KUONEKANA KWA MWEZI WA RAMADHAN

 

Suala 1: Aliyeona mwezi peke yake na ushahidi wake aliyo utoa kuwa yeye ameuona mwezi ukakataliwa na watu au wanavyuoni. Je afunge kwa kuona kwake huo mwezi wa ramadhani na afutari (afungue) kwa kuona kwake huo mwezi?

Jawabu: Saumu imeambatanishwa(imethibiti) kwa kuonekana mwezi, ikiwa kwa kuuona kwa macho au kwa ushahidi wa watu waaminifu wawili au kwa ushahidi wa umashuhuri wa watu wote. Wakakhitalifiana wanavyuoni kwa mtu muaminifu mmoja tu akiwa yeye peke yake ameuona mwezi je, ushahidi wake unakubaliwa au haukubaliwi? Kutokana na hivyo, kuona mtu mwezi peke yake inakuwa ni dalili juu yake tu kuwa saumu ni wajib kwake yeye kwa kuona mwezi, na haimjuzii kujidanganya nafsi yake, basi inamuwajibikia afunge ramadhani na afutari (afungue) mwisho wa ramadhani kwa siri ili ajiepushe na kudhaniwa vibaya na watu, na ni juu yake aidhihirishe saumu na ajizuie na vitu vyote vinavyo futarisha, hili ndio neno (jawabu) lenye nguvu ambalo wanavyuoni wa kiibadhi na wanavyuoni wengi wamelikubali. Na madhehebu ya Imam Hanbali, ameona kuwa huyo mtu awafuate watu wote kwa kufunga saumu na kufungua (kufutari) saumu yao ikiwa ushahidi wake wa kuona mwezi peke yake umekataliwa, basi afunge na afungue pamoja na watu. Na hoja yao ni hadithi ya Mtume (SAW): (Saumu ni siku watu wanayo funga na kufutari ni siku watu wanayo futar1, na Hajji ni siku watu wanayo hijji). Lakini makusudio ya hadithi hii, ni kuwa watu wana abudu kwa habari  iliyowafikia wao, na ikiwa kuuona mwezi kutafichika kwa ajili ya mawingu au kitu chochote kile, wakaichelewesha saumu kwa kufuata amri ya mtume (SAW), kwa kukamilisha mwezi wa kiislamu siku thalathini (30), kwani saumu inayo inayo kubalika juu yao ni ile saumu ambayo wameifunga. Saumu yao na kufutari kwao inategemea lile lilothibiti juu yao wote kwa kuuona mwezi. Na si makusudio ya hadithi hii kuwa mtu ajizuie na lile analo abudu yeye mwenyewe katika nafsi yake, na kuna hoja gani kubwa zaidi kuliko mtu kuona mwezi kwa macho yake, jambo ambalo limeambatanishwa kwa kuthibiti kufunga au kufungua. kwani Mwenyezi Mungu anasema: (Na atakae uona mwezi katika nyie basi na afunge), na Mtume (SAW) anasema : ( Fungeni kwa kuuona mwezi na fungueni kwa kuuona mwezi). Na hili ndilo lililothibiti juu yake huyo aliyeuliza suala, kuwa yeye ameuona mwezi na yeye anabudu kwa kule kuona kwake mwezi. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Suala 2: Ni masharti gani yanatakikana yapatikane juu ya yule mwenye kuona mwezi wa ramadhani ili ushahidi wake ukubaliwe?
Jawabu:Ni lazima awe ni mwenye akili(si mwendawazimu n.k), mtu baaligh, mtu muadilifu katika dini yake(anafuata dini yake sawasawa), na ushahidi wake uwe haukanushwi na ukweli wa mazingara ya maumbile ya kilimwengu (mawingu) (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).
 

Suala 3: Nini hukumu juu ya aliyefunga kwa nyakati za watu wa Oman, kisha akasafiri nchi nyingine iliyotangulia kufunga, ikawa saumu ya hiyo nchi ni siku thalathini (30), akafungua (akafutari) nao, hali ya kuwa yeye amefunga siku ishirini na tisa tu (29). Je inamuajibikia ailipe hiyo siku moja ikiwa watu wa Oman watakamilisha kufunga siku thalathini (30). Na nini hukumu ya aliyefunga siku thalathini kisha akasafiri kwenye nchi iliyochelewa kufunga, je afunge nao na saumu yake iwe ni siku thalathini na moja (31) au afutari (afungue)?

