AINA ZA NAJASA

TAHARA

MAANA YA TAHARA

1.  Katika lugha tahara maana yake ni: kuwa msafi na uchafu wowote ambao unauhisi na kuuona kwa macho, na usafi wa moyo kutokuwa na machafu yeyote yale.

2.  Katika sheria ya kiislamu maana yake ni: Kuondosha uchafu wowote ule kwa kutumia maji.

UMUHIMU WA MTU KUWA TAHIR (MSAFI):-

Tahara katika uislamu ni kitu dharuri katika kutekeleza ibada ambayo ndio sababu ya sisi kuumbwa. Na kama tunavyojua kuwa sala ni nguzo muhimu katika uislamu haiwezekani kusimamishwa isipokuwa mtu awe msafi wa mwili na wa moyo, basi hivyo hivyo ibada zoote kama vile Saumu, Hajj, kusoma Quraan n.k. ni lazima mtu awe msafi wa kiwiliwili na msafi wa moyo kutokuwa na machafu ambayo yanamghadhibisha Mola.

“HAKIKA M. MUNGU ANAWAPENDA WENYE KUTUBIA NA ANAWAPENDA WENYE KUJITAHIRISHA(KUJIWEKA WASAFI) albaqra#222.

ADABU ZA KUFANYA HAJA NDOGO AU KUBWA:-

Yeyote yule mwenye kutaka kusali basi ni lazima ajizoweshe kwenda chooni ili atoe choo kidogo au kikubwa kabla ya kusali. Ili asije mtu akajishughulisha wakati ameshaanza kusali na ‘khushuu’ isije ikatoweka wakati wa kusali.

Kasema Mtume Moh’d(SAW): “Asisali mmoja wenu na huku anazuwia choo kidogo ndani ya kibofu cha mkojo”.

Na Bwana Mtume(SAW): amekataza mtu asisali ikiwa anajaribu kuzuwia haja ndogo au kubwa kutoka katika njia zake.

Basi anaetaka kwenda chooni basi afuate adabu zifuatazo:-

1.     Atayarishe kitu kinachoweza kusafisha choo kidogo/kikubwa. Mfano maji n.k.

2.     Asichukuwe chooni kitu chochote chenye aya za Quraan au jina la M.Mungu.

3.     Asifanye mtu haja yake mbele ya watu, na kama atafanya haja yake mahali palipo wazi (porini, jangwani) basi ni lazima ajitahidi kwendambali ili watu wasimuone anapofanya haja yake. Pia inapendezewa kuwa mtu asiinue nguo yake mpaka awe ameshachuchumaa.

4.     Ikiwa mtu atafanya haja yake chooni basi ni lazima atangulize mguu wa kushoto, na akiaanza kuingia aseme “ BISMILLAH, ALLAHUMA INNI AUDHU BIKA MINA ALKHUBTH WALKHABAAITH”.

5.     Asifanye mtu haja yake huku amesimama.

6.     Akitaka mtu kufanya haja yake mahali palipo wazi (porini, jangwani)  basi azingatie yafuatayo:-

I)                  Asifanye mtu haja yake chini ya mti ambao unatoa matunda au watu wanakaa chini yake kwa ajili ya kivuli. Pia katika njia watu wanazopita.

II)     Asifanye mtu haja yake katika ardhi ngumu ili mkojo usije ukamrukia.

III)   Asielekee upepo ili mkojo usije kuruka katika mwili au kivazi.

IV)   Asielekeze utupu wake wa mbele au wa nyuma QIBLA wakati akifanya haja yake. Lakini baadhi ya wanavyuoni wamesema mtu anaweza kufanya haja yake na huku ameelekea Qibla ikiwa mbele yake kuna ukuta, mfano Choo. Lakini ni ubora kujitahidi kutokuelekea Qibla hata kama umo ndani ya choo.

7.     Asifanye mtu haja yake katika maji yaliyotwama, mfano vidimbwi au katika maji yanayotembea ambayo watu wanayatumia kunawia au kunywa n.k. mfano falaj.

8.     Mtu anapofanya haja asizungumze wala asiitikie salamu.

9. Akimaliza kukojoa ni lazima ajikamue utupu wake kwa kutumia  mkono wa kushoto mpaka kitone cha mwisho cha mkojo kiondoke.

10. Kabla ya kujikosha na maji ni muhimu kutumia vijiwe au tissue ili    kukausha mkojo, haja kubwa au Alwadi (maji meupe yanayoteleza ambayo yanayotoka baada ya kukojoa au wakati wa baridi na hayasafikishi kwa kutumia maji peke yake).

11. Hairuhusiwi kutumia mifupa , ngozi au choo cha mnyama kilichokauka kwa kujifutia haja ndogo/kubwa.

12. Ni muhimu kuanza kuosha utupu wa mbele kisha wa nyuma ikiwa mtu amepata choo kidogo na kikubwa. Na ni lazima mtu ahakikishe kuwa amejisafisha vizuri tupu zake kabla ya kutoka chooni.

