|

FADHILA ZA KUMI LA
MWISHO
Assalaamu 'alaykum warahmatullah wabarakaatuh
Wapenzi Waslamu:
Alhamdulilal
tunamshukuru Allah aliyetuwezesha kuifunga Saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani
kwa wakati uliopita, Na hivi sasa waislamu wanalisubiri kwa hamu fadhila za kumi
la mwisho la mwezi huu, siku kumi ambazo hupatika ndani yake kheri nyingi, ndani
yake kuna usiku ambao ni bora kuliko ibada za miezi elfu, (miaka 83).
Kasema Allah
katika Suratil Qadr:
(إنا أنزلناه في ليلة القدر ، وما أدراك ما ليلة
القدر، ليلة القدر خير من ألف شهر، تنزل الملائكة والروح فيها بإذن ربهم من كل أمر،
سلام هي حتى مطلع الفجر)
(Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani katika
Laylatul Qadri, Usiku wa Cheo Kitukufu * Na nini kitacho kujuulisha nini Laylatul
Qadri? * Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu. * Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo
kwa idhini ya Mola wao Mlezi kwa kila jambo. * Amani usiku huo mpaka mapambazuko ya
alfajiri).
Ndio maana bwana Mtume
(S.A.W) akatufundisha suna moja muhimu, ambayo hivi sasa watu wengi sana
wameiacha, nayo ni suna ya (Itikafu) kulazimu msikiti na kukaa ndani yake
muda wa hizi siku kumi ili kupata fadhila, kuacha kulala sana na kula sana
na kuwaacha watoto kidogo kwa ajili ya Alla subhanahu wataala, kwa kutaka
kupata fadhila za usiku huu mtukufu wa (LAYLATUL QADR).
Muislamu akijitahidi
kufanya ibada katika usiku huu, kwa kusali sana na kusoma kuraan na
kumdhukuru Allah na kufanya vitendo vingeni vya kheri kama kuwalisha
masikini na kuwatazama wanaohitaji katika waislamu wenzake, basi huwenda
akapata fadhila za usiku huu, bila kuona ishara zozote zile kama
wanavyoitakidi watu wengi ya kuwa lazima eti uone taa inameremeta kama
karabai au uone maajabu fulani, Maneno haya yote hayana dalili sahihi kuwa
lazima yatokezee hayo, wewe amka tu na ufanye ibada na Allah ndie mwenye
kujua siri ya usiku huu.
Ndio maana siku yake
maalumu ikafichwa asiijuwe mtu, hata Bwana Mtume S.A.W alibainishiwa wakati
wake, lakini hakuchukuwa muda hapo hapo akaisahau, kwa maana tunatakiwa
kujitahidi katika zile siku muki zote za mwisho katika Mwezi huu mtukufu wa
Ramadhani.
Imepokelewa kutoka kwa
Mtume S.A.W hadithi isemayo:
من قام ليلة القدر إيمانا غفر له ما تقدم من
ذنبه
"Atakae simama usiku wa Laylatul
Qadr kwa kufanya ibada kwa imani kamili, basi hufutiwa madhambi yake yote
yaliyotangulia,"
Na tuchukue mfano mzuri kwa bwana wetu
S.A.W katika kutenda ibada, alikuwa S.A.W zikifika siku za kumi la mwisho
basi hujitayarisha na kuingia msikitini kwa niya ya Itikafu, na kufanya
ibada. Mama Aisha Radhi za Allah ziwe juu yake alimuuliza Mtume S.A.W dua
gani nzuri kusoma katika usiku huu, akamjibu sema:
اللهم انك عفو تحب العفو فاعف عني
Waislamu, hii ni fursa
kubwa kwa kila mwenye kutaka kujikurubisha kwa Mola wake, ni njia pekee
ambayo humsaidia kila mwenye kutaka kurudi kwa Mwenyezi Mungu. Hujuwi kama
utaishi mpaka mwakani ili uweze kufunga tena, kwa nini tunachelewesha tawba.
|