|
|
BIBI AAMINA
MAMA YAKE
NABII MU`HAMMAD (S. A. W. ) |
Hatutatumiya sana ushahidi wa Quran katika
haya yetu mazungumzo. Si kama hakuna, bali tunaoneleya kama itatubidi kuleta
ushahidi wo wote kwa ajili ya kutiliya nguvu maneno yetu ; basi tutatumiya
Hadithi zake wetu Mtume (`Alayihi Azkaa Ttahiyya) pamoja na yale
waliyoyasema watu juu yake. Mtume (SAW) alikuwa akijisifu kwa kusema maneno
yenye maana ifuatayo :-
لم يزل الله ينقلني من الاصلاب الطيبين الى الارحام الطاهرين , مصفى مهذبا" .
لاتتشعب شعبتان الا كنت فى أخيرهما.
"Lam yazali Llaahu yungiluni mi`na
laslaabi ttayyibiina ila larhaami ttaahirati Muusaaffan muhadhdhaban. Laa
tatasha`abu shu`ubataani illa kuntu fii akhairihimaa"
{"Mola wangu hakuacha kuniyondosha kuumeni
kuzuri na kunipeleka kuukeni safi, tahir na mwenye malezi mema. Kila
kukiendeleya kutengana huku kuwili mimi huwa ule upande mzuri zayidi"}
Kwa nini asijisifu namna hiyo aw zayidi na
kujinata na hali yakuwa aliyoyasema yote ni kweli, yeye ni mtukufu kwa baba
na mama. Hana dowa katu. Mama yake Mu`hammad (Salaawatu Llaahi wa Salamuhu
Alaihi) ni Aminah bint Wahab bn Abdul Manaf bn Zuhra bn Kilab bn Murrah.
Wazee wake ni mabwana wa Kikureshi, wenye kuidhibiti Makka kwa kila njiya.
Na mama yake (wifi yake) ni Birra bint Abdul Iza bn Uthman bn Abdul Daar
bn Qusai. Mradi kila mmoja ni miongoni mwa vigogo vya Makka.
Bibi Aamina kakuliya mastakimu mazuri na
kulelewa malezi mema. Hakuwa akiyonekana na watu na kucheza ovyo ovyo.
Hapakuwa aliyeweza kuyeleza vizuri sura yake aw umbo lake aw wasfu wake
abadan. Mtu hawonekani.
Uzuri wa ubora wake ingawa hawakuwa
wakimuwona lakini uliwavutia sana vijana wa Kiqureshi kwa zile habari na
sifa zake walizokuwa wakizisikiya. Kila mmoja kati yawo alitamani nyota hiyo
iliwachunga yeye. Nyota iliwachagua bwana Abdullah bn Abdul Muttalib bn
Hashim kujuwana na mtoto wa ami yake Aamina bint Wahab, kwa vile ilivyokuwa
Banii Hashim na Bani Zuhra ni ndugu na wamoja na hawakutengana tokeya huwo
wakati wa babu yake Kilab bn Murrah, nao ni Qusai na Zuhra.
Wote wawili Abdullah na Aamina walikuwa ni
wacheza wamoja, walikuwa haweshi kukutana katika michezo yawo ya majumbani.
Ilifikiya wakati ikawa lazima Aamina ajifiche ndani na asiyonekane tena na
watu, hata na wachezaji wenziwe aw hata na nduguye Abdullah na wenginewo.
Baadhi ya wazee wake Aamina hawakupendezewa
sana na ndowa za Abdullah kwa vile wajuavyo habari ya nadhiri ya Abdul
Muttalib wakati alipokuwa yeye anachimba kisima cha Zamazam aw tuseme
alipokuwa akikifukuwa, kwani hichi kisima tulieleza nyuma juu ya habari ya
Haajir na Nabii Ismaaiil (AS), namna ilivyokuwa hata kikapatikana.
