PAGE NO 2

ELIMU INAOONDOA SHAKA NA INAJIBU MASWALI

Kila aina ya elimu ina faida kwa mwanaadamu, na hapana shaka kwamba kufahamu ni bora kuliko kuwa mjinga au kutokufahamu. Na ni ukweli usiofichika kwamba manufaa na faida yanayopatikana yanatofautiana kufuatana na aina ya elimu yenyewe inayohusika na kupatikana. Kwa sababu hii, basi bora ya elimu ni ile ambayo itamfanya mwanaadamu huyu afahamu kwa kinaganaga, wapi ametoka? Wapi anakwenda? Nini majukumu yake, na ni nini kazi yake katika dunia hii iliyojaa dhulma?, Jee ni mzigo upi aliobeba?, Vipi utakuwa uhusiano wake baina yake na baina ya watu wengine, na pia baina yake na baina ya ulimwengu anaoishi na kila kilichomo ndani yake?. Haya yote yanahitajia elimu na mwongozo, na elimu ya aina hii haiwezi kupatikana au kufikiwa kwa njia ya kufanyiwa utafiti na majaribio au kwa fikra za kibinaadamu. Kwani Elimu hii inatoka kwa Mwenyezi Mungu S.W.T. kupitia kwa Mitume Yake. Na ndiyo sababu Mwenyezi Mungu S.W.T. akatuma Mitume wakiwa waonyaji wa adhabu kali na wabashiriaji wa habari njema, na ili kuja kuondoa ile shaka na fikira potofu ambazo hujitokeza mara kwa mara katika akili na nyoyo za watu.

ELIMU YA MWENYEZI MUNGU IMEWEKA MAKATAZO NA MIPAKA KATIKA TABIA YA MWANADAMU

Jinsia ya tabia ya nafsi ya mwanaadamu ni ubahili na yenye kutaka kumiliki na kudhibiti kila kitu anachotamani. Kwa ajili hiyo basi, watu wote wanao ule mwelekeo wa tabia ya kutafuta au kupata maslahi yao hata ikawa itamaanisha ni kwa kuwaumiza wengine. Kwa sababu hizi mwanaadamu alihitajia kuwekewa mipaka ili iweze kumdhibiti na kumuongoza. Mipaka na muongozo huu umetajwa tu katika ujumbe wa Mwenyezi Mungu uliyoletwa kwa waja wake duniani kupitia kwa Mitume wake.

Ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa mitume wote ulifikia kikomo na kukamilika kwa risala ya mwisho ambayo alipewa mja wake Mtume Muhammad S.A.W., na ambayo inaelezea kwa kirefu na kwa ufasaha na kwa kinaganaga maisha ya mwanaadamu na makusudio ya kuwepo kwake ulimwenguni. Na imekigusa kila kitu kidogo na kikubwa kinachoingiliana na yeye. Ujumbe huu ulikuja kuongoza na kutengeneza tabia ya mwanadamu katika dunia hii, kwa makusudio ya kuyarekebisha maisha ya mwanaadamu yawe bora yenye kupendeza, na mwisho wa kilele cha malipo yake yamrudie yule atakayefuata na kutii maagizo yake na kutenda vitendo kama alivyoamrisha Mwenyezi Mungu S.W.T. kupitia Mitume ambao aliowaleta duniani.

Ni muhimu kuelezea kuwa ujumbe huu aliokuja nao Mtume Muhammad S.A.W. yaani ujumbe wa Uisilamu ni ujumbe ule ule uliotumwa kwa mataifa na watu wote wengine waliopita kabla kupitia kwa Mitume wao, na halafu baadae kuchaguliwa umma huu wa Muhammad S.A.W. kuupeleka ujumbe huu kwa watu wote ulimwenguni.

KUTAFUTA ELIMU NI MUHIMU KATIKA FANI ZOTE

Kwa kuongezea ni muhimu kwa mtu kujifunza elimu katika fani mbalimbali kufuatana na mahitajio ya jamii. Umma wa Kiisilamu unahitajia wanasayansi, unahitajia madaktari, mafundi wa kila fani, mabingwa wa kilimo, mabingwa wa fani nyingine mbali mbali, waalimu, wanajeshi na kazi nyinginezo kama hizo kwani kazi zote hizi ni kwa manufaa ya jamii ya wanaadamu wote kwa ujumla.

Lakini ni muhimu wakati Muisilamu anajifunza kazi fulani maalum anahitajika atambue kwanza kabla ya yote, sababu ya kuwepo kwake yeye hapa duniani, na anawajibika atimize majukumu yote yale ambayo amemfaradhishia Mwenyezi Mungu na hii ina maanisha lazima ajifunze elimu ya dini kufuatana na majukumu na mahitajio yake kwa wakati wake.

ADABU ZA KUULIZA SUALA

Watu wengi wanapotaka kuuliza suala basi huuliza kwa njia mbaya bila yao kujuwa, tena huwenda suala hilo akaulizwa shekhe mkubwa au katika wanavyuoni maarufu. Mifano mingi tunaweza Kutoa ili kuyabainisha makosa haya. Kwa mfano kuwenda mtu akamuuliza Shekh kwa kusema: eti Sheikh ukinywa pombe au ukizini au ukifanya…. Suala kama ili isimpigie mfano umuulizaye. Ulizi hivi: ikiwa mtu kanywa pombe au kazini au!.. Ili usije ukamkera unayemuuliza.

Ndio mara moja kuna mtu alimuuliza shekh Suala kwa kusema: Ikifa baba wa mkeo …kabla hajakamilisha Sheikh akajibu, mimi baba wa mke wangu kishafariki zamani.

Au mara nyengine mtu hujifedhehesha yeye mweyewe mbele za watu bila kujuwa. Unapokwenda kumuuliza Shekh suala na kumwambia ukasema mimi nilizini au nilikunywa pombe! Au..jaribu kuuliza tu ili wewe ujuwe hukumu yake ili upate ukufuata.

Mambo kama haya lazima Muislamu ayafahamu wazi wazi kwani daima kuwemo katika mzunguko wa masomo na kuuliza masuala, na bila ya kuuliza masuala basi itakuwa vigumu kupata elimu. Wala hakuna kuona haya kuuliza kwani mwenye kuona haya hatosoma.

 

Copyright ©2004  Uislam.net