|
Ø
Uislamu:
Dini aliyoiridhia Allah, na maana yake ni “Kujisalimisha Mja
kwa Allah kwa kufuata Sharia yake”.
Ø
Allah:
Jina la aliyeumba kila kitu -hata sehemu na wakati-, hajafanana na chochote,
habadiliki, ni Mkamilifu wa Dhati kwa kila Sifa, hahitaji, hana mwanzo, wala
hatuwezi kumfikiri wala kumuona, na yeye haonekani kabisa.
Ø
Muislamu:
Yeyote aliyejisalimisha kwa Allah kwa kukubali kufuata Sheria yake. Mtu
atakua Muislamu kwa kushuhudia mambo matatu:
1.
Kua hakuna wa kuabudiwa kwa Haki isipokua Allah.
2.
Kua Muhammad ni Mtume wa Allah.
3.
Kua aliyokuja nayo Muhammad ni Haki inayotoka kwa Allah.
Ø
Nguzo za Uislamu:
Shahada, Sala, Zaka, Funga, na Hija.
Ø
Shahada:
Neno
la Ahadi ya kuingia katika Dini ya Uislamu nalo ni: Ninashuhudia kua hakuna
wa kuabudiwa kwa Haki isipokua Allah, na ninashudia kua Muhammad ni Mtume wa
Allah, na nimekubali kua aliyokuja nayo Muhammad ni Haki inayotoka kwa
Allah.
Ø
Sala:
Ibada maalumu inayolazimika kila siku mara tano, iliyokusanya Takbira,
Kusoma Qurani, Kurukuu, Kusujudu, Tasbihi na, Salamu.
Ø
Zaka:
Fungu
maalumu linatolewa na Matajiri katika Mali zao, kila mwaka mara moja kwa
ajili ya Mafakiri, Masikini, Kuunganisha Nyoyo, Wenye kuikusanya, Wapita
njia, Waliozidiwa na Madeni, Ukombozi wa Watumwa na Njia ya Allah.
Ø
Funga:
Kujizuia na kula, kunywa, kuingiliana kindoa, na kila kosa kubwa kuanzia
kuchomoza kwa Alfajiri mpaka kuzama kwa jua wakati wa Magharibi kwa nia ya
Ibada, kwa mwezi mzima wa Ramadhani, nao ni mwezi wa Tisa kwa mujibu wa
Kalenda ya Kiislamu.
Ø
Hija:
Ibada
maalumu ya Kuitembelea Al-kaaba, na sehemu takatifu zilizoko Hijaz katika
Mji wa Makka katika mwezi maalumu wa Hija.
Ø
Sheria:
Mafunzo ya Mtume katika Mitume ya Allah.
Ø
Mtume:
Mtu aliyepewa Sheria kutoka kwa Allah, muda wake utamalizika kwa kuja Mtume
mwengine baada yake, na kila watu wanalazimika kufuata Sheria ya Mtume wao.
Ø
Muhammad:
Mtume wa mwisho katika Mitume ya Allah. Na yeye amefuta Sheria za waliopita
kabla yake: Nuuh, Ibrahim, Mussa, Daudi, Sulaiman, Issa mwana wa Maryam,
n.w. wala hakuna Mtume mwengine baada yake.
Ø
Qur-ani:
Kitabu alichopewa Mtume Muhammad, kilichokusanya Sheria ya Allah, nacho ni
Dalili ya Utume wake, na hakuna kitabu kilichokua na mfano wake. Allah
amechukua ahadi ya kukihifadhi, basi kimehifadhiwa kwa Lugha yake, Muandiko
wake, na Visomo vyake kizazi kwa kizazi, nacho ni msingi wa mwanzo wa Sheria
katika Uislamu.
Ø
Sunna:
Yaliyo sahihi katika kupatikana kutoka kwa Mtume (s.a.w) ikiwa ni
Maneno, Vitendo au Maridhio kwa yaliyofanywa, nao ni Msingi wa Pili wa
Sheria katika Uislamu.
