|
Nitawatambuaje wenye UKIMWI (AIDS) ili nijiepushe nao? (Dalili za Ukimwi)
Si rahisi kumtambua mtu mwenye UKIMWI kwa sababu dalili za ugonjwa
zinahitilafiana kufuatana na ugonjwa uliomnyemelea baada ya kuvurugika
kwa baadhi ya silaha zake za kujihami. Kwa mfano mtu mwenye UKIMWI
Baridi hataonyesha dalili zozote; na mtu mwenye UKIMWI Moto ambaye
amenyemelewa na viini vya ugonjwa wa kifua ataonyesha dalili za magonjwa
ya kifua kama vile kichomi, kukohoa, kutokwa na jasho usiku n.k.
Lakini kuna dalili fulanifulani ambazo mara kwa mara huonekana kwa wale
wenye UKIMWI Moto au Vuguvugu. Baadhi ya dalili hizo ni:
1. Unyong'onyevu na uchovu usio na sababu
maalum.
2. Kuvimba tezi shingoni, kwapani na kinenani.
3. Kukonda.
4. Homa ya muda mrefu.
5. Kuendesha endesha kwa muda mrefu.
6. Utando mweupe kinywani, vidonda mdomoni, na vidonda kooni. vyenye
kusababisha maumivu wakati wa kumeza.
7. Ukurutu katika ngozi
8. Kuvurugika akili
9. Kupungukiwa na damu.
Baadhi ya dalili kama hizo zinapoonekana kwa mtu ambaye haonyeshi kiasi
halisi cha ugonjwa unaozisababisha, basi anza kuwa mwangalifu zaidi
kuhusu ushirikiano wa karibu sana naye ambao utaruhusu kugusana na vitu
vitakavyokuwa vinamtoka?
Mtu mwenye UKIMWI (AIDS) anaambukizaje wengine?
Kila kimtokacho mtu mwenye UKIMWI (iwe UKIMWI Moto au Vuguvugu, au
Baridi) ndicho kinachoeneza ugonjwa kwa wengine. Baadhi ya vitu hivyo
vinavyotoka na ambavyo imethibitika kwamba mna viini vya UKIMWI ndani
yake ni:
Maji ya kiume ya uzazi, damu, maziwa na shahawa ya kike.
Njia yoyote inayoruhusu ama kuwezesha vitu hivi vinavyomtoka mtu mwenye
UKIMWI vipenye na kumwingia mtu mwingine tunaweza kuviita ni daraja la
kuvusha ama kueneza ugonjwa huu.
Kwa hiyo mtu mwenye UKIMWI ataweza kuambukiza wengine ugonjwa wake kwa
njia zifuatazo:
(a) Kama atakutana kimwili na watu wengine.
b) Kama atajitolea kutoa damu yake kuwasaidia wengine wenye
kuhitaji damu.
c
) Kama vyombo vitakavyotumika kumhudumia (anapodungwa sindano; au
anapochanjwa; au anapotahiriwa; au anapotoga masikio; au anaposhonwa na
kufungwa vijeraha n.k.) vitatumika pia kuwahudumia watu wengine kabla ya
kusafishwa na kuchemshwa sawa sawa inavyopasa.
d) Kama atabeba mimba na kuzaa watoto.
Mama mwenye UKIMWI(AIDS) humwambukizaje mwanawe?
Mama anaweza kumwambukiza mwanawe kwa njia zifuatazo:
1. Kwa kupitia sehemu inayounganisha mama na mtoto katika nyumba ya
uzazi, viini vya UKIMWI kutoka damu ya mama vinaweza kumwingia mtoto
akiwa bado tumboni, yaani kabla ya kuzaliwa.
2. Wakati wa kujifungua damu (yenye viini vya UKIMWI) inayomtoka mama
inaweza kumwingia mtoto.
3. Mama anaweza akamwambukiza mwanawe wakati wa kunyonyesha,
kutokana na viini vya UKIMWI vitakavyoweza kuwemo katika hayo maziwa
atakayokuwa ananyonya mtoto wake.
4. Pia kutokana na uhusiano na ushirikiano wa karibu sana uliopo
kati yao, kwa nadra mama asiye mwangalifu anaweza kwa njia ya vijeraha
mwilini au kwa njia nyingine za uzembe kusababisha damu au majimaji
mengine kutoka mwilini mwake ya mwingie mwanawe wakati anapomshika; au
wakati anapomwogesha; au anapomlisha; au anapochezacheza naye, n.k.
Je, ni vizuri watoto wenye UKIMWI Baridi waruhusiwe kukaa shuleni pamoja
wa wenzao?
Hakuna ubaya kufanya
hivyo, mradi tu uangalifu mkubwa zaidi uchukuliwe kuhakikisha kwamba
endapo watajeruhiwa au kutokwa na damu kwa njia yeyote ile wanapewa
haraka huduma kuzuia damu zao zisiwafikie watoto wengine.
|