|
Bismillahi Rrahmani Rrahim. Baada ya
kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumtakiya rehma Bwana Mtume wetu Muhammad Salla
Llahu Alayhi Wasalam na Masahaba zake wote.
Amaa Baad:
Ndugu zangu Waislamu. Assalamu Alaykum
Warahamatu Llaahi Taala Wabarakatuhu. Nina furaha kubwa kwa kukutana tena na
wasomaji watukufu baada ya kile kitabu kilichopita Marafiki Wabaya, nikaona
kuwa bora tuendeleze harakati zetu za kukumbushana katika mema na kupeana
nasaha zitakazotufaa katika maisha yetu. Kwani ni wajibu wa kila mmoja wetu
kumpa nasaha mwenzake na vile vile ni wajibu wa kila apewaye nasaha njema ni
kuikubali tu bila ya kupinga na kukanusha, akajiona kuwe yeye kakamilika
wala hana kosa. Japo kuwa hufanyi makosa basi ikubali nasaha hiyo ili upate
makumbusho. Kwani sisi Waislamu kila mmoja wetu mbele ya mwenzake ni sawa
sawa na kiyoo, yaani hujiona kama ana makosa pale ambapo anamuona mwenzake
anatenda mema, basi na tujaribu kuyatizama maisha ya watu wema ili na sisi
tupate kufuata mwendo wao mzuri. Mara nyengine ni uzuri kumuuliza Mtu mwema
vipi unaishi maisha yako? Si kwa sababu ya umbea, hasha! Bali kutaka kujuwa
mwendo mzuri ili uufuate.
Watu wengi hujipangia maisha yao vile
wanavyoyataka wao wenyewe bila ya kujali amri na sheria za Mwenyezi Mungu.
Utawaona jambo la kwanza kwao ni kuishibisha nafsi na kuyafuata matamanio
yao. Lakini hawajui kwamba Mola wao aliyewaumba kawapangilia mwendo mzuri wa
maisha yao ili waishi katika usalama na amani bila ya kudhulumu wala
kudhulumiwa. Baada ya hayo akampa kiumbe huyu kila neema zitakazomsaidia
kuendeleza maisha yake hapa duniani. Neema ambazo mja huyu akitaka
kuzihisabu basi atashindwa wala hataweza kamwe kuzilipa, bali hata katika
neema ndogo tu aliyokupa Allah hutoweza kuilipa ewe kiumbe. Basi nini
kikudanganyacho ukawacha kumtii Mola wako?
Na katika neema kubwa alizopewa mwanaadamu
huyu katika maisha yake ni hii neema ya kuweza kuzungumza ukaeleza nini
ulitakalo na ukaweza kuwabainishia watu jema wakalifuata na baya wakaliacha.
Huo ni (ULIMI) kiungo kidogo tu! ukikifananisha na vengine, lakini hatari
yake kubwa kuliko hivo vengine. Huwenda mtu kutiwa motoni asitoke kwa sababu
ya ulimi wake mbaya. Na huwenda ukawa sababu ya kupata radhi za Mwenyezi
Mungu katika pepo zake. Viungo vyote vinauwita ulimi kwa kusema:
( اتَّقِ اللَّهَ فِينَا فَإِنَّكَ
إِنِ اسْتَقَمْتَ اسْتَقَمْنَا وَأَنِ اعْوَجَجْتَ اعْوَجَجْنَا )
“Ewe ulimi Mche Mola juu yetu, kwani ukinyooka wewe nasi tutanyooka na
ukikaa upande wewe nasi tutakaa upande”.
Ndio huwenda mtu akasifika mbali kwa sababu
ya maneno yake mazuri yenye maana na heshima, na watu wakampa heshima. Na
huwenda mwengine akasifika kwa mbali, kwa ulimi wake ulivyo mbaya hata
wengine wakawa wanamkimbia ili kuepukana na maneno yake machafu. Ole wake
Mtu kama huyo, tena Ole wake.