Ø
Ijmaa:
Makubaliano ya Wanavyuoni wa Kiislamu katika Hukumu ya Kitu iliofichika
Hukumu yake, bila ya kwenda kinyume na yaliyomo katika Qur-ani na Sunna
sahihi. Ijmaa ni Msingi wa Tatu katika Misingi ya Sheria katika Uislamu.
Ø
Hukumu:
Katika Uislamu kuna Hukumu tano; jambo lolote halitoki nje ya Hukumu
hizo tano, nazo zinathibiti kwa hiyo Misingi ya sheria ya Uislamu, nazo ni
Wajibu, Haramu, Man-duubu, Mak-ruuhu, na Mubaah.
Ø
Wajibu:
Ni Hukumu inayojuilisha kulazimika kukifanya kitu, anayefanya Wajibu anapata
Thawabu, anayewacha anapata Kosa la Dhambi kubwa; k.m: Kuwatii Wazee,
kusali, kufunga, kuhiji.
Ø
Haramu:
Ni Hukumu inayojuilisha kulazimika kukiacha kitu, anaefanya Haramu anapata
Kosa la Dhambi kubwa, anaewacha anapata Thawabu; k.m: Kuzini, Kulewa, kuvuta
Sigereti.
Ø
Man-duub:
Ni Hukumu anayojulisha kupendelewa kitu, anayefanya Man-duub anapata
Thawabu, anayewacha hana Kosa; k.m: Kuandikiana wenye kudaiana walio
waaminifu.
Ø
Mak-ruuhu:
Ni Hukumu anayojulisha kuchukizwa kitu, anayewacha Mak-ruuhu anapata
Thawabu, anayefanya hana Kosa; k.m: Kukaa na mwenye kutuhumiwa katika Dini.
Ø
Mubaah:
Ni Hukumu inayojuilisha kua kinachokusudiwa hakimo katika
moja ya Hukumu yoyote miongoni mwa hizo zilizopita; k.m: Kujichagulia
chakula katika yaliyo Halali, na Mja katika Mubaah analipwa kwa mujibu wa
Nia yake.
Ø
Nguzo za Imani:
Kuamini: Allah, Malaika wake, Vitabu vyake, Mitume yake, Siku ya Mwisho, na
Kadari ya Allah katika Matokeo yote.
Ø
Allah:
Jina la yule aliyeumba kila kitu, asiyekua na mwanzo wala
mwisho, kuwepo kwake ni kwa lazima, yeye ni mkamilifu wa dhati"
Ø
Malaika:
Viumbe wa Allah wasio muasi, wasioacha Ibada, wenye kufanya kila Amri
wanayoamrishwa, hatuwezi kuwaona, wako wanaoandika na kushuhudia yote
wanayoyafanya Waja wa Allah, wao wameumbwa kwa Nuru.
Ø
Vitabu:
Maandiko maalumu aliyoyajaalia Allah kua ni mkusanyo wa Sheria za Mitume;
vikiwemo Zaburi cha Mtume Daudi, Taurati cha Mtume Mussa, Injili cha Mtume
Issa na Qur-ani cha Mtume Muhammad. Na vitabu hivyo hakuna kilichobakia
katika Asili yake isipokua Qur-ani peke yake.
Ø
Mitume:
Watu aliowateuwa Allah kua ndio njia ya kufikisha Sheria zake kwa
Waja wake, wao wamehifadhiwa na Makosa makubwa, wanapata Ufunuo utokao kwa
Allah, na wao ni Hoja juu ya Waja. Mitume ni wengi sana miongoni mwao ni
Nuuh, Huud, Swaleh, Ibrahim, Is-haka, Is-mail, Yaaqub, Yuusuf, Yuunus, Luut,
Id-ris, Daud, Sulleiman, Mussa, Yahya, Issa, na wa mwisho wao ni Muhammad
(s.a.w), na kila Mtume inamalizika Ahadi yake kwa kuja Mtume wa mbele yake.
