SAUMU YA SAFARI

 

Suala 1: Lipi bora kufunguwa saumu au kufunga ukiwa safarini?

Jawabu: Imekuja katika hadithi aliyoitoa Al-Imaam Al-Rabii kwa njia ya Anas bin Maalik (RA) kuwa amesema: (Tumesafiri na Bwana Mtume (SAW) na miongoni mwetu wako waliofunga na wasiofunga, na hajamtia ila aliyefunga yule asiyefunga, wala asiyefunga yule aliyefunga. Na ikatolewa riwaya hii na mashekhe wawili (Bukhari na Muslim) na wengineo kwa tamko (na hajatia ila aliyefunga juu ya asiyefunga, wala asiyefunga juu ya aliyefunga). Na juu ya riwaya zote mbili katika hadithi zina hukumu ya (kuinua) kulipa nguvu jambo. Ama riwaya ya Al-Imaam Al-Rabii yeye amekataa kuwa Mtume (SAW) amemtia ila aliyefunga juu ya aliyefunguwa wala aliyefunguwa juu ya aliyefunga. Yaani Mtume hajawalazimisha kufunga peke yake bila ya kufutari wala kuwalazimisha wafunguwe bila ya kufunga, bali wote (walio funga na waliofunguwa-walio kula) walikuwa sawa sawa katika hukumu, na katika hayo waliyoyafanya (nusu kufunga na nusu kufunguwa) mtume akawaacha juu ya jambo walilokuwa nalo. Ama  katika riwaya nyingine hadithi inaonyesha kuwa wao (masahaba) waliofunga na waliofunguwa walikuwa karibu na Mtume(SAW), jambo hilo wamelitenda huku Mtume(SAW) ameliona kwani walikuwa safarini na mtume (SAW). Na hii ni dalili kuonyesha kuwa mtume amelikubali jambo hili (kuwa nusu wamefunga na nusu hawakufunga), na kukubali jambo Mtume kwa tendo au kwa neno lake inaipa nguvu hukumu ya kukubaliwa.

Ama kuhusu nani ni mbora (aliyefunga au aliyefunguwa) Ulamaa wamekhitalifiana katika jambo hili. Wengine wamefadhilisha kufunga katika safari kwa kutegemea maneno ya Mwenyezi Mungu:(na mkifunga ni bora kwenu), lakini hii aya si nassi ya hili jambo kwani imekuja  baada ya kutaja fidia ikiwa mtu hawezi kufunga. Na kutokana na hilo ndio maana wanavyuoni wakafika kukhitalifiana katika hiyo fidia, je hukumu yake imebaki au imefutwa? Kama vile yalivyotandaa kwenye vitabu vya tafsiri na fiqh.

Na ambao mamefadhilisha kufungua safarini juu ya kufunga wametoa baadhi ya dalili katika riwaya nyingi nazo:

Hadithi inayosema (Si katika wema kufunga safarini) nayo ni hadithi sahihi aliyoitoa Imam Bukhari kwa njia ya Jabeer bin Abdullah. Lakini katika hii riwaya kuna linalojulisha sababu, nako ni kuwa Mtume (SAW) alimuona mtu aliyepata tabu sana kwa ajili ya kufunga safarini, ndio Mtume akamwambia: (Si katika wema kufunga katika safari), yaani mtu akifika akapata shida kupita kiasi kama hali hiyo iliyotajwa kabla.

Na hadithi hata kama wataichukulia kuwa ni hoja wale ambao hawajakubalisha kufunga katika safari, mpaka wakafika kusema (atakae funga katika safari ni kama amefunguwa akiwa nyumbani kwake) . Kuchukulia hadithi hii na amri ya Mtume (SAW) kwa kuamrisha masahaba wafunguwe mwaka walio walio ikomboa Mecca. Bali hamna hoja katika riwaya hizi mbili kukataza watu wasifunge wakiwa safarini.