Watu wengi wanapuuza sana wayasemayo na wala
hawayafikirii, jee ni mema au mabaya, je yanamridhisha Mwenyezi Mungu au Laa.
Wao wamo tu, almuradi waseme tu, hawajali kama jema au baya. Hebu tegeni
masikio vyema muisikilize Hadithi ya Bwana Mtume (S.A.W) aliyepewa ulimi
bora akawafikishia watu wote ujumbe wa Mola Mtukufu. Hadithi ni kisa
anakieleza Sahaba mmoja anaitwa Muaadh bni Jabal (Radhi za Mola ziwe juu
yake). Hadithi hii imepokelewa na Imam Tirmidhiy na Ibn Majah na Ahmad:
عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ قَالَ كُنْتُ مَعَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهم
عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي سَفَرٍ فَأَصْبَحْتُ يَوْمًا قَرِيبًا مِنْهُ وَنَحْنُ
نَسِيرُ فَقُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ أَخْبِرْنِي بِعَمَلٍ يُدْخِلُنِي
الْجَنَّةَ وَيُبَاعِدُنِي مِنَ النَّارِ قَالَ لَقَدْ سَأَلْتَ عَظِيمًا
وَإِنَّهُ لَيَسِيرٌ عَلَى مَنْ يَسَّرَهُ اللَّهُ عَلَيْهِ تَعْبُدُ اللَّهَ
لَا تُشْرِكُ بِهِ شَيْئًا وَتُقِيمُ الصَّلَاةَ وَتُؤْتِي الزَّكَاةَ
وَتَصُومُ رَمَضَانَ وَتَحُجَّ الْبَيْتَ ثُـمَّ
قَالَ أَلَا أَدُلُّكَ عَلَى أَبْوَابِ الْخَيْرِ الصَّوْمُ جُنَّةٌ
وَالصَّدَقَةُ تُطْفِئُ الْخَطِيئَةَ كَمَا يُطْفِئُ النَّارَ الْمَاءُ
وَصَلَاةُ الرَّجُلِ مِنْ جَوْفِ اللَّيْلِ ثُمَّ قَرَأَ: (تَتَجَافَى جُنُوبُهُمْ عَنِ
الْمَضَاجِعِ
) حَتَّى بَلَغَ (
جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ) ثُمَّ قَالَ أَلَا أُخْبِرُكَ
بِرَأْسِ الْأَمْرِ وَعَمُودِهِ وَذُرْوَةِ سَنَامِهِ الْجِهَادُ ، ثُمَّ قَالَ
أَلَا أُخْبِرُكَ بِمِلَاكِ ذَلِكَ كُلِّهِ قُلْتُ بَلَى فَأَخَذَ بِلِسَانِهِ
فَقَالَ تَكُفُّ عَلَيْكَ هَذَا قُلْتُ يَا نَبِيَّ اللَّهِ وَإِنَّا
لَمُؤَاخَذُونَ بِمَا نَتَكَلَّمُ بِهِ قَالَ ثَكِلَتْكَ أُمُّكَ يَا مُعَاذُ
وَهَلْ يُكِبُّ النَّاسَ عَلَى وُجُوهِهِمْ فِي النَّارِ إِلَّا حَصَائِدُ
أَلْسِنَتِهِمْ )
Maana yake:
“Kutoka kwa Muaadh bni Jabal
kasema kwamba; nilikuwa safarini pamoja na Bwana Mtume (S.A.W) nikaamka siku
moja karibu naye tukawa tunakwenda, nikasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu.