Ø
Siku ya mwisho:
Siku ya Malipo, ukubwa wake ni sawa na mika 50,000 ya hapa
Duniani, watasimama watu wote kwa ajili ya kulipwa kila mmoja kwa Imani yake
na matendo yake, aliyekua mwema kwa Kuifuata Sheria ya Mtume wake
aliyepelekwa katika zama zake; huyo atalipwa makazi mema katika Pepo yenye
kudumu, atapata humo kila analolitamani; na aliyekua Muovu kwa Kumuasi Mtume
wake, na yeye hakutubia, huyo atakua katika Adhabu yenye kudumu ya Motoni,
kwa mujibu wa Makosa yake, Allah atuepushe nao (Amin).
Ø
Kadari:
Makadirio ya mambo yote yatakayotokeza katika viumbe tokea kuanza kuumba,
nayo ni Siri ya Allah mtukufu, sisi ni juu yetu kujitahidi kwa kufuata
Sheria ya Allah, na huku tunaamini kua hakuna linalotokezea isipokua Allah
ametaka litokeze ikiwa ni Zuri au Baya, kwa sababu Allah haasiwi kwa
kushindwa, wala haadhibu kwa kudhulumu, na yanayowapata Waja ni kwa Mavuno
ya Utiifu au Kuasi kwao, au hua ni Mtihani kwa Waja wake.
Ø
Watu
ni watatu:
Muumini, Mnafiki na Mshirikina, mtu yeyote atakua ni mmoja katika hawa; na
yeye atakua ima Muislamu au Mshirikina, na atakua ima Muumini au Mkafiri.
Ø
Muumini:
Aliyekubali Sheria ya Allah na Ikamuhukumu katika Maisha yake katika fikra,
maneno na matendo yake.
Ø
Mnafiki:
Aliyekubali Sheria ya Allah lakini yumo katika Kumuasi Allah kwa kosa kubwa
katika fikra, au maneno, au vitendo vyake, mpaka atubie kwa Allah.
Ø
Mshirikina:
Anayeabudu asiyekua Allah, au kumshirikisha na chengine katika Ibada, au
kumkataa, au kupinga Hukumu iliyomo katika Sheria ya Allah inayojulikana
katika Uislamu kwa yakini, na kwa makubaliano.
Ø
Muislamu:
Muumini na Mnafiki.
Ø
Mkafiri:
Mshirikina na Mnafiki.
Ø
Ukafiri:
Kumuasi Allah kwa kosa kubwa lolote, nao umegawika vigao viwili: Ukafiri wa
Kinafiki na Ukafiri wa Kishirikina.
Ø
Ukafiri wa Kinafiki:
Kumuasi Allah kwa Kosa Kubwa lisilokua la ushirikina, mwenye kua na sifa
hiyo atapata haki zote za Waislamu isipokua Walayah.
Ø
Walayah:
Mapenzi kwa ajili ya kumtii Allah, kwa kusaidia, kupenda, kunusuru,
kurehemu, na kuridhia.
Ø
Ukafiri
wa Kishirikina:
Kumuasi Allah kwa Kosa la ushirikina, mwenye kosa hilo hana haki yoyote ya
Kiislamu, na haki yake ni Baraa-a.
Ø
Baraa-a:
Kinyume cha Walayah, nayo inalazimika kwa kila mwenye sifa ya Ukafiri, kwa
sababu kila Kafiri ni Adui wa Sheria ya Allah, basi laana ya Allah inakua
juu yake mpaka atubie.
Ø
Mezani siku ya Malipo:
Kila mja yatapimwa Matendo yake siku ya Malipo, Ima mezani zake zitakua
mzito au zitakua nyepesi.
Ø
Mezani mzito:
Mezani za Mja zitakua mzito kwa kukubaliwa Mema yake hata kama ni Jema moja,
atalipwa kwa hilo Jema lake, na kuongezewa na Allah mtukufu, na yeye atakua
katika Makazi mema katika Pepo bila ya Kuadhibiwa katika Moto, na Allah
anayakubali ya Waumini Wachamungu.