13. Mtu akitoka chooni ni lazima atangulize mguu wa kulia na aseme ‘GHUFRAANAK’

Kuna aina kumi za NAJASAT (uchafu) ambao ulamaa wote wamekubaliana kuhusu hivyo vitu.

 Navyo ni:-

1)       Kitu chochote chenye roho ambacho kimekufa bila ya kuchinjwa(MAITI/MZOGA).

2)       Damu

3)       Nyama ya Nguruwe

4)       Choo kikubwa

5)       Choo kidogo

6)       Mannii

7)       Al-Wadii

8)       AL-madhii

9)       Tahara za wanawake (Hedhi,Nifas, n.k.)

10)    Ulevi (Ulamaa wengi sana wanasema si najis, kwa sababu asili yake ni chakula).

1)       Kitu chochote chenye roho ambacho kimetoka roho bila ya kuchinjwa(MAITI/MZOGA):

        Na aina hii ya wanyama ni mbili:

a)       Wanyama wa nchi kavu.

b)       Wanyama wa baharini.

a) Wanyama wa nchi kavu wako aina mbili:

 I)Wanyama wenye damu inayochuruzika wanapojikata au kuchinjwa.

II)Wanyama ambao hawana damu inayochuruzika.

I)Wanyama wenye damu inayochuruzika wanapojikata au kuchinjwa.

Aina hii ya wanyama wakifa ni najis (mfano, Panya, ndege, nyoka, N’gombe n.k). Ama binadamu Muislamu si najis.

Amesema Mtume (SAW): Akifa Panya katika samli iliyoganda basi mtoeni Panya na ile samli iliyokaribu nae kisha itumieni, na akifa katika samli iliyoyayuka basi imwageni na msiitumie.

Baadhi ya ulamaa hawajakubaliana kuwa je maiti ya (Chawa(Ni NAJIS), Mbu, Kunguni,Viroboto n.k) ni NAJIS au SI NAJIS. Baadhi ya wanavyuoni wanasema ikiwa (Chawa, Mbu, Kunguni,Viroboto n.k) amekufa mwenyewe bila ya sababu juu ya mwili wa mtu na huku mtu huyo ameshatia udhu/ameshasali basi udhu ule haujatenguka wala sala haijaharibika, ama ikiwa mtu atamuua kwa mkono wake mwenyewe basi udhu/salaa itakuwa imeharibika.  

Lakini ni bora kuchukulia kuwa hawa wadudu ni najis kwa ajili tusije tukaingia kwenye shaka wakati tunafanya IBADA.

NOTE: Sehemu yeyote ya mnyama (mfano, Mguu, Paja n.k) ikiwa imekatwa kwa sababu yeyote ile na hali ya kuwa mnyama bado yuhai. Basi hiyo sehemu huwa ni NAJIS (MAYYITA) haifai kuliwa.

II)Wanyama ambao hawana damu inayochuruzika.

Aina hii ya wanyama wakifa au wakiingia ndani ya chakula na wakafa ndani yake si najis wala hicho chakula hakiwi najis.( mfano, N’zi, Sisiminzi, Sqaat, N’ge n.k)

Amesema Mtume (SAW): Akidumbukia N’zi kwenye chombo ambacho kina (maji,maziwa) basi mzamisheni ndani kisha mumtoe nje na munywe(maji,maziwa) hayo. Hakika bawa moja linamaradhi na jengine linadawa(shifaa), basi N’zi anatanguliza bawa lenye maradhi kabla ya bawa lenye dawa(shifaa).

b)     Wanyama wa baharini.

Aina hii ya wanyama(Samaki) wamekubaliana Ulamaa kuwa si najis na ni tahir kuwala bila ya kuchinjwa na pia damu yao SI NAJIS.

Amesema Mtume (SAW): Mmehalalishiwa vitu viwili vilivyokufa na damu aina mbili. Ama viwili vilivyokufa ni: (Samaki na N’zige). Na ama damu aina mbili ni: (Maini na Wengu la Mnyama anaeliwa).

Ama Samaki wanaokufa wenyewe bila ya kuvuliwa, baadhi ya Ulamaa wanasema ni HALALI kuwala. Na ikiwa wameanza kuharibika basi ni MAKRUH(haipendezewi) kuwala.

Wanasema Ulamaa kuwa wanyama halali wa baharini ambao wanaweza kuliwa bila kupigiwa “BISMILLAHI” ni Samaki tu, ama Nyangumi ni lazima apigiwe “BISMILLAHI” wakati anapovuliwa ndio huwa halali.(ALLAHU A’ALAM).

2)     Damu Masfuh:

Ni damu inayotoka kwa wingi kwenye wanyama(mfano, N’gombe, Mbuzi, Bin Aadam n.k), kwa kuchijwa au kuumia. Basi damu hii huwa ni NAJIS na haifai(haijuzu) kunywa na hutengua udhu.

