May 292011
 

الرّحمة والتّراحم

HURUMA KWA WANAADAMU NA VIUMBE WENGINE

بسم الله الرحمن الرحيم

Baada ya kumshukuru Allah Subhana Wataala kama anavyostahiki kushukuriwa , sala na salamu zimfikie Mjumbe wake Sayyidna Muhammad s.a.w. pamoja na sahaba zake na kila anayefuata njia yake.

Umma wa Kiislamu:

Mcheni Allah Mtukufu kama ipasavyo kumcha , kwani kamba iliyo madhubuti ni uchamungu , na tambueni ya kwamba kuoneana huruma ndio dawa ya uhai , na mlango wa furaha na utulivu , ndani yake huchungwa haki na kuhifadhiwa majukumu , na pindi ikipatikana sifa ya kuhurumiana , basi nyoyo hutulia na hupatikana utulivu , na muislamu aliyekamilika imani ni yule aliye na sehemu kubwa ya huruma .

Ndugu Waislamu:

Hakika Allah ameiwajibisha nafsi yake kuwa na rehma , pale aliposema:

كتب ربّكم على نفسه الرّحمة أنّه من عمل منكم سوءا بجهالة ثمّ تاب من بعده وأصلح فأنّه غفور رحيم . / الأنعام 54

Mola wenu amejiwajibishia rehma , kwamba atakayefanya miongoni mwenu uovu kwa ujinga , kisha akatubu baada yake na akafanya wema , basi Allah atamghufiria , kwani yeye ni mwingi wa msamaha na mwingi wa rehma.

Basi rehma za Allah zinawatosheleza viumbe vyote , na huwafikia waja wote , huonekana athari yake kwa kuwepo kwao katika hii dunia , na kuneemeshwa kwa kila neema , na katika kuingizwa kwao peponi , kwani hatoingia yeyote peponi kwa amali yake tu , bali na kwa rehma zake Subhana Wataala , imekuja hadithi iliyosimuliwa na Abu Huraira radhi za Allah zimfikie amesema , amesema Mjumbe wa Allah rehma na amani zimfikie :

جعل الله الرّحمة مائة جزء ، فأمسك عنده تسعة وتسعين ، وأنزل في الأرض جزءا واحدا فمن ذلك الجزء تتراحم الخلائق ، حتّى ترفع الدّابة حافرها عن ولدها خشية أن تصيبه .

Allah ameijaaliya rehma kuwa sehemu mia , kisha akazuwiya sehemu tisiini na tisa na akaiteremsha katika dunia sehemu moja , na katika sehemu hiyo hurehemeana viumbe , mpaka mnyama hunyanyua kwato yake kwa kuchelea kumkanyaga mwanawe.

Waja wa Allah:

Hakika muislamu anatakiwa kumuiga Mtume rehma na amani zimfikie na kujipamba kwa sifa zake , anasema Allah Mtukufu:

لقد كان لكم في رسول الله أسوة حسنة لمن كان يرجو الله واليوم الآخر وذكر الله كثيرا . / الأحزاب 21

Bila shaka mnao mfano mwema kwa mtume wa Allah , kwa mwenye kumuogopa Allah na siku ya mwisho na kumtaja Allah sana.

Na Mtume s.a.w. alikuwa mwingi wa huruma juu ya kila kitu , juu ya watu na wanyama na ndege na hata wanyama pori , na Allah amemsifu kwayo pale aliposema:

لقد جاءكم رسول من أنفسكم عزيز عليه ما عنتّم حريص عليكم بالمؤمنين رءوف رحيم . / التوبة 128

Amekufikieni Mtume aliye jinsi moja na nyinyi , yanamhuzunisha yanayokutaabisheni , anakuhangaikieni . Na kwa walioamini ni mpole na mwenye huruma .

Na akamsifu pahala pengine kwa kusema:

فبما رحمة من الله لنت لهم ولو كنت فظّا غليظ القلب لانفضّوا من حولك . / آل عمران 159

Basi kwa sababu ya rehma itokayo kwa Allah umekuwa laini kwao (Ewe Muhammad) . Na kama ungekuwa mkali na mwenye moyo mgumu bila shaka wangalikukimbia.

Na katika sira yake s.a.w. yapo yanayohitaji kuzingatiwa na kuongoza katika njia za warehemevu , amepokea Abdurahman bin Abdillah kutoka kwa baba yake radhi za Allah zimfikie amesema : Tulikuwa pamoja na Mjumbe wa Allah rehma na amani juu yake  katika safari , basi tukamuona ndege anamakinda yake mawili , basi tukawachukua , naye akawa anapiga piga mbawa zake , na alipokuja Mtume s.a.w. akasema : Ni nani aliyemhuzunisha huyu kwa kumchukulia wanawe , basi mrejesheeni mwenyewe wanawe .