Ø
Mezani
nyepesi:
Mezani za Mja zitakua nyepesi kwa kukataliwa Matendo yake, kwa sababu ya
Maasi yake makubwa, ikiwa hakutubia kwayo, kwa sababu Allah hasamehe kwa
aliyeendelea na Dhambi kubwa mpaka yanapofika Mauti anasema: Ninatubia hivi
sasa”, na Allah haridhii watu Mafasiki; basi mtu huyo atakua katika Adhabu
ya Motoni kwa Mujibu wa Makosa yake, na yeye humo atabakia Milele bila ya
kukoseana au kutoka.
Ø
Shafaa:
Uwombezi wa Mtume siku ya Malipo, nao wataupata Waja wema aliowaridhia Allah
tu, kwa kukubaliwa Toba zao, na kupandishwa Daraja zao, na kuondolewa kwa
Mazito ya Siku hiyo, kutokana na yale Makosa ambayo walitubia kwayo; wala
hakuna Shafaa kwa Waovu madhalimu wa nafsi zao, hawakutubia kwa Maasi
makubwa waliyoyafanya, kwani Allah haridhii watu Mafasiki.
Ø
Jihadi:
Kujitahidi kwa kila njia ya kuiweza Nafsi katika kuyahama Mabaya, na
kuichukua kwa mujibu wa Sheria ya Allah, na kuilinda Dini na Njama za
Maadui, na kuindeleza kwa njia za Sheria; kama Kusomesha, kuitangaza,
kushikamana nayo katika raha na shida, wepesi na uzito bila ya khofu, wala
aibu, wala haya, na kuzuia Uadui dhidi ya Waislamu.
Ø
Hijrah:
Kuhama kwa Mtume Muhammad (s.a.w) toka Mji wa Makka kwenda Mji wa Madina, na
ndipo ilipoanza Tarekhe ya Uislamu ndani ya Sheria ya Mtume Muhammad kwa
Ijimaa ya Maswahaba (r.a).
Ø
Sahaba:
Kila aliyekutana na Mtume -katika Uhai wake- hali ya kua ni
Muislamu na akafa katika Hali hiyo.
Ø
Shetani:
Kila mwenye kumuasi Allah kwa makosa Makubwa na kufanya kila Juhudi za
kuwapoteza wengine na kuwaingiza katika Kufuru.
Ø
Ibilisi:
Shetani wa mwanzo, ni katika Majini huyo, aliifanyia Kiburi Amri moja tu -ya
kumsujudia Adamu-, basi alilaaniwa na kufukuzwa, kwani alikataa kutubia,
lakini alichukua Ahadi ya kukipoteza Kizazi cha Adamu.
Ø
Jini:
Kiumbe alichokiumba Allah kutokana na Moto, hatuwezi kukiona, na wao
wanazaliana, na wanaishi, wako Waislamu kati yao, na wako wasiokua Waislamu.
Ø
Maamrisho:
Kumtakasa Allah na Kufanana na Viumbe, au Viumbe kufanana na Allah.
Kukubali kua Muhammad ni Mtume wa Allah. Kusimamisha Sala katika Wakati
wake. Kutoa Zaka nayo ni 2.5% kila mwaka baada ya kutimiza kiwango cha 85g
za Dhahabu au 600g za Fedha, pia kuna Zaka ya Wanyama kwa Wafugaji wa
Wanyama wa Miguu minne, na Zaka ya Mazao ya Nafaka za kula kwa wakulima ni
10% kwa asiotilia maji na 05% kwa wanaotilia maji. Kufunga mwezi wa
Ramadhani. Kuhiji na Umra kwa mwenye uwezo. Wasia kwa Jamaa wasiorithi.