 

 Baadhi Ulamaa wamekhitalifiana katika damu chache ambayo ikikusanywa kwenye (ngozi ya mtu au nguo) haiwezi kuchuruzika kuwa SI NAJIS wala HAITENGUI UDHU. Damu hiyo ni ile inayotoka kwenye mnyama ambae hajachinjwa (mfano, damu chache inayotoka kwenye mabawa ya kuku yakivutwa au damu chache inayotoka kwenye ngozi ya mnyama akiumia au binadamu akijitumbua jipu dogo).

Ama tone dogo la damu ya Mwanadamu au damu ya N’zi, Chawa(NAJIS) , kunguni, kiroboto n.k.  akiuliwa juu ya mwili wa mtu likaganda kwenye nguo imeruhusiwa kuwa  SI NAJIS na damu hiyo haitengui udhu.

Lakini ni bora kuchukulia kuwa hawa wadudu ni NAJIS na damu yao pia ni NAJIS. Kwa ajili tusije tukaingia kwenye shaka wakati tunafanya IBADA.(ALLAHU A’ALAM).

3)     Nyama ya Nguruwe:

Bila ya shaka chochote kinachotoka kwenye Nguruwe (ngozi,maziwa,mifupa,nyama n.k) ni haramu kukitumia na kukila. Kwa dalili ya Quraan na Sunna.

Amesema Mtume (SAW) : Nimetumwa kuvunja misalaba na kuuwa nguruwe.

Ama Nyani na Tembo wamewekwa katika kundi la Nguruwe kuwa ni NAJIS. Kwa hiyo haifai kutumia chochote kinachotokana na wanyama hawa. (ALLAHU A’ALAM).

NOTE: Kuhusu ndovu ya Tembo Ulamaa wamekhitalifiana kuwa je ni najis au si najis.

4)     Choo Kikubwa(Mavi) & ( 5) Choo Kidogo(Mkojo):

Bila Shaka wamekubaliana Ulamaa wote kwa dalili ya Quraan na Sunna kuwa choo Kikubwa na kidogo cha Mwanadamu ni NAJIS. Na wanasema Ulamaa kuwa chochote kinachotoka kwenye njia ya choo kikubwa au kidogo ni NAJIS ( mfano, Kijiwe au Mdudu)

Anasema M. Mungu : (AU AKIJIWA MMOJA WENU NA CHOO KIKUBWA) Al-nisaa43.

Amesema Mtume (SAW) : (Asisali mmoja wenu na huku anazuwia choo kikubwa na kidogo).

Ama kuhusu Choo Kikubwa cha wanyama walioruhusiwa kuliwa SI NAJIS.

Dalili ni kwamba Mtume (SAW) aliwaamrisha watu wa AL-JANIIN kutumia choo kikubwa cha wanyama kuwa ni chakula cha wanyama. Watu wa AL-JANIIN wakamwambia Mtume(SAW) : Ewe mtume lakini Wanadamu wanatia NAJIS choo hicho kwa kujisafishia uchafu wao(Mavi, Mkojo), ndio Mtume akakataza watu wasijisafishie uchafu wao kutumia mifupa pamoja na choo kikavu cha wanyama.  Lakini kuhusu MKOJO wa Wanyama walioruhusiwa na wasioruhusiwa kuliwa ni NAJIS.

Kwa dalili kuwa Mtume (SAW): Ameuita mkojo kuwa ni kitu Khabith.

NOTE:

1)    Kuna hadithi kuwa Mtume (SAW): Aliwaambia watu wa ARNAIN wanywe Mkojo wa Ngamia pamoja na maziwa yake walipomshitakia kuwa wamepata maradhi.

       Lakini Ulamaa wanasema kuwa hii ruhusa ni khasa kwa hao watu peke yao.

2)     Kuna hadithi kuwa Mtume (SAW) ananasema: ( Ikikukuta Salaa na uko ndani ya zizi la mbuzi sali, na ukiwa ndani ya zizi la Ngamia usisali) (ALLAHU A’ALAM).

Kuna vitu Vinatoka puani au tumboni kwa njia ya koo ambavyo ni NAJIS na vinatengua udhu:-

1)       AL-QAY(kucheuwa) kitu mpaka kikafika mdomoni.

2)       AL-QALAS(kucheuwa) kitu na kikafika kwenye koho peke yake.

3)       AL-RUAAF(damu inayotoka puani).

Amesema Mtume (SAW): ( Atakae cheuwa kitu mpaka kikafika mdomoni,au kwenye koho au akatoka damu puani, au akatoka Al-MADHII. Na aende akatawadhe. Ama kuhusu vitu vinavyotoka kwenye mwili wa mtu ,mfano: uchafu unaotoka kwenye vidonda au Hab shabaab (Weupe), usaha unaotoka kwenye jipu ambao ni mwingi kushinda damu, mafua, kamasi na makohozi wanasema Ulamaa kuwa si najis na havitengui udhu. (ALLAHU A’ALA)

6)    AL-MANII:

Ni maji meupe mazito yanatoka kwenye Dhakar ya Mwanamume kwa kutamani na kumwaga. Manii yanaharufu mbaya. Ama kwa mwanamke Manii ni maji mepesi.

