|
MASUALA MUHIMU YA KUJIULIZA
1. Je UKIMWI ni adhabu itokayo kwa Allah na kwa hivyo hakuna haja ya
kutafuta kinga au tiba au ni maradhi kama mengine inabidi kinga na tiba
zitafutwe?
Kwa mtazamo wa Kiislamu maradhi yoyote ni mtihani kwa waja kutoka kwa
Mungu ili awatizame watafanya nini katika mtihani huo hivyo unaweza kuwa
adabu au njia ya kupandishwa cheo . Lakini jambo ikiwa ni mtihani au ni
adhabu kutoka kwa Mungu haina maana kwamba halifai kulitafutia tiba au
kinga.
Kwa hivyo ni lazima kutafuta kinga na tiba ya UKIMWI na ya maradhi
mengine ijapokuwa maradhi hayo ni adhabu au la.
2. Je mtu aliyepatwa na maradhi ya UKIMWI anakuwa amelaaniwa na ni
muovu au mbali na mambo hayo?
Aliyepatwa na UKIMWI hawezi kushutumiwa kuwa amelaaniwa au ni
mwovu mpaka ithibiti kuwa ni muovu katika matendo yake au kauli zake
kama ilivyo kwa wagonjwa wanaopatwa na maradhi ya aina nyengine. Kwani
UKIMWI waweza kuambukizwa pia kwa sababu nyengine ambazo si za haramu
wala si za makosa yanayowajibisha laana za Mungu. Njia hizo ni kama
maambukizo kutoka kwa mume au mke wa halali , au kwa njia ya kutiwa damu
au kunyonya n.k.
3. Ni wajibu upi wa kidini unaomwajibikia aliyepatwa na UKIMWI?
Aridhie kuwa hiyo ni Qadar yake kutoka kwa Mungu, astaghafiru sana
kwa Mungu, asizidiwe na mawazo na masikitiko na wala asieneze maradhi
haya kwa wengine. Bali afuate vilivyo maagizo ya wataalamu na ya
washauri nasaha.
4. Ni wajibu gani wa familia kwa mgonjwa wa UKIMWI?
Wawe wapole kwa muathirika wala wasimtenge kwani UKIMWI hauenei kwa
kukaa na mgonjwa, kula nae au kwa kubadilishiana nguo. Hata hivyo ni
vyema wawe waangalifu katika matumizi ya vyombo na zana zilizoingia damu.
5. Ni wajibu gani kwa jamii kwa wenye UKIMWI?
Wamhudumie vyema mgonjwa, wamjali, wasimtegenge na wasimnyanyapae au
kumuaibisha. Hayo ndiyo mafundisho ya Mtume S.A.W. alipokuwa akielezea
namna ya kuishi na mgonjwa aliposema: (Wahurumieni waliopo ardhini, na
yeye aliyeko juu atakuhurumieni). Akasema tena S.A.W. katika hadithi
nyengine (unapokwenda kumzuru mgonjwa, basi zungumza maneno mazuri
matupu...)
Hata hivyo pia inabidi pachukuliwe hadhari ili pasije pakatokea
maambukizo mapya kwa wengine. |