Kuwafanyia wema Wazazi wawili, Jamaa, Jirani, Masikini, Rafiki, Mpita njia
na Mgeni. Kutia jando kwa Mwanamme. Kuoga Baada ya Hedhi na Nifasi kwa
Mwanamke. Usafi. Kuoga Janaba baada ya kuingiliana au kutokwa na Maji ya
Uzazi. Udhu kabla ya Sala. Kukata kucha kila wiki. Kunyoa sehemu za siri
kila mwezi. Kuacha ndevu. Kupunguza masharubu. Kuamrisha Mema na kukataza
mabaya. Kutaka Idhini ya kuingia katika Nyumba. Kutoa Salamu. Kurejesha
Salamu, Heshima kwa wakubwa. Kuwarehemu wadogo. Ukweli katika maneno na
ahadi. Uaminifu. Kutafuta Riziki ya Halali. Kuondosha Maudhi. Kutafuta
Elimu. Kuhifadhi utupu. kukwepusha Jicho kwa kutoangalia ya Haramu. Kuvaa
kwa kuyasitiri aliyoamrisha Allah yasitiriwe -kwa mwanamme kutoka Kitovu
mpaka Magoti, kwa mwanamke ni mwili mzima isipokua Uso na Viganja-. Sadaka.
Kutubia. Kusamehe. Kusimamisha Ushahidi kwa wakaribu na wambali. Kuoa kwa
asiyeweza kujizuia. Kumtunza Yatima na mali yake. Kutembelea mgonjwa.
Kumkosha Maiti wa Kiislamu, kumsalia na kumzika. Mirathi kama alivyogawa
Allah katika Qur-ani. Kusimamisha Uadilifu kwenye uwezo. Kuwahudimia Wake na
watoto. Kuwahifadhi Wazazi na kuwatii, Kumpenda mwenye Kumtii Allah na Mtume
wake. Kuwatii viongozi Waumini Waadilifu. Kujifunga na Wanavyuoni Waumini.
Hailazimishi Allah Nafsi yeyote nje ya Uwezo wake, na yeye anawapenda wenye
kutubia na wenye kujitakasa na makosa na uchafu.
Ø
Makatazo:
Kumshirikisha Allah kwa kumfanyia msawa katika Sifa, Ibada na Sheria (Amri
na Makatazo). Kuvunja undugu. Kulewa. Kuzini nako ni kumuingilia mwanamke
bila ya ndoa. Ndoa ya waliozini, Kulawiti nako ni kuingilia katika Utupu wa
nyuma. Kusagana nako ni kupitisha matamanio ya kuingiliana baina ya mwanamke
kwa mwanamke. Kuikaribia Zinaa nako ni kuingia katika kila kinachopelekea
kuzini k.m: Muziki, kuangalia, kukonyeza, kugusa, kufikiri, kujitoa
matamanio kwa kujichezea. Kuiba. Kiapo cha uongo. Kusengenya nako ni kumsema
mwenzio kwa asiyoyapenda. Kufitini nako ni kuchukua na kupeleka maneno kwa
kusababisha ugomvi na chuki. Uongo. Khiyana. Kujisemea bila ya Elimu.
Kuwaudhi Wazazi. Kuasi amri ya kiongozi muadilifu. Kula maiti, nguruwe,
damu, najisi, uchafu, punda, kilichochinjwa bila ya kutajwa Allah juu yake,
na kila chenye meno ya ncha katika wanyama, na chenye kuwinda kwa makucha
katika Ndege. Kujiua. Kuidhuru Nafsi. Rushwa. Khadaa. Shahada ya Uongo.
Kudhulumu. Kuua Nafsi bila ya Haki. Kuua watoto. Kumkaripia Masikini. Kuishi
na zaidi ya Wake wanne. Kiburi nako ni Kudharau Haki, na kujiona mbele ya
watu. Kutembea kwa maringo. Kudanganya katika vipimo. Uhasidi nao ni
kutamani kuondoka neema ya mwenzako. Kutembea Uchi. Kuvaa mwili wako hasa
kwa mwanamke. Kujifananiza na Jinsi nyengine; mwanamke kujiingiza ya wanaume
kitabia, kimavazi, kimaumbile, na mwanamme kujiingiza ya mwanamke katika
hayo; kama kuvaa Dhahabu au Hariri. Kujibadilisha kimaumbile k.m kinyoa
nyusi, kuunganisha nywele, kuchonga meno, kupaka nyeusi kwa kuficha mvi.