7)    AL-MADHII:

Ni Maji yanayoteleza na hayana rangi yanatoka kwenye Dhakar ya Mwanamume kwa ajili ya matamanio.

8)    AL-WADII:

Ni maji meupe yanatoka kwenye Dhakar ya Mwanamume bila ya matamanio baada ya mkojo, au kwa sababu ya baridi au maradhi.

9)    Tahara za Wanawake:

a)     Damu ya Hedhi: Ni damu inayotoka kwenye faraj(Uchi) wa mwanamke, nzito, nyeusi, na inaharufu mbaya. Na damu hii ni kawaida kwa wanawake wote kuwatoka katika kila mwezi kwa wakati maalumu.

b)     Damu ya Nifas: Ni sawasawa na damu ya Hedhi, lakini inatoka baada ya Mwanamke kuzaa mtoto.

Amesema Mtume (SAW) : ( Al-manii, na Al-madhii, na Al_wadii, na damu ya hedhi, na damu ya nifas ni NAJIS. Asisalie mtu nguo iliyoingia kitu chochote katika hivi mpaka akoshe nguo hiyo na ipotee athari yake).

c)       Damu ya Istihadha: Ni damu nyekundu nyepesi inamtoka mwanamke akiwa na maradhi.

Amesema Mtume (SAW) : ( Damu ya Istihadha ni najis, na inatengua udhu, kwasababu ni damu inayotoka kwenye mifupa ya damu,)

d)      Uchafu unaofuatilia Hedhi au Nifas, mfano: (Umanjamanjano)

e)      AL-QASSAT AL-BAIDHAA:  Ni maji meupe sana yanatoka baada ya hedhi au nifas. Haya maji ni dalili ya kuwa mwanamke ameshasafishika na hedhi au nifas. Haya maji ni najis kwa ajili yanatoka kwenye njia inayotoka najasa(Uchafu).

10)   Ulevi: (Ulamaa wengi sana wanasema si najis, kwa sababu asili yake ni chakula).

        Ulamaa wote wamekubaliana kwa dalili ya Quraan na Sunna kuwa ulevi ni najis. Na haifai   kutumia ulevi au siki yake au uchafu uliotengenezewa ulevi kuwa ni dawa ya kuponesha maradhi yeyote yale.

Amesema Mtume (SAW): ( Nimetumwa kumwaga “kuondosha” ulevi).

Lakini kuna baadhi ya ulamaa, wanasema kuwa ulevi ni TAHIR si NAJIS. Sababu ni kuwa ulevi ni najasa MAANAWIYA(najasa ambayo haionekani na haiondoki mpaka kwa nia, na kwa kukoga janaba,na kwa kuondoka athari ya hicho kitu) na si najasa HISIYA( najasa ambayo inaonekana mfano: Choo kikubwa/kidogo). Kwa ajili asili ya kitu ni tahir isipokuwa kile kilichosimama dalili juu yake kuwa ni najis. Na pia kitu kilichoharamishwa si lazima kitu hicho kiwe najis, kwani bangi ni haramu lakini si najis. (ALLAHU A’ALAM)

KUNA BAADHI YA VITU ULAMAA WAMEKHITALIFIANA KUWA JE NI NAJIS AU SI NAJIS.

VITU HIVYO NI KAMA IFUATAVYO:

1)       Wanyama waliokuwa na meno marefu (Simba, Chui n.k)

2)       Ndege wenye makucha marefu (Eagle, kunguru n.k)

3)       Paka.

4)       Mbwa anelelewa na kufundishwa vitu.

5)       Mtu Mushrik (Kafiri)

6)       Jasho la Mlevi.

1)       Wanyama waliokuwa na meno marefu (Simba, Chui n.k) :

Wamesema baadhi ya ulamaa kuwa nyama zao na vyote vinavyotoka mwilini mwa mnyama huyo (maziwa, jasho,choo chake) ni haramu.

Amesema mtume (SAW): ( Kula mnyama yeyote mwenye meno marefu na makucha marefu ni haramu). Na pia Mtume(SAW): Amekataza watu kunwya maji yaliyobakishwa na wanyama hao ikiwa kiwango cha maji ni chini ya 200Litre.

Amesema Mtume (SAW): Yakiwa maji ni QILATAIN(200Litre), basi hayanajisiki.

Pia kuna Ulamaa waliokhitalifiana kuhusu kula nyama ya Farasi, Punda na Bighaal. Je inajuzu au haijuzu? Na watu wamechukia kula nyama zao baada ya Mtume (SAW): Kukataza kula nyama ya Punda anaetumiwa katika mambo ya kimaisha(Kubeba mizigo n.k). Na wengine wanasema kuwa haifai kula nyama za wanyama hawa kwa ajili ndio wanaotumiwa wakati wa vita.

