ISRAFU KATIKA MWEZI WA RAMADHANI

Assalaamu 'alaykum warahmatullah wabarakaatuh

Wapenzi katika Imaan:

Baada ya kuwaombea kila la kheri na baraka katika mwezi huu mtukufu uliojaa baraka na thawabu za bure kwa mwenye kutaka, napenda kutoa mchango wangu katika masaail mbalimbali yanayohusiana na mwezi huu wenye ukarimu usio na mfano.

Katika neema kubwa za Allah kwa waja wake ni kutuneemesha neema za kila aina ambazo hatutaweza  kuziihisabu, kati ya neema hizo ni huku kuweza kupta chakula cha aina tofauti katika maladhati ya Dunia, ili kiwili wili nacho kitape nguvu ya kutenda manufaa na kumuabudu Mwenyezi Mungu. Na Uislamu umetuwekea kiwango anachotakiwa mtu ale ili siha yake isije ikamuharibikia, Subhanallah kila kitu kikipindukia mipaka basi huwa kinaleta madhara hata cha halili kama chakula. Mtume S.A.W katueleza katika Hadithi iliyotolewa na Imam Atirimidhiy kasema:

"ما ملأ آدمي وعاءا شرا من بطنه، حسْب ابن آدم لقيمات يقمن صلبه، فإن كان لا محالة فثلث لطعامه، وثلث لشرابه، وثلث لنفسه"

"Hakujaza mwanadamu chombo kibaya kama tumbo lake, inamtosha binadamu tonge kidogo zikamsaidia uhai wake, kama hakuna budi basi aweke nafasi ya  thuluthi chakula na thuluthi maji na thuluthi aweke za pumzi".

Waislamu, mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa Ibada na kuomba maghfira, ni mwezi wa kujikaribisha kwa Allah na kuutumia wakati katika mambo ya kheri, kwani thawabu hizidishwa mara nyingi kama mnavyofahamu.

Lakini leo hii watu wengi wanadhani kuwa Ramadhani ni mwezi wa mavyakula na hupikwa vyakula ambayo hata havijulikani wala havina jina, marangi tofauti na ndio watu baada ya kutoka ramadhani na siha njema kama inavyotakiwa, basi wengine hutoka matumbo yanawauma na weshazidisha uzito kilo fulani.

Mwenyezi Mungu kakataza Israfu katika maisha yote, kwa hivyo kufanya israfu katika mwezi wa Ramadhani dhambi hizidi, kama vile thawadu zinapozidishwa. Leo hii kuna watu vyakula hawana, wala nguo za kuvaa za siku kuu hawajapata, laiti pesa hizi za maakulati wanapewa masikini bisi zingaliwafaa katika mambo yao. Lakini mtu ana khiyari kutupa chakula katika jaa, jirani yake masikini hajui nini anachokila.

Na Allah (SW) amekataza kutumia mali kuliko haja ya mtu kwa kusema:

( وكلوا واشربوا ولا تسرفوا إنّه لا يحبّ المسرفين )

“ Na kuleni (vizuri) na kunyweni (vizuri) lakini msipite kiasi tu. Hakika yeye (ALLAH) hawapendi wapitao kiasi”.

Waislamu sisi tuwe ni mfano mwema kwa waliobakia, ili wasihisi kwamba uislamu ni Dini ya Israfu na kutumia mali katika mambo yasiyokuwa na haja.

والــســلام عـلـيـكـم ورحـمـة اللّه وبـركــاتــه