Ama hadithi inayosema (Si katika wema kufunga katika safari), nayo hata kama imekuja kwa riwaya ya mtu mmoja lakini imekuja kwa tamko la ujumla. Na wamesema wanavyuoni (Hamna dalili ya kutegemea ikiwa jambo lime kuja khasa kwa jambo fulani lakini limekuja kwa tamko la ujumla), isipokuwa kuna la kulinganisha linajulisha kutizama hiyo sababu katika mfano wa hii hukumu pamoja na kujumuisha hii hukumu na riwaya nyenginezo. Na huku kulinganisha ni:

1)Kuwa Mtume (SAW) yeye mwenyewe alifunga katika safari na akafunguwa(akala), na masahaba walikuwa wakifunga na wakila, basi kuwepo vilinganishaji hivi inaonyesha kuwa Mtume (SAW) alitaka kuweka hii hukumu (ya kukataza kufunga safarini) juu ya yule aliyefika kilele cha kupata tabu kwa ajili ya kufunga safarini, si katika wema afunge, na kuna wanavyuoni waliosema kufunga katika safari si katika wema ni kuwa yule ambae amefunga safarini si kuwa amefikia kilele cha juu kabisa katika kufanya ibada na si dhidi yake kuwa yeye amefanya fujuur (makosa). Mfano wake ni maneno ya Mwenyezi Mungu (Hamuta fikia daraja (kilele) cha kuwa wema mpaka mtoe vile mnavyovipenda) kwani mtu akitoa misaada hata kama katika mali yake mbaya (nguo mbovu, pesa kidogo) haambiwi kuwa yeye si katika wema na kuwa kutoa kwake huku ni fujuur (makosa). Lakini kutoa kwake huko si kuwa katika kilele cha juu kabisa cha kuwa mtu mwema wa daraja ya juu kabisa.

2) Na tendo la mtume (SAW) katika mwaka wa kuikomboa Mecca kuwaamrisha masahaba wasifunge ilikuwa ni kwa ajili ya kukutana (kupigana) na maadui wa uislamu. Na ilikuwa mwanzo Mtume (SAW) amewakubalia masahaba wafunge kwa yule atakae taka kufunga, na alikuwa yeye na masahaba wamefunga mpaka walipofika pahali panapoitwa AL-KADEED akafunguwa(akala) na akawaamrisha masahaba wafunguwe(wale), ndio ikawa ni ruhusa kama anavyosema Abu Said Al-Khudary. Kisha akasema Mtume (SAW) baada ya hapo; (Hakika mnakwenda kukutana na adui basi fungueni kwani kufutari ni kuwapa nguvu nyie). Ikageuka ruhusa kuwa ni azma (motivation) ya kukutana (kupigana) na maadui. Wala haimaanishi kuwa kufungua katika safari ni waajib kwa mwenye kuweza kufunga bali anayo haki ya kuchagua kufunga au kuto funga (kula), lakini inapendezea kula ikiwa mtu atapata tabu katika safari ikiwa amefunga na inapendezewa kufunga ikiwa mtu atapata raha katika safari ikiwa amefunga, kwa ajili kulazimika kufunguwa katika safari ni kujiepusha na madhara na kuondosha uzito juu ya watu, na kutokuwepo na madhara na uzito inapendezewa mtu afunge akiwa safarini mwezi huo mtukufu wa ramadhani ili yule mwenye kufunga apate fadhila za mwezi mtukufu na pia apate fadhila za kufunga saumu. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

Na akasema Shk Ahmed katika jawabu jingine: Mwenye kuwepo safarini basi na afunguwe ramadhani (asifunge) maadamu anatakikana afupishe sala (asali sala ya safari akiwa safarini). Na imekhitalifika lipi bora kufunga au kufunguwa, lakini ni bora zitizamwe hali (dhuruf) na matatizo yatakayo kuwepo kwa ajili kukubalisha kufunguwa ni kuleta wepesi juu ya watu, kwa dalili ya maneno ya Mwenyezi Mungu:

(Mwenyezi Mungu anawatakia mepesi na wala hawatakii mazito), AlBaqrah  Aya 185.

(Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 
Suala 2: Nini jawabu lenu juu ya mtu anaetoka Omani ndani (shamba) na yeye anaishi Muscat (mjini) na unapoingia mwezi wa ramadhani hafungi kwa hoja kuwa yeye ni msafiri na inampa tabu kufunga katika sehemu yenye joto. Kisha anailipa ramadhani katika miezi ya baridi (shitaa)?

Jawabu: Ikiwa anaishi Muscat (mjini) mkao wa kuwa Muscat ni watani wake basi haikubaliwi kufanya hivyo. Na juu yake ni kafara kwa kila mwezi asiofunga nayo ni kumuachia huru mtumwa, au kufunga miezi miwili kwa pamoja (mfululizo) au kulisha maskini sitini. Allahumma, (ila) isipokuwa akiumwa maradhi yanayo mjuzia kufunguwa, nayo ni maradhi yanayo mfanyisha asiweze kufunga na yana mletea matatizo yaliyowazi au anaogopa maradhi yasizidi, katika hali zote hizi anaruhusiwa kufunguwa sharti azilipe hizo siku baada ya ramadhani kwa dalili ya maneno ya Mwenyezi Mungu: (Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine) Al-Baqara Aya 184. Ama kuchelewesha saumu kutoka mwezi wa joto mpaka miezi ya baridi kwa ajili ya joto peke yake na huku anaweza kustahamili basi haimjuzii kwa njia yeyote ile. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Suala 3: Je inamlazimikia msafiri akirejea kwake wakati wa mchana wa ramadhani ajizuwie kula na mengineyo akiwa hakufunga kwa ajili ya safari?
Jawabu: Baadhi ya Ulamaa wamependezea juu yake ajizuwie na kula, lakini hamna dalili juu ya hilo. Na kauli yenye nguvu kuwa hakatazwi kula kwani kujizuwia kula hakumpi faida yeyote na huku ameamka hakufunga, na kutofunga (kula) kwake kulikuwa kwa ruhusa ya dini aliyopewa msafiri kuwa anaweza kufunguwa. Na imetajwa katika baadhi ya vitabu kuwa Imam Jabeer bin Zayid (RA) amerejea kutoka safari alikuwa hakufunga na akamkuta mkewe amekosha hedhi yake mchana, na akamuingilia mchana wa ramadhani. Na jambo hili linajulisha kuwa si lazima (kuegemea zaidi) kutojizuwia na kula onaporudi safarini. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

Na akasema Shk Ahmed katika jawabu jingine: Atakae funguwa akiwa safarini katika mwezi wa ramadhani kisha akarejea mjini kwake mchana wa ramadhani na huku hakufunga basi hana kosa akiendelea kula.  (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Suala 4: Atakae tia nia ya kutofunga kutokea usiku kwa ajili anataka kusafiri, lakini ikamtokea (ikachomoza) alfajiri kabla hajatoka nje ya mji wake. Je ajizuwie kula au afungue?

Jawabu: Inamlazimikia ailipe siku hiyo kwa kila hali, kwa sababu hamna saumu kwa yule aliyelala bila ya kutia nia usiku, na huyu alitia nia ya kuto funga. Ama kula baada ya yeye kuondoka kuna khilafu baina ya wanavyuoni. Lenye nguvu ni kukubaliwa kula, lakini ihtiyaatt bora kuacha kula.  (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Suala 5: Mtu kaondoka nchini kwao miaka mingi na hajafunga alipokuwa katika safari hiyo, kisha akarejea nchini kwake akafunga kulipa ile miaka kwa makadirio (taqriiban). Je kuna kafara yeyote juu yake?

Jawabu: Haimlazimikii msafiri akirudi nchini kwake, na huku haku funga kwenye safari hiyo, isipokuwa kulipa siku alizo kula. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).