TOHARA NA USAFI 

 

Suala: Ikiwa mtu anayakini kuwepo najasa (uchafu) kwenye sehemu ndogo ya mkeka wa kusalia. Je inajuzu kusali juu ya mkeka huo?
Jawabu: Ikiwa mkeka huo umetemgenezwa na makuti ya mtende kama inavyojulikana hapa Oman kuwa kuti hizo hazijakamata (hazija wasiliana), basi haidhuru kuwa na najasa katika upande wowote ule wa mkeka ikiwa mtu hatasali juu ya upande huo uliongia najasa. Ama ikiwa mkeka wenyewe ni kama busati basi kuingia najasa hata kama ni sehemu ndogo tu katika mkeka hu haifai kusalia kwa kuwasiliana nyuzi za hilo busati. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Suala: Je falaj (mchirizi unaotembea maji) inaingia najasa ikiwa majusi (mshirikina-Hindus-Bhudist) ataogolea ndani yake?

Jawabu: Imepokewa kutoka kwa Imama Al-Rabii bin Habib kupitia kwa Abi Ubaida kwa njia ya Jaber Ibn Abaas (radhi za Mola ziwe juu yao) kuwa Bwana Mtume (SAW) amesema: (Maji ni kitu tahir hakiwi najasa isipokuwa yakiingiliwa na kitu, yakabadilika rangi yake, utamu wake na harufu yake) na hii inajumuisha maji yanayotembea au maji mengi yaliyotuwa hata kama hayatembei, na kunakhilafu katika maji machache yaliyotuwa. Kutokana na hayo inaonyesha kuwa falaj hainajisiki kwa kukoga (kuogelea) majusi ndani yake.  (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Suala: Je nguo ya mwenye janaba inakuwa najisi ikiingiwa na jasho la huyo mtu? Na je nguo ya mwenye hedhi na nifas pia inakuwa najisi ikiingiwa na jasho la hawa watu wenye hedhi na nifas? 

Mwili wa mtu mwenye janaba sio najisi wa kufanya nguo inayogusa mwili huo kuwa najis, na vivo hivyo kwa mwanamke mwenye hedhi au nifas nguo zao haziwi najis kwa kuguswa na jasho lao. Na kuamrishwa watu hawa kukoga baada kuwa na janaba,hedhi na nifas si kwa ajili ya najasa waliyokuwa nayo bali ni amri ya kuabudu kama vile kuosha viungo vya udhu wakati wa kusali baada ya hadath ndogo (kufanya haja ndogo au kubwa). Na dalili juu ya jambo hili ni nyingi, moja wapo ni kuwa Mtume (SAW): Alikuwa akisali na nguo aliyokuwa amevaa wakati akiingiliana na wake zake. Na katika dalili nyingine ni pale Mtume (SAW) alipomuambia mkewe Aisha: (NAWILINI AL-KHAMRA) Nipe kitambaa cha kujifutia/kusalia. Aisha akasema mimi ninahedhi. Mtume (SAW) akamwambia: Hedhi yako haimo mikononi mwako. Na Mtume (SAW) alikuwa akilala na wakeze na huku wanahedhi na mwili wake ulikuwa ukigusana na mwili wao. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Nini hukumu ya ISTIJMAAR kujifuta na vijiwe au tissue kabla ya kunawa na maji? Na je inakuwa kwa choo kidogo (mkojo) tu, au kwa choo na kikubwa ?

Jawabu: Wanavyuoni wetu wa Maghrib-Morocco wameshikilia kuwa ni wajibu kwa kuamrishwa kwake kwenye hadithi ya Mtume(SAW). Na asili ni kuwa jambo hili lime egemezwa kuwa ni wajibu, na wanavyuoni wengine wakasema kuwa jambo hili linapendezewa kulifanya. Na kauli ya mwanzo kuwa jambo hili ni wajibu, ni bora kuifuata. Na hamna tofauti baina ya choo kidogo au kikubwa. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Suala: Nini hukumu ya maji ya wadi (maji yanayomiminika kama vile mito inapokuja mvua) ambayo ni tahir yakibadilika moja katika sifa zake kama vile rangi kwa ajili ya udongo-matope yanayovutwa na maji hayo?

Jawabu: Maji hayawi najisi isipokuwa yakishindwa (yakibadilishwa) sifa yake na kitu chingine kikasababisha kubadilika kwa rangi yake, utamu wake na harufu yake, sharti kitu hicho kiwe ni najisi. Ama udongo (matope) si najisi bali umeshirikiana na maji katika sifa zake nazo ni tohara na kutahirisha basi kimojawapo hakimshindi mwingine.(Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Suala: Nini hukumu ya kutawadha kwa maji yaliyotwama yakiingiwa na najasa?

Jawabu: Maji yakiwa ni mengi kadiri ya kiwango cha Kulatayn (200kg-200lt) inajuzu kutawadhia kwa kuwafikiana wanavyuoni wote. Na maji hayo yakiwa chini ya kiwango hicho basi kuna khilafu kujuzu kwake ikiwa hayatabadilika rangi yake au utamu wake au harufu yake.(Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Nini tofauti baina ya Manii na Al-Madhiy na Al-Wadiy. Na nini hukumu ya kila kimojawapo?  

