HUKUMU YA KUVAA NGUO NDEFU KWA MWANAMME

 

Imethibiti katika Hadithi nyingi sana za Mtume (S.A.W) kwamba kasema: Nguo ya  Mwislamu mwanamume mpaka nusu ya miguu, na hapana ubaya kuwa baina ya magoti na baina ya vifundo vya miguu. Na Mwenyezi Mungu hamtazami mwanamme anayeburura nguo yake kwa majivuno”

Pia akasema Mtume (S.A.W) katika Hadithi nyengine: Kila nguo inayogusa chini (kwa urefu wake basi katika moto”

Na akasema (S.A.W): “Ionekane miguu katika kuvaa kikoi (nguo)”.

Na kwa hakika Mtume (S.A.W) alimuona mwanamme anaburura nguo akamkataza kufanya hivyo, na akasema yule kijana: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Hakika mimi miguu yangu ni myembamba iliyokonda sana (ninaificha isionekane). Mtume (S.A.W) akasema: “Kila umbo la Mwenyezi Mungu ni zuri”.

Na Hadithi kuhusu jambo hili (la kukatazwa kuvaa nguo refu) ni nyingi sana na ahadi ya kupata adhabu ngumu kwa kuvaa nguo ndefu. Na Mtume (S.A.W) alimuona mwamame anasali naye amevaa nguo ndefu akamwamrisha arudie kutia udhu mara mbili, akaulizwa Mtume (S.A.W). Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mbona umemwamrisha kutia udhu mara mbili? Akasema Mtume (S.A.W): “Hakika amesali na nguo yake ndefu na Mwenyezi Mungu haikubali sala ya mwenye nguo ndefu”.

Pia akasema Mtume (S.AW): “Mwenye kusali na nguo ndefu basi sala yake si chochote kwa Mwenyezi Mungu."

Yaani sala yake haikubaliwi. Na kwa haya inatosha kuwa ni dalili kubwa ya kuwa kuvaa nguo ndefu ni katika madhambi makubwa na sala ya mwenye nguo ndefu haikubaliwi na haijuzu asalishe au kuwa ni Imamu. Na Allah ndie ajuwae zaidi.

 

Copyright ©2004  Uislam.net