|
|
KUTOKANA NA
IHRAM YA HAJ NA UMRA |
Akimaliza
mwenye kuhiji siku ya kuchinja (10 Dhulhija) kupiga jamra na kuchinja
atatokana na ihramu yake kwa kunyoa au kupunguza nywele. Dalili ya hayo ni
hadithi ya Anas “kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema za Allah na amani
zimshukie -
alifika Mina akaja kwenye Jamra akalipiga kisha akenda alikofikia katika
Mina akachinja, kisha akamwambia kinyozi: ‘Ondoa’,
akaonyesha upande wake wa kulia wa kichwa kisha wa kushoto.”
Imepokewa na Muslim na Ahmad.
Mwanamke
haruhusiwi kunyoa kwa ajili ya umra wala hija, bali anapunguza kadiri ya
inchi moja. Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie
- amesema: “Na linalowapasa wanawake ni
kupunguza tu nywele zao.” Imepokewa na Abu Daud.
Kunyoa
ni bora kuliko kupunguza, kwasababu Mwenyezi Mungu amekutaja mwanzo katika
kauli Yake Aliyetukuka:
)
مُحَلِّقِينَ رُؤُوسَكُمْ
وَمُقَصِّرِينَ(
{mkinyoa vichwa
vyenu na mkipunguza nywele} [Al-fat`h, 27], na
kwasababu Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie - amesema:
“Allah awarehemu wenye kunyoa”
mara tatu, pakasemwa: ‘na wenye kupunguza?’, akasema:
“Na wenye kupunguza.”
Imepokewa na Rabiu, Bukhari na Muslim.
Yanamhalalikia
mwenye kuhiji baada kunyoa (au kupunguza) yale yote aliyozuiliwa kwasababu
ya ihramu isipokuwa mke na kuwinda. Hali hii huitwa “tahal-lul as-ghar”
yaani kutokana na ihramu kudogo. Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie
- amesema: “Mkishapiga jamra na kunyoa
itakuwa halali kweni kila kitu ila wake zenu.” Imepokewa
na Nasaaiy, Ahmed na Baihaqiy.
TAWAFU YA IFADHA NA SAI
Tawafu ya ifadha ni moja
kati ya nguzo za hija; hija huharibika kwa kuiacha.
Ni katika sunna
kutekeleza mawili haya siku ya tarehe 10 Dhul-hija baada ya kupiga jamra,
kuchinja na kunyoa au kupunguza nywele, lakini inajuzu kuyaakhirisha japo
baada ya siku za tashriq.
Mwenye hedhi
ataakhirisha tawafu ya ifadha mpaka atahirike.
Baada ya kutekeleza
mawili haya inakuwa halali kwa mwenye kuhiji kila alichokuwa kazuiliwa
isipokuwa kuwinda kwenye eneo la Haram; na hali hii huitwa “tahal-lul akbar”
yaani kutokana na ihramu kukubwa.
MATANGAZIO:
- Atakayetufu
tawafu ya ifadha kisha akalala Maka mchana na kurejea Mina jioni hapana kitu
juu yake lakini amefanya kinyume na lililo bora.
- Haizuiwi
kula na kunywa Maka baada ya tawafu ya ifadha, ila imekataliwa kulala hapo
mchana, lakini linalotegemewa katika fatwa ni kuwa inajuzu kulala mchana kwa
vile imethibiti kuwa Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie
- alilala mchana baada ya kutufu.
- Aliyetufu
tawafu ya ifadha mizunguko sita akakumbuka baada ya kurejea nchini kwake
itamlazimu arudi kwenye Haram na arudie tawafu ya ufadha katika mwaka wake
huo, na hapana kitu juu yake kwa rai ya baadhi ya wanazuoni ikiwa
hajamuingilia mkewe; ama ikiwa vinginevyo basi hana budi kuhiji tena.
|