May 292011
 

رعاية اليتيم في الإسلام

MALEZI YA MAYATIMA KATIKA UISLAMU

بسم الله الرحمن الرحيم

Baada ya kumshukuru ALLAH (SW) kama anavyostahiki kushukuriwa, sala na salamu zimfikie mjumbe wake Sayyidina Muhammad (saw) pamoja na Masaba wake na kila anaefuata njia yake kwa wema mpaka siku ya malipo.

Enyi Waja wa ALLAH !

Mcheni ALLAH Mtukufu na ikumbukeni kauli yake isemayo :

( يا أيّها الناّس اتّقوا ربّكم الّذي خلقكم من نفس واحدة وخلق منها زوجها وبثّ منهما رجالا كثيرا ونساء واتّقوا الله الّذي تساءلون به والأرحام إنّ الله كان عليكم رقيبا )

“Enyi watu ! Mcheni Mola wenu ambae amekuumbeni kutokana na nafsi moja. Na akaumba mkewe kutokana na nafsi ile ile. Na akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka katika wawili hao. Na mcheni ALLAH ambaye kwaye mnaombana na muwatazame jamaa. Hakika ALLAH ni mlinzi juu yenu”.

Tambueni kuwa Uislamu umetukuza haki za madhaifu kama vile masikini, mafakiri, vizuka na mayatima, kwani katika hayo kuna taathira kubwa katika nafsi na hisia zao, hasa kwa yatima alieondokewa na wazee wake wawili au mmoja wao. Huyu ana haja kubwa ya kuonewa huruma, kusaidiwa na kuongozwa tangu udogoni na kufunzwa adabu na tabia njema. Na ikiwa atakosa haya, bila ya shaka atainukia katika tabia mbaya na atakuwa na mtazamo wa chuki kwa jamii yake kwa sababu ya kumtupa na kumdharau.

Ndugu Waislamu:

Uislamu umekuwa mbele katika kumlinda yatima kimalezi na kumdhaminia maisha yake ili ainukie akiwa ni kiungo chenye manufaa katika jamii yake.

Qur-ani inatuhimiza kulinda haki za yatima na inatukataza kumdhalilisha na kumdharau, na inatuonesha kuwa kumdharau yatima ni dalili ya kukadhibisha siku ya malipo.

Anasema ALLAH (SW):

( فأمّا اليتيم فلا تقهر )

“ Basi usimuonee yatima”.

Na amesema vile vile:

( أرأيت الّذي يكذّب بالدّين  .  فذلك الّذي يدعّ اليتيم )

“ Jee umemuona yule anaekadhibisha dini ? Huyo ni yule anaemsukuma yatima”.

Zimekuja hadithi nyingi za Mtume (saw) zinazohimiza kuwatazama mayatima, na zikawabashiria wawatunzao mayatima kwa wema kuwa watakuwa pamoja na Mtume (saw) huko peponi.

Amesema Mtume (saw):

(( أنا وكافل اليتيم في الجنّة هكذا ، وأشار بأصابعه السّبّابة والوسطي وفرّج بينهما ))

“ Mimi na mwenye kumtazama yatima huko peponi tuko hivi, akiashiria kwa vidole vyake cha shahada na cha kati na kuvipambanua baina yake”.

Amesema vile vile:

(( كافل اليتيم له أو لغيره أنا وهو كهاتين في الجنّة ))

“Mwenye kumtazama yatima wake au wa mwenzake basi mimi na yeye tutakuwa pamoja peponi kama vidole viwili” .

Na amesema:

(( من قبض يتيما من بين المسلمين إلى طعامه وشرابه أدخله الله الجنّة البتّة إلا أن يعمل ذنبا لا يغفر له ))

“ Atakaemchukua yatima baina ya waislamu wawili kwa kumlisha na kumnywesha, basi  bila ya shaka ALLAH atamuingiza peponi, isipokuwa awe amefanya dhambi zisosameheka”.