Jawabu: Ikiwa amefunga siku ishirini na tisa (29) kisha akasafiri kwenye nchi watu wake wametangulia kufunga siku moja, na kufunga kwao kulithibitika kwa ushahidi uliokuwa hauna shaka basi afungue (ale) siku ya Eid yao. Ama ikiwa saumu yao na kufungua kwao ni kwa kufuata watu wa nchi nyingine, kama inavyofanyika siku hizi, basi akamilishe saumu yake mpaka ikamilike faridha hiyo kwa kuona mwezi.  Na akiwa amefunga siku thalathini na ikawa ameuona mwezi yeye mwenyewe ulipoingia mwezi wa ramadhani na akafunga kwa kuona kwake mwezi au kafunga kwa ushahidi wa watu waaminifu kuwa wao wameushuhudia mwezi, na ikawa ushahidi wao haujatiliwa shaka basi, haitakikani azidishe juu ya siku thalathini ikiwa atasafiri kwenye nchi iliyochelewa kufunga. Na akajibu Shk: Ahmed Al-Khalily suali lililofanana na hili:

Ikiwa mtu amefunga kwenye nchi kwa ushahidi uliokamilika katika kuonekana kwa mwezi katika nchi hiyo, kisha akasafiri kwenye nchi iliochelewa kufunga kwa kuto onekana mwezi, basi hana isipokuwa atimize siku thalathini tu, kwa ajili saumu haizidi siku thalathini (yaani saumu haiwezekani ikawa siku thalathini na moja). Ama ikiwa ramadhani imeingia katika nchi aliyoanzia ramadhani, bila ya kuonekana mwezi sahihi na uliothibiti, basi ni juu yake akamilishe saumu yake kama vile saumu ya watu wa nchi aliyosafiri, kwasababu kuanza kufunga kwake kulikuwa bila ya sababu iliyothibiti.  (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 
Suala 4: Atakae safiri kutoka nchini kwake na kwenda nchi nyingine iliyoitangulia nchi yake katika kuchomoza jua. Vipi inakuwa kufungua kwake wakati wa kula futari?
 
Jawabu: Atakae safiri katika nchi nyingine na huku amefunga, na baina ya hizo nchi mbili kuna tofauti katika kutoka kwa jua na kuzama kwake. Basi haitakikani afutari mpaka lizame jua katika nchi aliyo safiri ikiwa jua limetangulia kuchomoza au limechelewa kuzama katika nchi hiyo. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).
 
Suala 5:Nini afanye yule aliyefunga kwenye nchi kisha akasafiri kwenye nchi nyingine ambayo watu wake wamechelewa kufunga kwa siku moja?
 
Jawabu: Ikiwa mtu amefunga katika nchi kwa kuonekana mwezi kwa uhakika katika hiyo nchi kisha akasafiri katika nchi nyingine iliyochelewa kufunga, kwa sababu ya kutothibiti kuonekana kwa mwezi, basi hana isipokuwa atimize siku thalathini tu, kwa ajili saumu haiwezekani ikazidi siku thalathini. Ama ikiwa kuingia kwa ramadhani katika nchi alioanzia kufunga, si kwa kuonekana mwezi kwa uhakika na uthibitisho ulio wazi, basi ni juu yake akamilishe saumu yake  kama saumu ya watu wa nchi aliyosafiri (aliyokwenda), kwa sababu kuanza kufunga kwake kulianza bila ya dalili iliyothibiti kuwa mwezi umeonekana. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).
 

Suala 6:Mtu amefunga ramadhani katika nchi ya UAE, kisha akafungua siku tatu kwa sababu ya maradhi yaliyomkuta. Akarejea Oman kabla ya kumalizika mwezi wa ramadhani, akakuta kuwa saumu ya watu wa Oman wamechelewa siku moja kabla ya watu wa UAE, akaifunga ile siku. Je inawezekana aichukulie siku hiyo ya mwisho kuwa ni siku moja katika zile siku tatu alizofutari kwa sababu ya maradhi?

 
Jawabu: Inamuajibikia azifunge (azilipe) hizo siku tatu, bila ya hiyo siku moja aliyoifunga Oman kwa ajili hiyo siku inahisabika kuwa ni siku ya mwisho ya mwezi wa ramadhani. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).
 
Suala 7: Mtu amefunga nje ya nchi yake siku thalathini aliporudi baada ya hizo siku thalathini katika nchi yake, amekuta watu wanafunga siku ya mwisho ya ramadhani, je nini afanye?
 

Jawabu: Ikiwa kufunga kwake ni kwa kulithibitika kwa uhakika kuonekana kwa mwezi, basi haitakikani azidishe zaidi ya siku thalathini. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Suala 8: Mijadala imezidi kuhusu kuthibiti kuingia mwezi wa ramadhani kwa kutegemea hesabu za nyota (falak), nini haki ya ya jambo hilo? Je inawezekana mtu katika nchi fulani apinge (asifunge) saumu ya nchi jirani iliyokuwa karibu na nchi yake?