       Anasema Jabir(R.A): (Amekataza Mtume (SAW) wakati wa vita vya Khaibar kula nyama ya                  Punda wanaotumiwa na akaruhusu watu wale nyama ya Farasi). (ALLAHU A’ALAM)

2)      Ndege wenye makucha marefu (Eagle, kunguru n.k):

Wamesema baadhi ya ulamaa kuwa nyama zao na vyote vinavyotoka mwilini mwa Ndege hawa      (majimaji yanayotoka  mwilini mwake,choo chake) ni haramu.

Amesema mtume (SAW): ( Kula mnyama yeyote mwenye meno marefu na makucha marefu ni haramu).

Kuna Ulamaa wanasema kuwa inachukiza kuuwa aina sita ya ndege na wanyama. Kutokana na Hadithi iliyopokew kutoka kwa Mtume (SAW) kuwa Amesema: Musiuwe vitu sita: 1. CHURA hakika sauti mnayoisikia ya chura ni TASBIH NA KUMTUKUZA M.MUNGU, na aliporushwa Nabii Ibrahim kwenye moto, waliomba wanyama wa nchi kavu na ndege wauzime moto usimuunguze Nabii Ibrahim. M.Mngu akawapa ruhusa Vyura na wakajirusha kwenye moto, na thuluth(1/3) ya moto ikazimika, na thuluth(1/3) iliyobakia M.Mungu akabadisha joto la moto kuwa baridi ya maji. Na wala musiuwe mdudu Maji Moto(AL-NAMLA), hakika Nabii Suleman amekwenda pahali ili akanywe maji, akamuona mdudu Maji Moto(AL-NAMLA) ameinua mikono anasema: “EWE MOLA SISI NI VIUMBE KATIKA VIUMBE VYAKO WALA HATUWEZI KUKOSA FADHILA ZAKO, TUNAKUOMBA UTULETEE MVUA ILI MIMEA  IOTE”. Akasema Nabii Suleman: Rudini mumekwisha nyweshwa maji. Na wala musiuwe Nyuki, hakika wanawahifadhia vizuri na wanawalisha vizuri. Na wala musiuwe HUDHUD , kwani wao walikuwa wakipenda sana kumuabudu MOLA wakati palipokuwa  hakuna ABDU wa kuabudu. Na wala musiuwe AL-SARD ndie aliekuwa akimuonyesha njia Nabii Adam kutoka peponi mpaka ardhini kwa muda wa miaka arubaini. Na walamusiuwe        AL-KHATTAF, hakika huko kuzunguka kwake mnavyokuona ni sehemu ya Masjid AL-AQSA ulipounguzwa moto.

 (ALLAHU A’ALAM)

Wametilia mkazo AS’ HAAB( Ulamaa wa Kiibadhi). Kuhusu kuuwa wanyama hawa mpaka wakaweka kuwa, atakae wauwa wanyama hao ni lazima alipe fidia ya DIRHAM MBILI kwa kila mnyama. Ama fidia ya Chura ni MBUZI.

(ALLAHU A’ALAM)

3)     Paka:

Ipo khilaf  kuhusu Paka, Lakini lililo sahihi ni kuwa Paka ni Tahir si najis. Kwa sababu Paka ni mnyama ambae daima anaishi katika nyumba za wanadamu.

Anasema  Abi Qatada. Amesema Mtume (SAW), kuhusu Paka : (Paka si najis, hakika Paka ni mwenye kuzunguka baina yenu.)

Na wako waliosema kuwa Paka ni najis.  Kwa sababu Paka ni katika wanyama wenye meno marefu na wao ni najis. (ALLAHU A’ALAM)

4)     Mbwa anaelelewa na kufundishwa vitu:

Wamekhitalifiana Ulamaa, na wakasema baadhi yao si najis. Kwa sababu Mbwa huyo amezuiliwa kula vitu vichafu(KHABAITH). Lakini lenye nguvu ni kuwa Mbwa ni najis, kwa dalili ya hadithi ya Mtume(SAW).

Amesema Abi Huraira (R.A), Amesema Mtume (SAW) : Ikiwa Mbwa atakunywa/atakula katika chombo cha mmoja wenu, basi akoshe chombo hicho mara saba mwanzo wake kwa kutumia mchanga na mwisho wake pia kwa kutumia mchanga.

5)       Mtu Mushrik (Kafiri):

Wamekubaliana Ulamaa kuwa Mtu Mushrik ni najis.

Amesema M.Mungu :  (HAKIKA WASHIRIKINA NI NAJIS) al-tauba27.

Na Mtume (SAW): Ameamrisha ikiwa Muislamu atahitajia chombo alichotumia AHLU AL-KITAAB, basi ni lazima akioshe. Hii ndio ikawa ni dalili ya wao kuwa ni najis.

Ama baadhi ya Ulamaa wanasema ikiwa Mushrik ni katika Ahlu Al-Kitaab, basi majimaji yanayotoka katika mwili wake ni tahir.

NOTE:

Baadhi ya Ulamaa wanasema ukiwa umetawadha, na ukaamkiana na Mtu Mushrik na huku wewe au yeye ana majimaji katika mkono wake. Basi ni lazima utawadhe tena.

