ITIKAFU

 Maana ya Itikafu katika lugha: Kushikilia kitu.

Maana ya Itikafu katika Sheria: Ni kukaa msikitini na kubaki humo kwa mkalifiwa kwa namna maalumu, ili kujikurubisha kwa Allah Mtukufu hali ya kuwa anaepuka yanayopingana na hilo.

Itikafu ilikuwapo katika Sheria za Allah zilizotangulia. Kasema Mwenyezi Mungu katika Suratil Baqarah aya ya 125:

)æóÚóåöÏúäóÇ Åöáóì ÅöÈúÑóÇåöíãó æóÅöÓúãóÇÚöíáó Ãóäú ØóåøöÑóÇ ÈóíúÊöíó áöáØøóÇÆöÝöíäó æóÇáúÚóÇßöÝöíäó æóÇáÑøõßøóÚö ÇáÓøõÌõæÏö(

“Na tulimwusia Ibrahimu na Ismaili kuwa: "Itakaseni nyumba yangu kwa ajili ya wanao izunguka kwa ku'tufu, na wanaobaki humo kwa ibada, na wanao rukuu na kusujudu”.

HUKUMU YA ITIKAFU:

Asili ya itikafu ni kuwa sunna inayopendelewa, hasa katika kumi la mwisho la Ramadhani kutokana na mafundisho ya Mtume S.A.W, tena ina fadhila kubwa. Na inawezekana itikafu kuwa wajibu - kama ikiwa ya kutekeleza nadhiri.

PAHALA PA ITIKAFU:

Inapendelewa iwe katika Msikiti wa Ijumaa, ili isimbidi kutoka kwa ajili ya sala ya Ijumaa. Ikishindikana hivyo basi iwe katika msikiti unaosaliwa Sala ya Jamaa. Isipokuwa mwanamke; yeye hukaa  itikafu pale alipopafanya pa kusalia katika nyumba yake. Na inamjuzia kukaa itikafu msikitini na Mumewe, kwa sharti awe kwenye pahala palipowekwa kwa ajili ya wanawake.

MASHARTI YA ITIKAFU:

1-    Niya: Akusudie kwa kukaa itikafu kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu S.W. na kufuata Sunna ya Mtume S.A.W pamoja na kutaraji thawabu.

2-    Saumu: Kwani itikafu haisihi bila ya kufunga.

3-    Kubaki msikitini: Kwasababu Mtume S.A.W alikuwa akikaa itikafu msikitini na haingii nyumbani kwake ila kwa haja ya kibinaadamu.

AMALI ZA MWENYE KUKAA ITIKAFU:

Kwa vile mwenye kukaa itikafu niya yake ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, basi anatakiwa atumie wakati wake kwa kufanya ibada maalumu kama sala, kusoma Qur’ani, kujifunza elimu zenye manufaa, kumdhukuru Allah na kuomba dua na maghfira. Na hakuna ubaya kwa aliye katika itikafu kuzungumza yale ambayo  hayana makosa. Kwani imepokewa kwamba Mama Safia R.A mkewe Mtume S.A.W alimtembelea Mtume S.A.W msikitini akiwa katika itikafu, akazungumza naye muda, kisha akainuka arudi, Mtume akamsindikiza mpaka mlangoni mwa msikiti.

WAKATI WA ITIKAFU:

Mwenye kutaka kukaa itikafu usiku na mchana, basi aingie msikitini kabla ya magharibi (kabla ya kutua jua), na vile vile kwa mwenye kutaka kukaa itikafu siku kadha au mwezi. Ama akitaka kukaa itikafu mchana tu, basi aingie msikitini kabla ya kuchomoza alfajiri, na mwisho wa itikafu yake ni kutua kwa jua; asitoke kwenye itikafu kabla ya magharibi.

Na mwenye kutaka kukaa itikafu katika kumi la mwisho la Mwezi wa Ramadhani, ataingia msikitini kabla ya magharibi ya usiku wa kuamkia tarehe ishirini na moja, na atatoka baada ya kutua jua la siku ya mwisho ya Mwezi wa Ramadhani.

Inakatazwa kukaa itikafu katika siku zilizokatazwa kufunga, kama siku ya idi (siku kuu) na siku ya Shaka. Kwani katika masharti ya itikafu ni kufunga kama ilivyotangulia kutajwa.

YANAYOHARIBU ITIKAFU:

1-     Kufanya kitendo cha ndoa (Jimai) hata ikiwa usiku baada ya futari. Kasema Mwenyezi Mungu katika Suratil Baqarah aya ya: 187:

)æóáÇ ÊõÈóÇÔöÑõæåõäøó æóÃóäúÊõãú ÚóÇßöÝõæäó Ýöí ÇáúãóÓóÇÌöÏö(

(Wala msiwaingilie na hali mnakaa itikafu msikitini).

Kujitoa manii kwa makusudi pia hupewa hukumu hii; kwa hiyo mwenye kusababisha kutokwa na manii hubatilisha itikafu yake.

2-     Kuharibu Saumu: kwa kula au kunywa, au kufanya maasi – kwa kauli iliyo sahihi, au mengineyo yanayobalitisha saumu kama kutia dawa ya macho, kujitapisha kwa makusudi, n.k.

3-     Kutoka msikitini bila dharura: mwenye kufanya hivyo huharibu itikafu yake; na kuna kauli kwamba arudi na aendelee kisha alipe kwa kukaa msikitini muda kama aliotoka.

4-     Kutoka bila dharura na kuto kurudi tena.

  MASUALA TOFAUTI YANAYOHUSU ITIKAFU:

1-    Mwanamke mwenye kukaa itikafu, akipatwa na hedhi mchana, basi itikafu ya siku hiyo huharibika, na atatoka msikitini mpaka akisha tahirika atarudi na kuendeleza itikafu yake.

2-    Mwenye kukaa itikafu akijiwekea sharti ya kufanya jambo ambalo itikafu hailiruhusu, kama kwenda mazikoni au kulala nyumbani kwake, basi sharti yake hiyo ni batili kwa kauli ya wengi wa maulamaa; na kwa hiyo akilifanya  itikafu yake huharibika.

3-    Hakuna neno kwa mwenye kukaa itikafu kumtuma mtu mwengine amtekelezee haja zake na yanayohusu maslahi ya maisha yake. Vile vile anaweza kufungisha ndoa, kujitia manukato na kujisafisha mwili.