Maqureshi wote walikula njama na kumzuiya
Abdul Muttalib asikifikuwe na kumkejeli kuwa yeye ni maskini wa watoto. Hapo
aliweka nadhiri kuwa akiruzukiwa watoto kumi na wakawa wakubwa, basi yeye
atamchinja mmoja kuwa yeye ni nadhiri yake.
Mambo haya jamani ! Umati wa wake kwa waume
wamejazana mbele ya Ka`aba mikono yawo vifuani wanangojeya matokeyo ya kura
ya watoto wa Abdul Muttalib. Habari zilitapakaa kuwa kura imemuangukiya
Abdullah, na Aamina yupo mtaani. Alizidi kujipweteka kwa habari hii.
Maqureshi wote walimpinga Abdul Muttalib na
kumpa shauri ya kwenda kutazamiya huko Khaibar.
Wakatoka pamoja naye. Mji wote haukusaliya
mwanamume ila walikwenda pamoja naye. Kwa haya basi, hilaki za Bi Aamina
zilizidi kwa kuwona mpaka jiyoni hapana hata mtu mmoja wa kiyume aliyerudi
kumpa zayidi ya habari kuwa Abdulla kesha chinjwa aw vipi.
Baada ya siku ishirini msafara wa Maqureshi
ulirejeya Makka na shauri ya kupigwa kura kwa kutia mgamiya kumi upande
mmoja na wa pili Abdulla. Kama kura ni yake basi wawe wakiyongeza ngamiya
kumi kumi hadi Mungu wawo aridhike na kukubali. Haikuchukuwa muda ila Aamina
alikuwa machozi yakimtoka kwa furaha ya kuwokoka Abdulla na kutolewa muhanga
kwa ngamiya miya moja.
Birra, kwa hakika hakujiya haya, ila alikuwa
na matayarisho ya jambo muhimu zayidi. Nalo ni kwa Abdul Muttalib kaja
kutaka mkono wa Aamina.
Mashoga na viroro walijaa nyumbani kumpa
mkono wa furaha Aamina na kumtoleya kila aina ya hadithi. Hadithi zote
zilikuwa ni za wivu na za kumuoneya maya Aamina kwa mchumba wake kichinchiri.
Kila mwana kinda kindaki mwana halali wa nyuki alikuwa ananung`unika kwa
nini hakuja kuposwa yeye. Usiku ule ule aliyohamishwa biarusi kwake aliyota
ndoto ya ajabu. Asubuhi hakuweza ila yeye alimuhadithiya mumewe. Kwa ufupi
ndoto ilikuwa :- "KAWONA NURU IKITOKANA NAYE MWILINI MWAKE NA KUNG`ARISHA
KILA KITU KILIYOPO KARIBU NAYE, KAMA KWAMBA DUNIYA NZIMA IMEZAGAA NURU HIYO
NA HUKU SAUTI ITOKAYO MBALI IKIMWAMBIYA :-
"WEWE UNA MIMBA YA BWANA WA UMMA HUU."
Baada ya siku kumi hivi Abdulla ilimbidi
amuwache Biyarusi kabla ya ule utamu wa fungate hawujesha ili aunge msafara
wa biashara unaokwenda Sham - (Syria).
Upepo ulisita na palikuwa kama pana wingu
wakati ule Abdulla akimuaga mkewe Aamina. Aamina kila atazamapo kipaji cha
Abdulla hawoni ile nuru aliokuwa akiiyona na roho yake nzito kuliko jabali
kumuachiliya mumewe kuondoka. Abdulla alijichekesha na kunena : " Ewe
mpenzi, si uzuri kuwa mwingi wa huzuni. Baada ya majuma machache tu nitarudi.
Jipumbaze na kuvuli changu ambacho kila wakati kitakuwa kikikutembelea..
Bibi Aamina alisaliya kama gogo kasimama
penye kizingiti cha chumbani baada ya kuondoka Abdulla. Mpaka akaja Barke
mtumishi wake, na kumkamata mkono mpaka kitandani kwake ambapo alikaa siku
nenda siku rudi, bila ya kuondoka.
