UKIMWI (AIDS) husababishwa na nini? 

UKIMWI husabaishwa na viini vidogo sana kupita kiasi vyenye uhai ambavyo wataalam huviita "VIRUS" au KIRUSI. Hivi ni viumbe vidogo sana sana ambavyo havionekani kwa macho wala kwa darubini za kawaida. Viumbe wa kabila hili la "virus" wapo wa aina nyingi na hutofautiana kwa maumbile na kwa madhara au magonjwa wanayoleta. Kwa mfano kuna virus wanaoleta ugonjwa wa mafua; na kuna virus wanaoleta ugonjwa wa surua; n.k.

Kwa kawaida mwili unao katika damu chembechembe maalum ambazo hutumika kama askari au silaha za kupigana na maadui, yaani viini vinavyoleta magonjwa. Viini vinavyoleta UKIMWI (AIDS) vikipata nafasi ya kupenya na kuingia katika damu yako vitaanza kuingia ndani ya baadhi ya chembechembe hizo maalum ambazo ndizo zenye jukumu la ulinzi na usalama mwilini. Baadhi ya chembechembe hizo zilizoingiliwa huweza kufa baada ya muda wa siku 20 hivi; baadhi nyingine huenda zikadhurika lakini zisife; na baadhi nyingine huenda zikadhurika kidogo tu. Kwa vyovyote viini vya UKIMWI ni kiboko kikali kwa chembechembe hizi ambazo ni baadhi ya silaha muhimu za mwili.

Viini vya UKIMWI vitakavyoingia ndani ya chembechembe hizo maalum za kujihami vitaweza kuendelea kuzaana humo na baadhi yake vitaweza hata kutoka na kuingia katika ubongo ambako vitaweza kujificha ama kuendelea kuzaana.

Viini hivyo vya UKIMWI vinapoendelea kuishi mwilini mwako huenda mambo matatu yakaweza kutokea baada ya kupita muda wa miezi minne mpaka miaka mitano au zaidi.

       1.    Utaweza kunyemelewa na magonjwa ya hatari ambayo yatakuletea kifo. Jambo hilo likitokea tutasema umepatikana na UKIMWI Moto.

       2.    Utaweza kunyemelewa na magonjwa rejareja yasiyoweza kuleta kifo. Jambo hilo likitokea tutasema umekumbwa na UKIMWI Vuguvugu.

       3.    Utaweza kuendelea kuwa na afya nzuri kama kawaida ya watu wengine. Jambo hilo likitokea tutasema kwamba UKIMWI ulionao ni Baridi.

    a.   UKIMWI Moto: Endapo viini vya UKIMWI vilivyoko mwilini vitafaulu kwa kiasi kikubwa kuvuruga silaha zako za kujihami, basi mwili wako utakuwa na uwezo mdogo wa kupambana na  magonjwa. Viini vya (magonjwa maalum mbalimbali ambavyo hapo awali vilikuwa havithubutu kukuingilia sasa vitakunyemelea kwa vile wewe umekuwa askari asiye na silaha zake kamili za kujitetea. Kwa mfano kama viini vya magonjwa ya tumbo, au vya magonjwa ya kifua vitabahatisha kuingia mwilini mwako kwa njia yoyote ile, vitakuta hakuna upinzani mkali; na kwa hiyo magonjwa hayo yatapata mteremko wa kukufyeka. Ukweli ni kwamba ukikumbwa na UKIMWI moto kitakachokuua sio viini vya UKIMWI moto kitakachokuua sio viini vya UKIMWI bali ni hayo magonjwa mengine yatakayokunyemelea kutokana na hali yako duni ya kujihami.

       b.    UKIMWI Vuguvugu: Endapo silaha zako za kujihami hazitavurugika sana basi uwezo wako wa kujihami hautakuwa duni sana, na kwa hiyo viini vya magonjwa vitakavyojaribu kukunyemelea vitakiona cha mtema kuni. Hata hivyo utakuwa unasumbuliwa sumbuliwa na magonjwa. Lakini wakati mwingine huenda huo UKIMWI wako uliyo vuguvugu ukaweza kubadilika na kuwa UKIMWI Moto kufuatana na mabadiliko fulani fulani yatakyoweza kutokea mwilini mwako, ama katika hivyo viini vya UKIMWI vitakavyoendelea kuishi mwilini mwako.

       c.    UKIMWI Baridi:

       Endapo viini vya UKIMWI vilivyoingia mwilini vitashindwa kuvuruga silaha zako za kujihami basi wewe hutasumbuliwa na magonjwa ya kunyemelea ama kuotea, na afya yako itaendelea kuwa ya kawaida. Isipokuwa yawezekana pia huo UKIMWI wako baridi ukaweza kubadilika hapo baadaye na kuwa vuguvugu au moto kutokana na mabadiliko yatakayoweza kukutokea wewe au kutokea hivyo viini vya UKIMWI vilivyomo mwilini mwako.

Copyright ©2004-2005  www.uislam.net