(ALLAHU A’ALAM).

Ama chakula cha AHLU AL-KITAAB ni halali juu yetu.

 Amesema M.Mungu : ( NA CHAKULA CHA WALIOPEWA KITABU NI HALALI JUU YENU)al-maaida5. (ALLAHU A’ALAM)

6)       Jasho la Mlevi:

Ama kuhusu jasho la mlevi, na maziwa ya mwanamke anaekunywa ulevi, wanasema Ulamaa kuwa ni bora na kujiepusha na jasho lao lisikuguse kwa muda wa siku nzima na usiku wake. Na hii ni makadirio kuwa chakula kinabaki ndani ya mwili wa mtu siku nzima na usiku wake.

(ALLAHU A’ALAM).

NOTE:

Wanasema Ulamaa ikiwa wanyama walioruhusiwa kuliwa, wakila kitu najis(Mzoga,Damu n.k),

basi li lazima wakae siku maalum ndio wachinjwe: Mfano,

a)    Ngamia ni lazima apewe chakula kisafi kwa muda wa siku kumi mpaka arubaini ndio achijwe.

b)       Ama N’gombe ni lazima apewe chakula kisafi kwa muda wa siku saba mpaka thalathini ndio achijwe.

c)       Ama kuku ni lazima apewe chakula kisafi kwa muda wa siku mmoja mpaka siku tatu ndio achijwe.

NOTE:

“NI LAZIMA TUFAHAMU KUWA MAMBO HAYA YA FIQH NI MAMBO MUHIMU KATIKA MAISHA YA MUISLAMU. NA PIA MAMBO HAYA YANAKHITILAFU NYINGI SANA KWA HIYO BORA MTU KUCHUKUWA LILE AMBALO HALINA SHAKA NA LILE AMBALO ULAMAA WAMELIKUBALIANA,  NA HALIWEZI KUHARIBU IBADA YA MTU.

 AINA ZA MAJI

Baada ya kuzungumzia aina tafauti za vitu ambavyo ni Najis katika durus zilizopita. Hivi sasa ni lazima tuzungumzie vitu ambavyo vinaweza kuondosha hiyo Najasa ikimpata Mwanadamu.

 Kama inavyojulikana kuwa MAJI ndio kitu ambacho Mwenyezi mungu amekijaalia kuwa ndio kinachoweza kuondosha najasa kwenye mwili/nguo ya Mwanadamu.

Anasema Mola katika Surat Al-Anfaal#11 : “ Na anawashushieni kutoka mbinguni maji ili yakutahirisheni(yakusafisheni).

 Lakini maji huwenda yakabadilika tabia yake(yakanajisika), kwasababu ya kuchanganyikana na vitu vingine.

Kwasababu hiyo, maji yanagawanyika katika makundi matatu katika kuwa tahir au sio tahir:-

1)      MAJI MUTLAQ (TAHUR) :- Nayo ni maji yaliyobakia katika asili yake, na hayajapoteza rangi yake wala utamu wake wala rangi yake. Na hukumu ya maji haya ni tahir yanaondosha najasa na yanafaa kutawadhia( yanafaa kuogea janaba nk na pia yanafaa kutawadhia udhu wa salaa nk). Mfano wa maji haya ni:- maji ya mvua, maji ya barafu, maji ya bahari, maji ya mito , na maji ya falaj.

2)      MAJI TAHIR:- Nayo ni maji yaliyopoteza usafi wake kwa kuchanganyikana na kitu tahir. Hukumu ya maji haya ni kuwa yanaweza kutumiwa kuondosha uchafu kwenye mwili, lakini hayawezi kutumiwa kwa kuogea Hedhi, Nifas wala Janaba, na pia kutawadhia udhu wowote ule. Mfano wa maji haya ni :- maji yaliyotiwa kitu ndani yake mfano sabuni au zaafarani au maji yanayotolewa kwenye miti.

3)      MAJI NAJIS:- Nayo ni maji yaliyoingia najasa. Na hukumu ya maji haya ni najis yakibadilika rangi,utamu, na harufu. Basi maji haya hayafai kutumiwa na muislamu kufanyia chochote kile (kuogea, kusafishia vitu na kutawadhia).

UDHUU:-

FADHILA ZA KUTAWADHA NA UMUHIMU WAKE:

Udhu ni alama(sifa) katika alama za waislamu hapa duniani na kesho akhera. Ameulizwa Bwana Mtume(SAW): “Vipi utawajuwa watakao kuja baada yako. Akasema Mtume(SAW): Mnaonaje akiwa mtu ana farasi mwenye alama nyeupe kwenye kipaji cha uso na miguu yake, akiwa amechanganyika na farasi wengine wengi. Je ? mtu huyo hatamtambua farasi wake? Wakajibu Masahaba; ndio Bwana Mtume atamjua. Akasema Mtume(SAW): Basi watu hao watakuja siku ya kiyama wana alama nyeupe kwenye vipaji vyao vya uso na kwenye miguu yao, kwa ajili ya athari ya udhuu”.

