KUJIANDAA NA HIJA

 

Mwenye kutaka kuhiji anatakiwa afanye mambo kadha kabla kuingia safarini, nayo ni:

1. Kumtakasia nia Allah aliyetukuka na kutakasika; kwani Allah hapokei ila kilichokuwa kwa ajili yake pekee.

) وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاء وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ وَذَلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ(

{Wala hawakuamrishwa ila kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia dini, waache dini za upotofu, na wasimamishe sala na kutoa zaka, na hiyo ndiyo dini iliyo sawa} [Albayyinah, 5]

) أَلَا لِلَّهِ الدِّينُ الْخَالِصُ(

{Mwenyezi Mungu ndiye wa kutakasiwa dini bila kushirikishwa} [Az-zumar, 3]

2.  Toba ya kweli kutokana na kila kosa alilofanya ili aje kwa Mola wake akiwa msafi wa moyo.

3.  Awaachie wanaomlazimu matumizi ya lazima hadi kurudi kwake. Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie - anasema: “Ni kosa la kumtosha mtu kuwatupa waliomlazimu.” Ameipokea Bukhari.

4.  Ajichukulie mahitaji ya safari ya kutosheleza ili abaki katika tabia ya kupendeza. Kutoka kwa Ibnu Abbas – Allah awaridhie – amesema: Watu wa Yemen walikuwa wakihiji na hawachukui mahitaji ya safari, na wakisema: Sisi ndio tunaomtegemea Allah. Wakifika Maka huwaomba watu. Allah Mtukufu akateremsha kauli Yake: “Na jichukulieni mahitaji ya safari, kwani mahitaji bora ya safari ni ucha-Mungu.” Ameipokea Bukhari na Abu Daud.

5.  Alipe madeni yake, arudishe alivyoazima na amana za watu, na atokane na kila jukumu lililo juu yake; kutokana na kauli ya Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie: “Nafsi ya Muumini (aliyekufa) imewekwa rehani” – na katika riwaya moja “imetundikwa - kwa deni lake mpaka alipiwe.” Ameipokea Tirmidhi akaihasanisha na Ibnu Majah.

6.      Aandike wasia wake na haki zilizomlazimu. Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie anasema: “Si halali kwa mtu Muislamu aliye na kitu cha kuusia kulala siku mbili ila na wasia wake umeandikwa, uko kichwani kwake.” Ameipokea Rabiu, Bukhari na Muslim.

7. Awatake radhi watu wa nyumbani kwake, jamaa zake, jirani zake na wenzake, na awaage anapoondoka.

8. Ajifunze vipi kuhiji; kwani ibada haisihi kwa asiyeijua. Akichukua kitabu kilichokusanya yanayohusu hija ni bora.

9.  Afuatane na watu wema watakaomsaidia kutekeleza ibada za hija.

10. Ajitahidi matumizi yake yawe ya halali yasiyo na shaka.

11. Inapendelewa safari yake iwe siku ya Alkhamisi; kwani imekuja kwenye Sahihi Mbili kutoka kwa Kaab bin Malik - Allah amridhie – amesema: “Mara chache Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie – aliingia safarini siku isiyokuwa Alkhamisi; ikiwa imempita basi ni siku ya Jumatatu; maana ndiyo siku aliyohama Mtume wa Allah - rehema za Allah na amani zimshukie – kutoka Maka.”

12. Wamempendelea baadhi ya wanazuoni anaposafiri aiage nyumba yake kwa rakaa mbili na aombe dua ya safari.

 

Copyright ©2004  Uislam.net