Wakati wa kurejea masafara umekuwa karibu
kama pua na mdomo na zayidi kidogo. Bi Aamina yumo kumgoja Abdulla kwa hamu
kubwa sana.
Vup ! Aamina anamuwona baba yake, bwana
Wahab na mkwewe bwana Abdul Muttalib, mumewe Abdulla hayumo.
Habari za mwisho na za huzuni ndizo
zimgojazo : Abdulla yupo Yathrib (Madina) yu mgonjwa, hakuweza kuvumiliya
shida za safari. Bora yeye akaye kumuombeya du`aa. Aamina aliendeleya na
du`aa kwa muda wa miezi miwili, na huku ndoto nzuri nzuri ya kizazi chema
haziishi kumjiya. Yakawa yaliyokuwa. Al Haarith anarudi peke yake kutoka
Yathrib na kachukuwa na kubeba mzigo mzito wa huzuni na majonzi :- Abdulla
KAFA.
Abdulla kafa ! Hatarejeya ! Aamina aliyona
kama kiwingu cha huzuni kimemshukia na duniya yote ilikuwa giza na totoro,
imechujuka na wala haina utamu tena baada ya kifo chake Abdulla. Ajabu hii
hata machozi yanafanya ubakhili na hayataki kuchiririka ? Kwa nini isiwe
hivyo na hali yakuwa maiti ni kijana mbichi wa miaka kumi na nane..?!
Majonzi na fikira za faida gani kutolewa ule
muhanga wa ngamiya miya moja, na hali ya kuwa huyo aliyetolewa muhanga huwo
ilibidi afe. Majonzi yaliondoka mara tu baada ya kujuwa muhanga ule ulikuwa
ni kwa sababu ya hicho kizazi kitukufu kiliyomo tumboni mwake Aamina. Mwezi
wa Mfungo sita aw Agosti 570 Nuru Tukufu iliyanza kuzagaa na kutanda mote
kwa miyezi michache baada ya kifo cha baba yake, Abdulla.
Ukisoma habari za maisha ya Nabii Mu`hammad
(SAW) utawona fikra zinagongana. Kuna wasemawo kuwa baba yake kafa kabla ya
kuzaliwa kwake. Wengine wanasema kafa baada ya kuzaliwa. Piya hawa
wanatofautiyana huko kufa kwake kwa muda gani, tokeya majuma mawili tangu
kuzaliwa kwa mtoto hata kwa wa miyezi kumi na moja.
Yenye nguvu zayidi ni kufa kabla ya kuzaliwa.
Ilichukuwa kiasi cha siku khamsini tokeya kushindwa Abraha kuipiga L-Ka`aba
na kuzaliwa kwa Mu`hammad (SAW). Wengine wanasema siku ile ile na wengine
wanasema mwaka ule ule.
Usiku wa manane ndoto nzuri zilimjiya
Aamina. Sauti nzuri ilimwambia :-
أعيذه بالواحده من كل حاسد , وسميه محمد.
Aidhiihi bil waahid, min kulli haasidi, wa
Sammiihi Mu`hammadi.
{"Mkinge kwa Wahedi, na shari za hasidi,
umwite Mu`hammad}
Baada ya ndoto hii aliyota nyengine kuwa
kazungukwa na wanawake wengi pande zote za kitanda. Hakuwafahamu kina nani
ila aliyona kuwa wawo ni kama Maryam bint `Amraan, na Asiya mke wa Firauni,
na Haajir mame Ismaaiili. Papo hapo akazaa NURU TUKUFU na miujiza namna kwa
namna ilitokeya.
Kwa kishindo cha kifo cha mumewe, maziwa ya
Aamina yalikawuka na asiweze kumnyonyesha mwanawe. Kwa hivyo akapewa
Thuwayiba, ambaye aliwahi kumnyonyesha ami yake Hamza bn Abdul Muttalib
mpaka waje mamama walezi aw kwa jina jengine wanyonyeshaji. Ambawo karibu
wote baada ya kufika walimkataa kwa vile yeye ni masikini na ni yatima.