Udhu huwa ni usafi wa kusafisha vitu vya mwilini kwa nje. Lakini udhu pia huwa ni usafi wa kusafisha vitu vya mwili kwa undani. Kwani udhu husafisha na kuondosha uchafu na vumbi kwenye:- mdomo, pua, uso, mikono , masikio, miguu na kichwa. Pia udhu husafisha viungo hivi na madhambi ambayo viungo hivyo vimefanya, mfano: mdomo kusema mambo mabaya, pua kunusa harufu ya manukato ya mwanamke ajnabii, macho kutizama mambo yaliyokatazwa, mikono kugusa vitu ambavyo imekatazwa kugusa, kama vile kumgusa mwanamke ajnabii mwili wake, masikio kusikiliza machafu kama vile nyimbo, na miguu kwenda kwenye haramu. Basi udhu ni tahara ya vyote hivyo. Ama madhambi ambayo yanafutika kwa ajili ya kutawadha ni madhambi madogo ama madhambi makubwa hayafutiki mpaka kwa tauba ya kweli.

Amesema Mtume (SAW):- “ Je niwaambieni yale ambayo MOLA humfutia mja madhambi yake na humuinulia daraja yake? Kutia udhu kwa ukamilifu katika viungo, kuzidisha kwenda msikitini na kungoja salaa baada ya sala. Basi huu ndio mshikamano, kasema hivyo Mtume mara tatu.”

Na kutawadha kabla ya sala ni wajib, kwa dalili ya Quraan.

Anasema Mola:- “ ENYI AMBAO MMEAMINI, MKIINUKA KWENDA KUSALI, OSHENI NYUSO ZENU NA MIKONO YENU MPAKA KWENYE VIGANJA, NA PANGUSENI VICHWA VYENU NA MIGUU YENU MPAKA KWENYE VIFUNDO” Al-maaida#6.

Kasema Mtume(SAW):- “ hana imani ambae hasali, na wala hana sala ambae hana udhu, na hana mtu saumu isipokuwa kwa kuacha mambo haramu aliyoyakataza M.Mungu.”

NAMNA YA KUTAWADHA:-

Inatakiwa mtu kabla ya kutawadha, ajisafishe na uchafu wowote ule kwenye mwili/nguo. Na atawadhe kwa kutumia maji masafi.

Basi Mtu akianza kutawadha ni lazima afuatilie mambo yafuatayo:-

a)      Atie NIA kwenye moyo wake kuwa anatawadha kwa ajili ya ibada.

b)      Aanze kutawadha kwa kusema “BISMILAHI RAHMANI RAHIM”

c)      Akoshe mikono yake mpaka kwenye kifundo mara 3.

d)      Atie maji mdomoni mara 3.

e)      Atie maji puani  mara 3.

f)        Akoshe uso wake mara 3.

g)      Akoshe mkono wa kulia kuanzia vidoleni mpaka juu ya kifundo mara 3.

h)      Akoshe mkono wa kushoto kuanzia vidoleni mpaka juu ya kifundo  mara 3.

i)        Apanguse kichwa chake kwa maji  mara 3.

j)        Akoshe masikio n’nje na ndani  mara 3.

k)      Akoshe mguu wa kulia pamoja na vidole na chini ya nyayo mpaka juu ya

      kifundo  mara 3.

l)        Akoshe mguu wa kushoto pamoja na vidole na chini ya nyayo mpaka juu ya kifundo mara 3.

NOTE:- Inatakiwa mtu akimaliza kutawadha asome duaa ifuatayo :-

“ASH’ HADU AN LAA ILAHA ILA ALLAH, WA ASH’ HADU ANNA MUHAMMADAN ABDUHU WA RASULUH. ALLAHUMA IJ’ ALANI MINA AL-TAWABINA WAJ’ ALANI MINA AL-MUTA’ TTAHIRIN”

FARIDHA ZA UDHUU:-

1)       NIA:- Nayo ni lazima kabla ya kufanya ibada yeyote ile. Nia hutiwa ndani ya moyo kuwa hivi sasa mimi nina anza kutawadha kwa ajili ya salaa.

     Amesema Mtume (SAW):- “ Hakika kila AMAL ni NIA”

2)       Kuosha Uso.

3)       Kuosha mikono miwili pamoja na vifundo vya mikono.

4)       Kupangusa kichwa.

5)       Kuosha miguu miwili pamoja na vifundo vya miguu. Na ni lazima mtu ahakikishe kuwa atasafisha baina ya vidole vyake vya miguu kwa kutumie vidole vya mikono, sio mtu aweke mguu wake kwenye bomba huku maji yanamwagikia bila ya kutumia mkono kwa kusafisha miguu.

Amesema Mtume(SAW):- “Safisheni baina ya vidole nyenu vya miguu, kabla hamjasafishwa na misumari ya moto”

SUNNA ZA UDHU:-

1)     Kusema “BISMI LAHI RAHMANI RAHIM” unapoanza kutawadha.