Niambie amali gani nifanye ili iniingize Peponi na iniepushe na Moto. Mtume
(S.A.W) akasema: Umeuliza jambo kubwa, nalo ni jepesi kwa yule
aliyorahisishiwa na Mwenyezi Mungu. Umuabudu Mwenyezi Mungu na wala
usimshirikishe na kitu. Na usimamishe Sala na utowe Zaka na ufunge Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani na uwende Kuhiji Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Kisha Mtume
akaendelea kusema: Je nikufundishe milango ya kheri? Saumu ni kinga na
Sadaka huzima moto wa dhambi (hufuta) kama maji yanavouzima moto, na Sala ya
mtu pinga pinga la usiku, Kisha Mtume (S.A.W) akasoma Aya (Huiniuka mbavu
zao kutoka vitandani wakati wa usiku ili kumuabudu Mola wao….) mpaka akafika
Aya isemayo (Hayo ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyafanya) Surat Sajdah Aya
16 – 17.
Kisha Mtume (S.A.W) akasema: Jee nikwambie
jambo kubwa kuliko yote hayo; ni (Jihadi). Kisha akasema tena: Je nikwambiye
kinachotawala yote hayo yaliyopita? Muaadh akasema: ndio niambie, Mtume (S.A.W)
akachukuwa ncha ya ulimi wake na kusema: Jiepushe na huu (ulimi). Muaadh
akamuuliza Mtume (S.A.W) Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Kwani sisi
tunahisabiwa kwa kila tunayoyasema? Mtume (S.A.W) akashangaa na kusema: (Thakilatka
Ummuk) yaani ole wako! Kwani hawatomiminwa watu katika Moto isipokuwa kwa
ncha za ndimi zao.” Yaani kwa sababu ya madhambi ya ulimi ndio watu
watatumbukizwa katika moto.
Wallahi Hadithi hii ni muhimu sana kila
mmoja wetu kuijuwa, wanaume na wanawake, wadogo na wakubwa. Ili kila mmoja
awe anatahadhari sana na kuchuma madhambi ya ulimi bila yeye kujuwa. Na
inatutosha onyo kali kutoka kwa Mtume (S.A.W) pale aliposema katika Hadithi
sahihi iliyopokelewa na Imam Al Bukhary na wengineo:
( مَنْ كَانَ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَلْيَقُلْ خَيْرًا أَوْ
لِيَصْمُتْ )
Maana yake:
“Mwenye Kumuamini Mwenyezi Mungu
na kuiamini siku ya Mwisho basi aseme la kheri au anyamaze kimya”.
Na kumbuka kwamba neno unapolitamka tu, basi
kuna Malaika tayari wanaliandika katika daftari lako. Kasema Mwenyezi Mungu
katika Surat Qaaf Aya ya (18):
( مَا يَلْفِظُ مِنْ قَوْلٍ إِلَّا
لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ )
Maana yake:
“Hatoi mtu kauli yoyote
isipokuwa karibu naye yuko mngojeaji tayari (kuandika).
Basi kwa nini ewe mja ulijaze daftari lako
kwa mabaya ambayo ulikuwa ukiyachuma mwenyewe kwa ulimi wako. Ulikuwa
ukiwachekesha wenzako kwa kusema uwongo ili usifiwe. Jee Wako wapi leo?
Mbona hawakusaidii lolote, wewe ndie mwenye kukhasirika. Soma kwa makini
Hadithi ya Mtume pale anapomtahadharisha msema uwongo mwenye kuwafurahisha
wenzake vikaoni. Kasema Mtume (S.A.W) katika Hadithi iliyotolewa na Imam
Tirmidhy na Abi Daud na Imam Ahmad:
(وَيْلٌ لِلَّذِي يُحَدِّثُ
بِالْحَدِيثِ لِيُضْحِكَ بِهِ الْقَوْمَ فَيَكْذِبُ وَيْلٌ لَهُ وَيْلٌ لَهُ)
Maana yake:
“Ole wake mwenye kuhadithia
hadithi ili awachekeshe watu na huku akisema uwongo. Ole wake tena Ole wake”
Hatari kubwa hiyo. Lazima watu watahadhari
na wazichunge ndimi zao ili wajiokowe na adhabu kali ya Mwenyezi Mungu.
Tunamuomba Allah atuwezeshe kusema kila la haki na la kheri na kuwacha
maneno ya upuuzi (Amin).
|