Aamina yalimjaa majonzi kuyawona haya.
Huzuni hizi ziliondoka jioni baada ya
kuondoka Halima Ssa`adiya, ambaye karejea kumchukuwa kwa vile wenziwe
walirejeya na watoto ila yeye ; kwa hivyo aliona haya kurejeya mikono mitupu.
Bora kupata japo nusu ya ole kuliko kuondokeya patupu.
Halima kumchukuwa Mu`hammad (SAW) miyujiza
iliyanza. Chuchu zilijaa maziwa, na hata ngamiya wawo alijaa maziwa. Neema
ya maziwa ya wale wanyama wake iliendeleya.
Nyumba ilikuwa nzito na ilimuinamiya Aamina
kwa vile mumuwe kafa na alisaliya na maliwazo mamoja tu nayo ni kiliomo
tumboni mwake. Lewo kitu hicho kipo duniyani nacho hakipo hapo nyumbani,
bali kipo huko katika jangwa la Bani Saad. Hapana kitu cha kumpumbaza ila
majonzi na huzuni ambazo zilimuathiri sana afiya yake.
Hayikuchukuwa muda ila miyaka miwili
ilikwisha kama mchezo na Halima alirejeya na Mu`hammad (SAW) anataka
kutumbuka kwa wingi wa damu iliokuwa ikimwenda mwilini. Halima alimpembejeya
sana Aamina amuwachiliye yeye huyu mtoto amlee, kwa vile mjini jangwani kuna
hewa safi na upepo mzuri mpaka akapewa.
Halima kwa ghafla tunamuwona yu njiyani
kambeba Mu`hammad (ASS) akirudi naye kwa Aamina kwa hofu ya wale Malaika
wawili waliompasuwa tumbo na wale makohani waliyotaka kumchukuwa. Waandishi
wengine wa tarehe wanasema Mu`hammad (AS) alikaa kwa Bani Sa`ad hadi kufika
hirimu kidogo ndipo walipomrejesha.
Kutimu Mu`hammad (ATT) miyaka sita Aamina
alifunga safari yeye na mwanawe kwenda Yathrib kulizuru KABURI TUKUFU.
Nyumba yake aliitazama kwa jicho la muagano, na baada akenda Ka`aba
kuzunguka kwa kuiaga.
Aamina njiyani alimlowanisha Mu`hammad kwa
vile kumbusu na kumkumbatiya mpaka wakafika huko salama. Kiyasi cha mwezi
Aamina hakuwa na kazi ila kwenda maziyarani na kujipumbaza na kusema na
kaburi na kuliliya hadi macho yakachoka huko kuliya. Wakiwa njiyani katika
msafara wawo wa kurudi Makka ulivuma upepo mkali sana, hata ikabidi wasite
na kule kuendeleya na safari. Hapa nguvu za Aamina ziliyanza kidogo kidogo
kutoka.
Alinusurika na kumkumbatiya Mu`hammad (SAW)
huku yumo kunena maneno yake ya mwisho :-
"Kila chenya uhayi na kufa ni lazima, kipya
huchakaa. KIKUBWA CHO CHOTE HUTOWEKA. MIMI NAFA NA MAKUMBUSHO YAPO.
NIMEYACHA KHERI NA NIMEZAA KITU SAFI NA TAHIRI
".
Duniya yote imejiinamiya, kila kitu kimejaa
huzuni hapana sauti kusikilizana aw kitu cho chote kutaharuki. Mu`hammad
(SAW) kayinama juu ya kiwili wili cha maiti ya mama yake. Mu`hammad (SAW)
hujisifu na kunena :- Mimi ni mwana wa mwanamke wa Kikureshi alaye nyama ya
kukausha kama ng`onda" Na mimi ni mtoto wa kina Aatika katika Bani Saliim.
|