Kula Riba nayo ni ongezo kwa mujibu wa wakati katika jinsi ya kitu. Kamari
nayo ni pato linalopatikana kwa kukusanya vya wengi kisha akapewa mwenye
kuangukiwa na kura na ndio wakaipa jina la Bahati na sibu ((Nipate au
nikupate)). Uadui. Kusaidia katika Dhambi na Uadui. Kumpenda mwenye kumuasi
Allah na Mtume wake. Na Allah anawapenda wenye kutubia na kujitakasa.
Ø
Neema:
Kila alilotupa Allah katika Uhai huu ni Neema kwetu sisi Waja wake,
basi ni wajibu wetu sisi Waja kumshukuru Allah katika Neema zake zote.
Ø
Kushukuru:
Kizitumia Neema za Allah katika anayoridhia Allah, Mja atapata Barka na
Nyongeza katika Maisha yake iwapo atashukuru; hata ikiwa ni Baya kwa
kusubiri kwani huo ni Mtihani.
Ø
Tahadhari:
Watu wengi wamepotea kwa sababu tatu: Kukipa kiumbe Sifa ya Muumba,
Kumpa Muumba Sifa ya Kiumbe, na kuitakidi Usamehevu bila ya Toba; na huu
wote ni upotevu katika Sifa za Muumba. Allah ametakasika na kila Upungufu na
Kuhitaji, na kwenda kinyume na aliyoahidi kwa Mitume yake (s.a.w); atuepushe
Allaha na Udhalimu wa kufuata Mapendwa moyo (Amin).
Ø
Kukipa
kiumbe sifa ya Muumba:
Hawa ni wale waliopotea kwa kujifanyia Mungu katika Vuimbe, ima Watu katika
Mitume, Wafalme, na Waja wema, Miti, Milima, Makaburi, Masanamu, n.v. wao
wanaviomba na kuviabudu, wanavipa uwezo wa aliyeumba kua navyo vinadhuru na
kufaa, vina Amri na Katazo, vinalipa na kuadhibu, ni vya Tangu havina Mwanzo
n.m.
Ø
Kumpa Muumba sifa za Viumbe:
Hawa ni wale walioitakidi kua Muumba anahitaji vitu vyengine katika
Ufalme wake, wakaitakidi kua yeye ana Sehemu, Sura, na Viungo vyote isipokua
Uchi na Ndevu, anashuka na kupanda, wako waliosema yeye ni kama sisi, na
wengine wakajificha kwa neno lao: Yeye sio kama sisi, lakini hayo anayo
kiuhakika, na Uhakika wake anaujua yeye mwenyewe.
Ø
Zinduka:
Sifa za Allah ni Maana za kuzingatia Ukamilifu wa Allah, na sio kitu
chengine kilicho nje ya Uhakika wake, kwa sababu yeye ni Mkwasi hategemei
wala hahitaji. Ametakasika na kila sifa inayolazimisha kupatikana chengine
ndio nayo ipatikane k.v: Mkono, Mguu, Macho, Masikio, Pua, Kuwepo katika
sehemu fulani n.k, kwa sababu yeye yupo kabla ya kuwepo kitu chochote, na
yeye hahitaji kitu, Sifa zake za Dhati ni yeye mwenyewe, anajua kwa Dhati
yake, Anaweza kwa Dhati yake, Anasikia kwa Dhati yake, kwa maana Dhati yake
imekamilika haihitaji kitu chengine katika kusifika, Uhai wake ni wakidhati,
Usikuvu wake ni wakidhati, Uoni wake ni wakidhati, Elimu yake ni yakidhati,
Uwezo wake ni wakidhati, na namna hivi.