Jawabu: Amri ya kufunga na kufungua saumu ya ramadhani imeambatanishwa na jambo la kuonekana mwezi, kwani Mtume (SAW) anasema: (Fungeni kwa kuuona mwezi na fungueni kwa kuuona mwezi). Na amesema pia: (msifunge mpaka muuone mwezi, wala msifungue (msifutari) mpaka muuone mwezi, na ukifichika kwa kuzibwa na  mawingu basi kamilisheni siku thalathini).

Na ziko riwaya mbali mbali nyingine zinaingia katika njia hii nazo zote zinaonyesha kuwa kufunga na kufungua ramadhani imeambatanishwa na kuthibiti kwa kuonekana kwa mwezi, na jambo la kuuona mwezi ni jepesi kwani kila mtu anaweza kuuona mwezi mwenyewe ikiwa anaona (anayo macho), na akubali ushahidi wa atakae sema ameuona mwezi ikiwa yeye mwenyewe hajauona mwezi. Na amri ya jambo hili ni maarufu kwa watu wote wenye elimu na wasiokuwa na elimu, na linashirikiana baina ya mwanamume na mwanamke na mtoto na mkubwa na mwenye akili na mjinga na mwanachuoni na hamna tafauti baina yao. Ndio maana Mwenyezi Mungu akasahilisha (akarahisisha) sababu ambazo zimeambatanishwa kwa kuthibiti kufunga au kufungua ramadhani. Ndio ikawa kutegemea hesabu za kutizama nyota kuna jambo la kubahatisha (Take a chance), na inabainika jambo hilo kwa hadithi ya Mtume (SAW):  (Sisi ni umma uliokua haujasoma hatuandiki wala hatujui hesabu), na hili linathibiti kwa watu wengi hata kama watakuwepo wenye kuhesabu na kuandika, lakini inatazamwa hali ya watu wengi wa kawaida ambao hawawezi kuandika. Ama hesabu jambo lake ni gumu (zito) lazima wapatikane watu waliozama katika fani hiyo, na watu wengi wa kawaida haiwezekani wakawa daraja moja na waliozama katika fani ya hesabu za nyota. Kutokana na hayo tunaona kutegemea yaliyothibiti kwenye sheria ya dini kwa kuona mwezi, au ushahidi wa kweli au umashuhuri wa kuuona mwezi ambao hauna shaka ndio jambo bora. Lakini ikienea kwa watu uwongo na kusema maneno ambayo si ya haki na kuzidi kwa maneno maneno yasiokuwa na msingi kuhusu kuonekana kwa mwezi, tunaona kuwa  haikatazwi kuwa hesabu za kutizama nyota ikawa ndio njia ya kujuwa ukweli wa kuonekana mwezi kwa kujibu uwongo wa kuto onekana mwezi, itakapokuwa kuna uhakika kuwa mwezi hauwezekani ukaonekana kwa macho. Kama vile mfano wakitoa watu ushahidi kuwa wao wameuona mwezi siku ambayo mawingu yametanda kwa wingi na kila mmoja anajuwa kuwa kuonekana mwezi ni kitu hakiwezekani, basi ushahidi huu hata kama unatoka kwa mtu muadilifu kwenye dini yake unarejeshwa (unakataliwa), na wakishuhudia watu kuwa wameuona mwezi pahali ambapo si kawaida ya mwezi kuchomoza kwake, basi bila shaka ushahidi wao ni baatil, hata kama walioushuhudia ni watu waadilifu katika dini yao. Na ikithibitika kwa uhakika kuwa mwezi hauwezekani ukaonekana siku hiyo. Basi hakuna neno kutegemea utafiti wa elimu ya kutizama nyota, katika kujibu ushahidi ambao si wa kweli, hivi ndivyo tunavyo ona na tunavyo tegemea. Kutokana na hayo, ikithibiti kuonekana mwezi kwenye nchi, inawalazimika watu wa nchi jirani ambayo haina tofauti na nchi iliyoonekana mwezi masafa (umbali) unaotafautiana katika kuchomoza na kuzama kwa kujua (kutafautiana kwa nyakati- (Time zone)), na hii ndio iliyokuja katika kitabu “Al-Neel”  (Na nchi ikiwa hazija tofautiana nyakati zake, basi khilafu zake zote inawajibikia zibebane baadhi yake kwa baadhi) (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu)

 

Suala 9: Samahat Shk Ahmed Al-Khalily: Tunapata upinzani mkubwa, tunaposema kuwa ni lazima kila nchi ifunge kwa kutegemea kuona mwezi katika nchi hiyo, na haitakikani kufuata nchi nyingine kuwa wao wamefunga na sisi tufunge, na labda hoja wanazozitoa kuwa nchi fulani ndio bora katika kuwakilisha uislamu kwa ajili ya daraja juu ya nchi nyingine zote ulimwenguni. Je unaweza kututatulia (kutufafanulia) matatizo haya?