Na siku moja aliingia Mtume s.a.w. katika bustani ya mtu mmoja wa kiansar akamkuta ngamia ndani yake , basi huyu ngamia alipomuona Mtume s.a.w. alimsikitikia na kutokwa na machozi machoni mwake , naye Mtume s.a.w. akamkaribia na akampangusa basi akanyamaza , kisha Mtume akasema : nani mlezi wa huyu ngamia ? , pale pale akaja kijana wa kiansari akasema ni wangu Ewe Mjumbe wa Allah , akamwambia Je! Humuogopi Allah juu ya huyu mnyama aliyekupa , kwani yeye amenishitakia kuwa unamuweka na njaa na unamuudhi .

Kwa hivyo ikiwa huruma zake s.a.w. juu ya wanyama kiasi hiki , kefu kwa binaadamu? .

Ndugu Waislam:

Katika nyakati za mghafala hutoweka huruma , na inapozidi jeuri hukanyagwa chini ya miguu , na pindi watu wakiifikia hali hii , basi nafsi zao huwa ngumu na kutokwa na huruma na nyoyo zao kuwa kama mawe na wakati huo mtoto mdogo haonewi huruma kwa udogo wake , wala mzee kwa uzee wake na haonewi huruma hata mnyama asiyejua kusema , na kwa kutokana na haya hufanywa mambo si ya kawaida na uovu usiostahamilika , na kufanya hivi ni katika upotovu uliodhahiri , anasema Allah Mtukufu kutubainishia hayo pale aliposema :

فكأيّن من قرية أهلكناها وهي ظالمة فهي خاوية على عروشها وبئر معطّلة وقصر مشيد ، أفلم يسيروا في الأرض فتكون لهم قلوب يعقلون بها أو آذان يسمعون بها فإنّها لا تعمى الأبصار ولكن تعمى القلوب الّتي في الصّدور . الحج / 45-46

Miji mingapi tuliiangamiza iliyokuwa ikidhulumu , ikaanguka juu ya mapaa yake , na visima vingapi vilivyoachwa , na majumba yaliyokuwa madhubuti ? . Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate akili za kufahamia , au masikio ya kusikilia ? kwa hakika macho hayapofoki  , lakini nyoyo ambazo zimo vifuani ndizo zinazopofoka.

Na mpaka hivi sasa ingali bado ujahilia unaendeleza ukatili wake , kwani tunaona dhiki na shida zinavyoandama nchi masikini , na tunasikia vilio vya waliofikwa na njaa na umasikini katika huu ulimwengu , na tunaona mambo haya ya kusikitisha katika nchi masikini bila ya kuchukuliwa hatua yoyote , basi kwa nini wanaadamu hawaoneani huruma? , ili ipatikane amani na kushikamana kwa pamoja na kuishi kwa furaha , anasema Allah Mtukufu :

ولو أنّ أهل القرى آمنوا واتّقوا لفتحنا عليهم بركات من السّماء والأرض ولكن كذّبوا فأخذناهم بما كانوا يكسبون . / الأعراف 96

Na lau kama watu wa miji wangaliamini na kuogopa , kwa yakini tungaliwafungulia baraka za mbingu na ardhi . Lakini walikadhibisha , tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma .

Umma wa Kiislamu:

Mcheni Allah Mtukufu , na tambueni ya kwamba uislamu ni dini ya rehma na kuoneana huruma , na Mtume wetu rehma na amani zimfikie , amekuja kwa lengo la kueneza rehma baina ya walimwengu , anasema Allah Mtukufu kuhusu ulinganio wake :

وما أرسلناك إلاّ رحمة للعالمين . / الأنبياء 107

Nasi hatukukutuma ila uwe rehma kwa walimwengu wote.

Basi na tuwe walinganiaji wenye huruma na ionekane huruma katika matendo yetu , kwa kuiga mifano ya mitume na watu wema , na kufuata amri za Allah . Na kwa yaliyoufika umma wa kiislamu hii leo huwa ni wajibu juu yetu kuzihisabu nafsi juu ya uhusiano wetu na mwenendo wetu mbele za watu ,

إنّ الله لا يغيّر ما بقوم حتّى يغيّروا ما بأنفسهم . / الرعد 11

Hakika Allah habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo katika nafsi zao .

Na mambo tunayoyaona katika zama hizi , yakiwemo uvunjaji wa haki za binaadamu na misingi ya kuhurumiana , ni mambo yanayokataliwa na uislamu na mwenye akili , kwa hivyo ni wajibu juu ya yetu umma wa kiislamu , tueneze misingi ya kuhurumiana baina yetu na tuhimizane kushikamana nayo na Allah hapotezi malipo ya mwenye kutenda amali njema .

Basi mcheni Allah ndugu waislam , na oneaneni huruma baina yenu kwani atakayemuondoshea dhiki muislamu mwenziwe naye Allah atamuondoshea dhiki katika dhiki za siku ya kiama , na Allah yu pamoja na mwenye kumsaidia mweziwe .

والسّلام عليكم ورحمة الله وبركاته .

 

   
© 2011 Uislam Suffusion theme by Sayontan Sinha