AL-MANII: Ni maji meupe mazito yanayotoka kwa nguvu na yanamalizika kwa kumalizika utamu(ladha) ikiwa yatatoka kwa Mwanamume au Mwanamke. Kwa Mwanamume inafuatilia kumalizika kutoka manii, kuanguka (kulala) kwa utupu wa Mwanamume, na kutoka kwa manii kunawajisha kukoga janaba.

 AL-MADHIY: Ni Maji yanayoteleza na hayana rangi yanatoka kwa ajili ya matamanio au kuchezeana baina ya mume na mke bila ya kufikia kilele cha kuvunjika matamanio hayo nayo ni mepesi kushinada manii.

 AL-WADIY: Ni maji meupe yanayotoka bila ya matamanio baada ya mkojo, au kwa sababu ya baridi au maradhi. Na maji haya mawili Al-MADHIY na AL-MADIY yanaharibu (yanavunja) udhu na wala hayawajibishi kukoga janaba yakitoka.(Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Suala: Je inajuzu kujisafisha choo kidogo au kikubwa kwa kutumia mawe au karatasi (ISTIJMAAR), bila ya maji kwa ajili ya kujitaarisha kusali?

Jawabu: kwetu sisi (Maibadhi) haijuzu kutumia mawe bila ya maji bali hamna budi kujumuisha baina ya maji na mawe, na haya ndiyo waliyoyafanya watu wa Qubaa ambao ALLAH amewasifu katika Qur'aan kwa kusema: (Msikiti ulio jengwa juu ya msingi wa uchamngu tangu siku ya mwanzo unastahiki zaidi wewe usimame ndani yake. Humo wamo watu wanao penda kujitakasa. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanao jitakasa)-Tawba, aya ya 108. Na Mtume (SAW) ameamrisha masahaba wafanye kama waliyo yafanya watu wa Qubaa, kwani Mtume(SAW) aliwajia watu wa Qubaa na akawauliza kitu gani kilichowafanya wasifiwe na ALLAH, wakasema kuwa wanajisafisha na vijiwe kwanza kisha ndiyo wanatawadha na maji. Kutokana na hayo atakae sahau kutumia maji basi alipe sala yake kwani sala yake haijatimia.(Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

 

Suala: Je ni inalazimika kutumia sabuni wakati wa kukoga janaba na kukosha najasa. Na je inajuzu kukoga janaba na kukosha najasa chini ya idadi ya josho tatu (kukosha janaba/najasa chini ya mara tatu)? 

Jawabu: Hailazimiki kutumia sabuni unapokoga janaba vivi hivyo katika kukosha najasa, isipokuwa najasa hiyo haita toka mpaka utumie sabuni. Na idadi inayotakikana katika kukosha najasa ni mpaka najasa hiyo isafishike (iondoke).(Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu)

 

Suala: je inamlazimika yule aliye na janaba akoshe mwili wake wote?

Jawabu: Sijui nini unakusudia kusema "aliye na janaba". Ikiwa unakusudia kuwa manii yamegusa (yameingia) sehemu katika mwili wake basi katika hali hii inamuajibikia asafishe ile sehemu iliyoguswa (iliyoingia) manii tu. Na si juu yake (lazima) kukosha mwili wake mzima.(Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu)

 

Suala: Mtu ana maradhi ya kumtoka upepo kwa muda mrefu,Wakati anatufu katika Al-Kaaba ukawa upepo huo unamtoka, na hajarejea kutawadha kwa hoja kuwa upepo huo utaendelea kumtoka kwa muda mrefu. Nini juu yake?

Jawabu: Ikiwa upepo utaendelea kumtoka mpaka akawa hapati nafasi ya kutufu (hawezi kutufu) bila ya kutoka upepo huo, basi hukumu yake ni  kama hukumu ya mwenye maradhi ya kutoka vidone vya mkojo kila wakati, nayo ni kutawadha mwanzo tu wakati anataka kuanza kutufu. Na upepo huo hautomdhuru baada ya hapo(Baada ya kutawadha udhu wa mwanzo), na vivo hivyo anafanya akitaka kusali. Na ni juu yake atawadhe upya kila anapotaka kusali na anapotaka kutufu. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu)

 

Suala: Nina matatizo ya kutokwa na gesi tumboni kama vile maji mazito na kusababisha kuwacha athari ya maji hayo katika nguo yangu inaponitoka gesi hiyo. Je inanijuzia kuwa imam wa sala (kusalisha watu)?

Jawabu: Ikiwa na yakini (uhakika) ya kutokwa na kitu hicho, basi haijuzu kuwa Imam wa kusalisha watu, lakini ikiwa hali hiyo inaendelea na haikatiki, basi juu yako utawadhe kila ukitaka kusali na usali bila ya kuwa imam wa watu, na hakita kudhuru kitakacho kutoka wakati umo ndani ya sala kwani hukumu yako ni kama ya mtu mwenye maradhi ya kutokwa na vidone vya mkojo kila wakati.(Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu)

 

Suala: Nini hukumu ya sala inayosaliwa na nguo ambayo ina harufu mbaya?

Jawabu: Ikiwa nguo hiyo haijaingia najasa basi sala inajuzu kwa kuvaa nguo hiyo, lakini ni bora nguo ya kusalia iwe ni yenye harufu nzuri. (Mwenyezi Mungu ndie mjuzi wa kila kitu).

<<<<  ENDELEA