Jawabu: Kufunga na kufungua kumeambatanishwa na kuonekana kwa mwezi, kwa dalili ya ubainisho ulio wazi katika sheria, kwani Mtume (SAW) amesema: (Fungeni kwa kuuona mwezi na fungueni kwa kuuona mwezi, na ukifichika kwa kuzibwa na mawingu basi kamilisheni siku thalathini), na hii hadithi imekuja kwa njia za riwaya nyingi sana, na matamko mbalimbali lakini zote zinakusudio moja. Na kuonekana kwa mwezi kuna tafautiana kutokana na tofauti ya kuchomoza na kuzama kwa jua katika kila nchi, kwa hiyo haiwezekani kuthibitisha kuwa mwezi umeonekana nchi fulani, ambayo kuchomoza na kuzama kwa jua kunaleta tofauti ya usiku na mchana, au kutangulia na kuchelewa, au kwa kuongezeka au kupunguzika urefu wa usiku na mchana. Ndio ikawa kuambatanika huku kwa kuonekana mwezi ndio hukumu ya kuthibiti kuingia ramadhani ikiwa hakuna linalokataza hukumu hii isichukuliwe, na khitilafu inajipinga katika kuhakikisha, kwani sala haitafautiani na saumu, na kila moja baina yao (sala na saumu) limeambatanishwa na jambo la mazingara nalo ni wakati. Na sala ya adhuhuri ime ambatanishwa kwa kuaza kuondoka jua wakati wa adhuhuri, na sala ya Al-Asri ni kuwa kivuli cha kila kitu ni kadiri ya hicho kitu baada ya kadiri ya kuondoka juu yake jua wakati wa Al-Asri,na sala ya magharibi ni kuzama kwa jua wakati Al-Maghrib, na sala ya Ishaa ni kuondoka wekundu wa jua na kuingia giza wakati wa Al-ishaa, na sala ya Al-fajiri ni kuchomoza kwa alfajiri iliyo ya ukweli wakati wa Al-Fajr. Na hili jambo linatabirika (linakubalika) kwa kila sehemu peke yake, wala haijuzu (haifai) watu wa nchi fulani wasali adhuhuri pale nilapo ondoka jua katika nchi ambayo si yao (yaani haifai watu wa nchi fulani wasali adhuhuri ikiwa wakati wa adhuhuri umefika katika nchi nyingine na si katika nchi yao), au wasali magharibi pale linapo anza kuzama jua wakati wa magharibi katika nchi nyingine, na kuendelea. Na ikiwa nchi iliochomoza jua na kuzama jua ndio nchi inayo takikana kuwakilisha uislamu (waislamu) kwa anavyo ona mwenye kusali basi pia saumu, kwani madai baadhi ya nchi kuwa wao ndio bora kuwakilisha uislamu si kweli. Hakika uislamu una wakilishwa popote unapokuwepo. Na nililolitaja kuhusu jambo la saumu ndio lililotajwa na sheria ya dini na wakalifanyia kazi wafuasi wote wema wa kiislamu, na dalili ya jambo hili ni lile lililotajwa na Imam muslim na watu wa Sunaa (As’haab Al-Sunnan), kuwa Kuraiyb amesema: Amenituma umm Al-fadhl bint Al-haarith mama yake Abdullahi bin Abas kwenda kwa Muawiya Shaam(Syria), ukaonekana mwezi wa ramadhani na mimi niko Shaam, nilipo mmalizia haja yake na niliporejea Madina Abdulhahi bin Abas akaniuliza : Lini mume uona mwezi? Nika mwambia : Tumeuona usiku wa kuamkia Ijumaa, akasema je wewe umeuona? Nikamjibu: ndio, na watu wote wameuona wakafunga na Muawiya pia akafunga. Akasema: lakini sisi tumeuona usiku wa Jumamosi , na bado tunaendelea kufunga mpaka tuone mwezi au tukamilishe siku thalathini.Nikamwambia je haitoshi kuona mwezi Muawiya na kufunga kwake? Akasema: Hapana, hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) - hadithi hii inaonyesha uwazi wa hukumu hii. Na kusema sahaba AMETUAMRISHA MTUME (SAW), inahukumu ya kuinua jambo kwa kukubaliana ulamaa wote wa hadithi, na ikiwa jambo hilo limetokea baina ya madina na Shaam na hali ya kuwa zimekaribiana, vipi nchi ambazo masafa yao yako mbali kupita kiasi?  Na jambo ambalo mumelichukua katika kutekeleza ibada yenu, ndilo la haki, wala msifuate yale wanayo yachukua majahili kwa kufananisha mambo na kuleta mparaganyiko. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu)

