FATWA ZA WANAWAKE

  Haijuzu kwa mwanamke kwenda hija au umra bila mahramu. Ikiwa hakupata mahramu wa kufuatana naye ameruhusiwa kusafiri kwa ajili ya hija ya fardhi pamoja na watu wema wanaofuatana na wake zao au wanawake walio mahramu zao.

  Mwanamke akipata hedhi kabla kutufu tawafu ya umra naye amenuia kuhiji kwa kutanguliza umra kabla hija (tamat-tuu) na hakutoharika kabla siku ya tarwiya (8 Dhul-hija), atabadili siku hiyo nia yake anuie kuchanganya hija na umra (qiraanu) - aingize hija kwenye umra, na itamtosha tawafu moja na sai moja kwa hija na umra yake.

   Masharti ya hija kwa mwanamke hayatafautiani na masharti ya hija kwa mwanamme; anachozidi mwanamke ni sharti moja tu, nayo ni kuwa afuatane na mumewe au mahramu yake kwa ajili ya uharamu wa kusafiri peke yake.

   Mwanamke mwenye kuhiji haimlazimu kusali katika Misikiti Miwili Mitukufu (wa Maka na wa Madina); hilo linapendelewa kwake iwapo ataepuka msongamano na wanaume na hatakuwa katika hali inayoogopewa mshawishiko. Yakikosekana masharti mawili haya kwake basi sala yake ni katika nyumba aliyomo.

  Kubadilisha nguo kwa mwanamke hakuathiri ihramu yake.

   Ziara ya makaburi ya Masahaba na ya Watu wa nyumba ya Mtume - rehema za Allah na amani zimshukie - ni jambo lenye hitilafu; na kujuzu kwa hilo ni kwa sharti ziara iwe kwa ajili ya mazingatio ya mauti na isiwe na kilio cha sauti wala mengineyo katika yaliyokatazwa.

   Haijuzu kwa mwanamke kufunika uso wake; akiufunika makusudi itamlazimu kuchinja; na ikiwa kwa kukosea au kusahau itampasa ajifunue haraka akikumbuka. Vilevile anazuiwa kuvaa glavu mikononi.

   Mwanamke inamwajibikia kupunguza katika ncha za nywele zake wakati wa kutokana na ihramu kadiri ya upana wa vidole viwili, na kuna kauli kadiri ya upana wa vidole vinne. Asipofanya akatokana na ihramu bila hilo itamlazimu kuchinja.

  Inamjuzia mwanamke kumwajiri mtu ampigie vijiwe jamra ikibidi.

  Inamjuzia mwanamke kutumia vidonge vya kuzuia hedhi kwa ajili ya dharura ya kuhiji au  kufanya umra.

   Mwanamke akipata habari ya kifo cha mumewe akiwa kwenye hija itamwajibikia kutimiza ibada za hija yake na haimjuzii kuiacha baada ya kuwa kishahirimia.

 

 

Copyright © 2004 uislamu.net