|

FADHILA ZA FUNGA YA RAMADHANI
Fadhila za saumu
hazimo katika funga ya Ramadhani pekee; bali saumu ni ibada ya
kimwili halisi ambayo fadhila zake zinamfika mwenye kufunga ikiwa ni
saumu ya Ramadhani au nyengineyo. Ndio maana zikaja hadithi nyingi
kutoka kwa Mtume (S.A.W) juu ya fadhila za saumu. Imepokewa kwa Sahl
bin Saad kuwa amesema: Amesema Mtume (S.A.W):
(في الجنة ثمانية أبواب منها باب يسمى الريان لا يدخل منه إلا
الصائمون)
“Peponi kuna milango minane, mmoja wao ni mlango unaoitwa Al-Rayyaan,
hawaingii kwa huo isipokuwa wanaofunga”.
Kwa wingi wa
fadhila za ibada hii na nafasi yake pekee kwa Mwenyezi Mungu,
amejipa Mwenyezi Mungu mwenyewe jukumu la kuithibitisha. Amesema Abu
Hurairah R.A: amesema Mtume wa Allah (S.A.W)
katika hadithi Qudsy:
(كل عمل ابن آدم يضاعف الحسنة
بعشر أمثالها إلى سبعمائة ضعف، قال الله تعالى: إلا الصوم فإنه لي وأنا
أجزي به، يدع شهوته وطعامه من أجلي، للصائم فرحتان، فرحة عند فطره
وفرحة عند لقاء ربه، ولخلوف فم الصائم أطيب عند الله من ريح المسك)
“Kila
amali njema ya mwanadamu huzidishwa katika malipo fadhila yake moja
mara kumi mpaka mara mia saba. Amesema Mwenyezi Mungu: isipokuwa
saumu, hii ni yangu Mimi, na Mimi ndiye Mwenye malipo yake; mtu
anaacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili yangu!. Mfungaji
ana furaha mbili: furaha anapofuturu na furaha anapokutana na Mola
wake. Na harufu ya mdomo wa mwenye kufunga ni nzuri kwa Mwenyezi
Mungu kushinda harufu ya Misk”.
Na kwa
riwaya ya Imam Rabii:
(فارق عبدي شهوته وطعامه من أجلي، فالصيام لي وأنا أجزي به).
“Ameacha mja wangu matamanio yake na chakula chake kwa ajili yangu!,
basi saumu ni yangu Mimi, na Mimi ndiye Mwenye malipo yake”.
Bali
kawaida ya saumu huitengeneza nafsi ya mwanadamu na kuielekeza
mwelekeo unaoridhiwa, na hupelekea kuvunja matamanio na kuizuia
nafsi na maasi. Mtume (S.A.W) anasema:
(الصوم جنة، فإذا كان أحدكم صائما فلا يرفث ولا يجهل، وإن امرؤ قاتله
أو شاتمه فليقل إني صائم)
“Saumu
ni kinga, basi akiwa mmoja wenu amefunga asifanye machafu wala
ujahili, na mtu akigombana nae au akimshutumu aseme mimi nimefunga”.
Fadhila za saumu ni
nyingi sana hawezi mwanadamu kuzichambua zote. Hizi tulizo zitaja ni
tone katika fadhila hizo.
Mwenyezi Mungu
ameumba viumbe vyake, na akaamua kufadhilisha baadhi yao juu ya
baadhi, na kumtukuza mmoja wao juu ya mwengine. Hivyo, kama
alivyomtukuza mwanadamu juu ya viumbe vyake vyote vingine,
amewafadhilisha kati ya wanaadamu mitume na manabii. Na kama
alivyowatukuza manabii na mitume, amemfadhilisha kati yao Mtume wetu
Muhammad (S.A.W) juu ya wengine wote. Halikadhalika kuhusiana na
mwahala; Mwenyezi Mungu ameitukuza misikiti kuliko maeneo mengineyo
katika ardhi, na akaifadhilisha Msikiti wa Makka na Msikiti wa
Madina pamoja na Al-Aqsa juu ya misikiti mingine yote. Na vivo hivyo
katika nyakati; akaufadhilisha mwezi wa Ramadhani juu ya miezi
mengine, akaufanya uwe pekee kwa sifa nyingi ambazo zimeinua hadhi
na utukufu wake, ukawa ni mwezi tofauti na miezi mingine,
zikajumuika hadithi nyingi kuhusiana na fadhila zake. Imepokewa
katika hadithi sahihi ya Mtume (S.A.W):
(إذا جاء رمضان فتحت أبواب السماء وأغلقت النار وصفدت الشياطين)
“Inapokuja Ramadhani hufunguliwa milango ya mbinguni na hufungwa ya
motoni na hutiwa pingu mashetani”.
Na imekuja katika
riwaya nyingine:
(فتحت أبواب الجنة وأغلقت أبواب النار وصفدت الشياطين )
“hufunguliwa milango ya peponi na hufungwa milango ya motoni na
hutiwa pingu mashetani”.
Na amesema Mtume (S.A.W):
(من صام رمضان إيمانا واحتسابا غفر له ما تقدم من ذنبه)
“Atakae funga Ramadhani kwa imani na kutaraji malipo, atafutiwa
madhambi yake yaliyo tangulia”.
Kisha Mwenyezi
Mungu ameupwekeza mwezi huu kwa usiku mkuu wa utukufu, mwingi wa
fadhila, amejaalia thawabu za atakae amka na kufanya ibada katika
usiku huu kwa imani na kutegemea thawabu, kufutiwa maovu na
kusamehewa madhambi. Imekuja katika hadithi tukufu kutoka kwa Mtume
(S.A.W):
(من قام ليلة القدر إيمانا واحتسابا غفر له ما تقدم من ذنبه)
“Atakae inuka kuabudu katika Usiku wa Utukufu kwa imani na kutaraji
malipo atafutiwa madhabi yake yaliyotangulia”.
Kisha Mwenyezi
Mungu ameupwekeza mwezi huu kwa usiku mkuu wa utukufu, mwingi wa
fadhila, amejaalia thawabu za atakae amka na kufanya ibada katika
usiku huu kwa imani na kutegemea thawabu, kufutiwa maovu na
kusamehewa madhambi. Imekuja katika hadithi tukufu kutoka kwa Mtume
(S.A.W):
(من قام ليلة القدر إيمانا واحتسابا غفر له ما تقدم من ذنبه)
“Atakae inuka kuabudu katika Usiku wa Utukufu kwa imani na kutaraji
malipo atafutiwa madhabi yake yaliyotangulia”.
Na mwezi wa
Ramadhani ni mwezi wa kupanda daraja na wa kuzidishwa mara nyingi
malipo ya mema. Mtume (S.A.W) kamwambia Um Sinan:
(فإذا جاء رمضان فاعتمري فإن عمرة فيه تعدل حجة)
“Ukija
mwezi wa Ramadhani nenda ukafanye Umra, kwani umra katika Ramadhani
ni sawa na kuhiji”.
Yanatosha
kuelezea fadhila za Ramadhani maneno yake Mtume (S.A.W) haya:
(ولو علمتم ما في رمضان لتمنيتم أن يكون سنة)
“Mungalijuwa yaliyomo katika Ramadhani mungalitamani iwe mwaka mzima.”
|