Akajibu Shk Jawabu jingine: Asili ya kufunga na kufungua ni kuona mwezi au kutimiza siku thalathini. Na zime miminika riwaya nyingi kuhusu jambo hili, na wakategemea riwaya hizo wafuasi wa mtume na wafuasi wa masahaba. Na inapokua kuona mwezi kwa macho moja kwa moja ni kitu kizito, mpaka inakuwa tabu kuuona mwezi kwa wingi wa mawingu basi haina neno kutegemea vyombo vya kisasa vinavyo aminika. Sharti viwe chini ya mikono ya waislamu au chini ya yule mwenye ujuzi wa kuleta dalili juu ya watu kuhusu kufunga saumu au kufungua saumu. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu)

 

Suala 10: Sisi wanafunzi tunasoma nnje ya nchi (India), na hatujui lini tufunge ramadhani, kwa ajili waislamu wa huku wanafunga ima kwa kufuata Saudi Arabia au calendar bila ya kutizama mwezi. Nini tufanye?
Jawabu: Ni juu yenu mufunge na mufungue kwa kutegemea kuona mwezi katika nchi mulio kuwepo kama mnavyo sali kwa kutegemea nyakati zake. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu)

 

Suala 11: Mtu ameamka hakufunga siku ya mwanzo ya ramadhani kwa kutojuwa kuwa mwezi umeonekana, kisha akajuwa kuwa mwezi umeonekana jana, je inamjuzia kuifunga hiyo siku (yaani ajizuwie kula na aendelee na saumu ya hiyo siku)?
Jawabu:  Kwa ajili yeye ameamka hali ya kuwa hakufunga, basi ni juu yake ailipe hiyo siku na hili halina khilafu baina ya ulamaa. Kuna khilafu akiwa kafunga hiyo siku, kuwa ni ramadhani basi yeye amefunga kwa ajili ya ramadhani, na ikiwa sio ramadhani basi amefunga ihtiyaatt, baadhi ya wanavyuoni wametosheka na kufunga kwake siku hiyo, na baadhi yao hawajatosheka na funga yake hiyo, kwani lenye nguvu (linalotegemewa) ni  kuto tosheka, kwa kuthibiti hadithi ya Mtume (SAW) kukataza mtu kufunga siku ambayo imetiliwa shaka. Na hadithi zilizotolewa juu ya jambo hili ni nyingi moja wapo, kusema kwake mtume (SAW): (msifunge mpaka muuone mwezi, wala msifutari mpaka muuone mwezi), Mtume ameiambatanisha saumu na kuonekana kwa mwezi, na kukataza kwake kufunga mpaka uonekane mwezi na kukataza kwake watu wasifutari mpaka wauone mwezi. Na katika jambo hili kunaonyesha kwa kuhakikisha kuwa kufunga siku hiyo ni haramu. Pia kwa kuthibiti kuwa Mtume (SAW) amekataza kutanguliza kufunga siku au siku mbili kabla ya ramadhani. Lakini imependezewa kuwa watu wajizuwie na kula ikiwa kuna mawingu mpaka ije habari kutoka sehemu za mbali, nako ni kurudi wachungaji wa wanyama mabondeni kwa kutegemea labda watapata habari kutoka kwao ambayo itatuliza nyoyo zao, na inakubalika na akili na moyo kuwa wameuona mwezi kwa kushuhudia wao wenyewe. Na kwa ajili inakatazwa kufunga siku hiyo kwa dalili yenye nguvu, ni bora asi itegemee saumu ya siku hiyo kwa kuchukuwa nafasi(chance), kwa ajili saumu ni ibada inasimama na nia ambayo haina shaka si kwa nia yenye shaka basi asitosheke na saumu ya siku hiyo. Ikiwa ameamka na nia ya saumu ikiwa siku hiyo ni ramadhani, basi siku hiyo ni saumu ya ramadhani na ikiwa si ramadhani basi funga ya siku hiyo ni ihtiyaatt. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu)