|
Baada kulipiga Jamra la
Aqaba mwenye kuhiji atachinja mnyama wake wa hadyi ili kumfuata Mtume -
rehema za Allah na amani zimshukie.
Kinachochinjwa huwa
ngamia au n`gombe au kondoo au mbuzi. Kondoo au mbuzi mmoja hutosheleza kwa
mtu mmoja ikiwa ametimiza mwaka, na kuna kauli miaka miwili. N`gombe
akiingia mwaka wa nne na ngamia akiingia mwaka wa sita hutosheleza kwa watu
saba.
ö
Kuchinja kuliko wajibu
huwa kwa mfanya-tamat-tuu na mfanya-qiraanu.
ö
Mnyama huyo huchinjwa
ndani ya eneo la Haram.
ö
Inapendelewa amchinje
mwenye kuhiji mwenyewe akiweza.
ö
Anapendelewa ale sehemu
ya nyama yake na atoe sadaka iliyobaki.
ö
Mfanya-ifraadu
hawajibiki kuchinja.
MAZINGATIO:
Iwapo amenunua mnyama wa
kuchinja na kwa ajili ya msongamano hakutowa thamani basi haitamwajibikia
kumrudisha, lakini atapaswa ikiwa hamjui mwenyewe aigawe thamani yake kwa
mafakiri.
Haimjuzii mwenye kuhiji
kununua mnyama wa kuchinja kwa njia ya Benki ya Kiislamu kwasababu kutokana
na ihramu kwa mfanya-tamat-tuu kunategemea kuchinja, naye hajui wakati gani
atachinjiwa, na kutokana na shaka ya hilo.
Haijuzu kumchinja mnyama
wa hadyi kabla wakati wake na vilevile haijuzu pasipo mahali pake. Wakati
wake ni siku ya kuchinja (10 Dhul-hija) na kwa hiyo atakaechinja kabla yake
basi na achinje tena.
Asipoweza mwenye kuhiji
kuchinja siku ya kuchinja atabaki na ihramu yake mpaka achinje kwasababu
haisihi kutokana na ihramu kabla kuchinja.
Asiyeweza kumpata mnyama
wa hadyi itampasa afunge siku ya tarehe: sita, saba, na nane Dhul-hija kisha
afunge siku saba baada kumaliza amali za hija.
Inajuzu kuchinja mnyama
wa hadyi katika sehemu zote za Haram na sio eneo la Mina pekee kwani hii ni
kauli ya baadhi ya wanazuoni tu.
Haijuzu kupewa nyama
mchinjaji kwa ajili ya uchinjaji bali ampe ujira wake mbali.
Mwenye kufanya umra
katika miezi ya hija kisha akarudi nchini kwake na akaazimia kuhiji kwa
ifraadu (kufanya hija pekee) haitamlazimu kuchinja kwasababu ya kutokuwa
katika hukumu ya mfanya-tamat-tuu.
KUTOKANA NA IHRAMU YA HIJA
Akimaliza
mwenye kuhiji siku ya kuchinja (10 Dhulhija) kupiga jamra na kuchinja
atatokana na ihramu yake kwa kunyoa au kupunguza nywele. Dalili ya hayo ni
hadithi ya Anas “kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema za Allah na amani
zimshukie -
alifika Mina akaja kwenye Jamra akalipiga kisha akenda alikofikia katika
Mina akachinja, kisha akamwambia kinyozi: ‘Ondoa’,
akaonyesha upande wake wa kulia wa kichwa kisha wa kushoto.”
Imepokewa na Muslim na Ahmad.
Mwanamke
haruhusiwi kunyoa kwa ajili ya umra wala hija, bali anapunguza kadiri ya
inchi moja. Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie
- amesema: “Na linalowapasa wanawake ni
kupunguza tu nywele zao.” Imepokewa na Abu Daud.
Kunyoa ni bora kuliko kupunguza, kwasababu Mwenyezi Mungu
amekutaja mwanzo katika kauli Yake Aliyetukuka:
)
مُحَلِّقِينَ رُؤُوسَكُمْ
وَمُقَصِّرِينَ(
{mkinyoa vichwa
vyenu na mkipunguza nywele} [Al-fat`h, 27], na
kwasababu Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie - amesema:
“Allah awarehemu wenye kunyoa”
mara tatu, pakasemwa: ‘na wenye kupunguza?’, akasema:
“Na wenye kupunguza.”
Imepokewa na Rabiu, Bukhari na Muslim.
Yanamhalalikia
mwenye kuhiji baada kunyoa (au kupunguza) yale yote aliyozuiliwa kwasababu
ya ihramu isipokuwa mke na kuwinda. Hali hii huitwa “tahal-lul as-ghar”
yaani kutokana na ihramu kudogo. Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie
- amesema: “Mkishapiga jamra na kunyoa itakuwa
halali kweni kila kitu ila wake zenu.” Imepokewa na Nasaaiy, Ahmed na
Baihaqiy.
|