Amesema Mtume(SAW):- “ hana udhu ambae haja taja jina la M.Mungu”

2)       Kukosha Mdomo

3)       Kukosha pua.

4)       Kukosha masikio n’nje na ndani.

5)       Kutawadha kila kiungo  mara 3.

6)       Kufuatilia mpangilio uliokuja kwenye sunna ( usitangulize kutawadha kiungo kabla ya kinachofuatilia, mfano: kuosha uso kabla ya pua)

7)       Kutawadha viuongo vyote wakati mmoja ( sio utawadhe baadhi ya viungo kisha baada ya muda ukamilishe vingine)

8)       Kusafisha ndevu kwa kupitisha vidole wakati wa kuosha uso.

 MANDUBAAT AL-UDHUU:- Ni mambo yanayopendezewa kufanywa wakati wa kutawadha na yakiwanchwa hayatengui udhu:-

1)       Kupiga mswaki kabla ya kutawadha. Amesema Mtume (SAW):- “Ningalikuwa si waogopei umma wangu, lingaliwaamrisha kupiga mswaki katika kila salaa na kila udhuu.

2)       Kutumia maji kiasi si kwa israfu.

3)       Kuomba duaa baada ya kutawadha.

MAMBO YANAYOCHUKIZA KUFANYA WAKATI WA KUTAWADHA:-

1)       Kumwaga maji kwa wingi.

2)       Kuzidisha kutawadha viungo zaidi ya mara tatu.

3)       Kuzungumza wakati wa kutawadha, isipokuwa kuomba dua au kumdhukuru M.Mungu.

4)       Kutawadha chooni.

5)       Kutawadhia chombo cha dhahabu au fedha.

6)       Kutawadha na hali uko uchi hata kama uko chooni peke yako au kutawadha na huku nguo yako iko juu ya magoti, na ikiwa mtu kakuona uchi wako, basi udhu utakuwa umetenguka.

MAMBO YANAYOTENGUA UDHU:-

1)       Chochote kitakachotoka kwenye tupu mbili ( utupu wa mbele au wa nyuma)

2)       Kutoka damu, ikiwa kutoka mdoni, au puani, au mwilini.

3)       Kuingia najasa mwilini au nguoni.

4)       Kutizama mambo yaliyoharamishwa, kama vile nywele au mwili wa mwanamke ambae unaweza kumuowa.

5)       Kugusa mwili wa mwanamke ambae unaweza kumuowa, ikiwa kwa kumuamkia nk, au kugusa utupu wako au wa mkeo.

6)       Kusikiliza nyimbo, na maneno machafu.

7)       Kusema maneno baatil(mabaya):- kusengenya mtu, kufitinisha watu, kudanganya, kulaani mtu na kutukana mtu nk.

8)       Kupotewa na fahamu(akili):- kwa kuzimia, kuwa kichaa, kulewa. Kwa maradhi, au kwa kulala ubavu, ama kulala huku umekaa bila ya kuegemea kitu udhu unakuwa haujatenguka.

9)       Aina zote za maasi(madhambi), mfano kula riba nk.

10)    Kuacha lolote lile la faridha au sunna za udhu, mfano: kutawadha juu ya socks bila ya kuzivua

HUKUMU YA KUTAWADHA JUU YA P.O.P AU JUU YA BENDEJI IKIWA MTU AMEUMIA ( MAS’H ALA JABIRA):-

Ikiwa mtu ameumia pahali na huku amefungwa P.O.P. au bendej juu ya pahali alipoumia, basi anatakiwa anapotawadha atie mkono wake maji kisha aukumute ndio kisha apanguse juu ya P.O.P au bendej hilo.

INAMUAJIBIKIA MTU AWE KATIKA UDHU (ATAWADHE) AKITAKA KUFANYA YAFUATAYO:

1)       Akitaka mtu kusali sala yeyote ile ya faridha au sunna. Na udhu wa salaa ni wajib.

2)       Akitaka mtu kutufu katika AL-KAABA. Amesema Mtume (SAW):- “ Tawaf ni salaa, isipokuwa M.Mungu ameruhusu watu kuzungumza.” Na udhu wa tawaf ni wajib.

3)       Akitaka mtu kulala. Amesema mtumu(SAW):- “ Ukitaka kulala, basi tawadha udhu wako wa salaa.” Na udhu wa kulala ni sunna.

4)       Akitaka mtu kusoma Qur’aan na kugusa msahafu. Kuna hadithi ya Mtume (SAW) kuwa amesema:- Juu ya watu wenye janaba na hedhi na wote ambao hawako katika udhu kuwa wasisome Qur’aan wala wasi ishike kwa mikono yao mpaka wawe wametawadha”. Na udhu wa kusoma Qur’aan au kuigusa ni sunna na ulamaa wengine wanasema kuwa ni wajib

Imeadikwa na:  Ahmed Saif  Al Harth

 

Copyright ©2004  Uislam.net