Na amesema:

(( خير بيت في المسلمين بيت فيه يتيم يحسن إليه ، وشرّ بيت في المسلمين بيت فيه يتيم يساء إليه ))

“ Nyumba ilio bora kwa Waislamu ni nyumba yenye yatima anaefanyiwa wema, na nyumba yenye shari kwa Waislamu ni nyumba yenye yatima anaefanyiwa uovu”.

Na imepokewa kuwa Mtume (saw) amesema:

“Mimi ni mtu wa mwanzo ataefunguwa mlango wa pepo, isipokuwa nitamuona mwanamke anataka kunitangulia, nami nitamuuliza : unataka nini? na wewe nani ? Nae atajibu : mimi ni mwanamke niliekuwa nikiwatizama mayatima wangu”.

Enyi Waja wa ALLAH:

Hakika haki za mayatima kimalezi na katika kuwatunzia mali zao zimetiliwa mkazo sana na Qur-ani na katika sunna za Mtume (saw). Na ilipoteremka amri ya kuchunga haki hizo katika Qur-ani, Masahaba waliingiwa na wasiwasi katika utekelazaji wake na wakamuuliza Mtume (saw) juu ya hayo, ikateremka kauli ya ALLAH (SW) isemayo :

( ويسألونك عن اليتامى قل إصلاح لهم خير وإن تخالطوهم فإخوانكم والله يعلم المفسد من المصلح ولو شاء الله لأعنتكم إنّ الله عزيز حكيم )

“ Na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema, kuwatendea wema ndio vizuri. Na kama mkichanganyika nao ( ndio wema vile vile) kwani hao ni ndugu zenu, na ALLAH anamjua fisadi na alie mwema. Hakika ALLAH ni mwenye nguvu na mwenye hikma”.

Ndugu Waislamu:

Kusimamia mambo ya mayatima ni jambo la wajibu na lenye kheri kubwa, na inampasa kila anaemlea yatima amlee kwa wema kama anavyowalea watoto wake mwenyewe, na iwapo yatima huyo atakuwa na mali basi ajiepushe kabisa na kula mali hiyo, kwani  kula mali za yatima pasi na haki ni katika madhambi makubwa.

Anasema ALLAH (SW):

( إنّ الذّين يأكلون أموال اليتامى ظلما إنّما يأكلون في بطونهم نارا وسيصلون سعيرا )

“ Hakika wale ambao wanakula mali za mayatima kwa dhulma, bila ya shaka wanakula moto katika matumbo yao, na wataungua katika huo moto ( wa Jahannamu ) uwakao”.

Na anasema Mtume (saw):

(( اجتنبوا السّبع الموبقات  – أي المهلكات – قالوا يا رسول الله وما هنّ ؟ قال : الشّرك بالله ، السّحر ، وقتل النّفس التي حرّم الله إلاّ بالحقّ ، وأكل الرّبا ، وأكل مال اليتيم ، والتولي يوم الزّحف ، وقذف المحصنات الغافلات المؤمنات ))

“ Jiepusheni na madhambi saba yaangamizayo. Wakasema ni yepi hayo ewe Mjumbe wa ALLAH ? Akasema : kumshirikisha ALLAH, uchawi, kuiuwa nafsi ambayo ALLAH ameharamisha kuiuwa ila kwa haki, kula riba, kula mali za yatima, kukimbia vitani na kuwasingizia mambo machafu wanawake wa kiislamu wenye heshima zao”.

Na imekuja katika kisa cha Miiraj wakati Mtume (saw) alipopandishwa mbinguni na kuoneshwa mambo ya huko ya kuwa, aliwaona watu wananyofoa nywele zao na wengine wanachukua mawe na kuyatia katika midomo yao kisha hutokea katika tupu zao. Akamuuliza Jibril (as) nani wale ? Jibril akamjibu : “hawa ni wale waliokula mali za mayatima kwa dhulma, hakika wanakula moto ndani ya matumbo yao”.

Enyi Waja wa ALLAH:

Mcheni ALLAH Mtukufu, tubieni kwake na muogopeni juu ya dhamana alizokupeni za mayatima na madhaifu, na fanyeni amali njema ili mpate kufuzu.

والسلام عليكم ورحمة الله تعالى وبركاته .

   
© 2011 Uislam Suffusion theme by Sayontan Sinha