Ø
Kuitakidi
Usamehevu bila ya Toba:
Mayahudi na Manasara walisema kua Pepo ni kwa ajili yao tu, na kua wao hata
kama wataadhibiwa basi ni kwa Muda mdogo wa siku chache tu, kisha
watasamehewa na kwenda Peponi, haya anayaeleza Allah katika kitabu chake, na
kueka wazi, kua ndio yaliyowapeleka katika kudharau Mafundisho ya Allah, na
kuyageuza ili yakubaliane na Mapendwa Moyo yao, na kuiharibu Dini kwa
kujichukulia Pato la kidunia, kisha wao Watasamehewa tu. Basi tujue kua haya
ndio Maradhi mabaya kabisa kwa waliopita, na ujihadhari yasije yakapata
Nafasi katika Fikra zako, kua na wewe maadamu ni Muislamu utafika Peponi tu,
hata kama utaadhibiwa basi ni kwa Muda tu, ukawa huna tofauti na hao
waliopita kabla yetu isipokua Majina tu, na ujue kua Allah ameiandaa Pepo
kwa ajili ya Waja wake walio Wachamungu Waumini waliowema, na kua Allah
ameandaa Adhabu ya Moto kwa ajili ya Waja wake Waovu wenye kumuasi wote,
ambao wameondoka na hawakutubia, basi na wewe ukiwa umo katika kosa Kubwa,
na hutubii ujijue kua Pepo ni haramu juu yako, na wala kutokosekana katika
Moto milele; basi tujiandae na sio kujipa matamanio tu, tukawa kama hao
waliopita.
Ø
Uislamu unahifadhi:
mambo matano ya Dharura katika Uhai; Dini, Akili, Nafsi,
Heshima na Mali.
1.
Dini:
inahakikisha Utulivu wenye malengo ya Kuridhiwa na Mola wako
-aliyeumba kila kitu- katika Maisha yako, basi ni lazima kulinda Dini kwa
Nafsi, Mali, Fikra, Malezi na Wakati.
2.
Akili:
Ni Haramu katika Uislamu kila linaloharibu Akili, k.m: Ulevi; Ni
lazima kuilinda na kila linaloharibu Akili, na kuihifadhi kwa kuikuza.
3.
Nafsi:
nayo
ni mwili, ni Haramu yanayosababisha kuiangamiza nafsi bila ya Haki, kama
vile kijiua, kuua, kuvuta Sigereti. Ni lazima kuuhifadhi Kiafya, Chakula
bora, na Usafi.
4.
Heshima:
Kila ninaloharibu heshima ya Muislamu ni Haramu, kama Matusi, Uzinifu,
kutembea Uchi; ni lazima kulinda Heshima zetu kwa Malezi bora ya Kiislamu,
na kukaa mbali na kila linalovunja na kuhatarisha Heshima zetu.
5.
Mali:
ya Muisalmu ni Haramu isipokua kwa kuridhika mwenyewe, na katika anayoridhia
Allah Mtukufu; ama wizi, dhulma, rushwa, riba, kamari, shahada za Uongo
vyote hivi ni Haramu.
Ndugu yangu huu
ndio Uislamu kama ulivyo katika kitabu cha Allah Qur-ani, na Mafundisho
sahihi yanayotoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w), na yasiyodhurika na mwenye
kwenda kinyume nayo, au kuyawacha, na kila Moja katika haya lina Ushahidi wa
Kutosha katika Kitabu cha Allah.
Assante sana.
Wassalamu alaykum warahmatullahi
wabarakatuh.
B
Ndugu yako: Hafidh. H. Seif Sawafiy
Imamu Msikiti wa Ibadhi - Bujumbura
sawafiy@yahoo.com
Box 17 Chake Pemba Tanzania
Tunakutakia usomaji mwema
(Amin).
1426A.H-2005A.D
|