuilinda kwake inahitaji subira na ushupavu kadri ya uwezo, na wala isikimbiliwe talaka ila zikikosekana njia zote . Basi mcheni Allah ndugu waislamu, na yasuluhisheni mambo yenu kwa hikma na busara , na ziimarisheni jamii zenu katika njia nzuri , naye Allah atakusaidieni . والسلام عليكم ورحمة الله وبركاته
|