SHEIKH AHMED BIN HAMED AL KHALILI
ELIMU NI HESHIMA
Hakika kimaumbile mwanaadamu anapendelea elimu, na elimu ni heshima, utukufu, pambo na daraja bora. Na kufuatana na elimu yenyewe ndiyo heshima na ubora wa daraja ya mtu inavyokuwa, kwani kuwa na elimu ni kupata heshima na utukufu.
Na ushahidi mzuri wa jambo hili ni kwamba utaona watu wengi wanajigamba kuwa na elimu ya fani fulani hata ya wao bila kuwa nayo, na hii ni kwa ajili ya kutaka kuheshimiwa, na kupata jaha na utukufu. Katika Uisilamu, elimu ina daraja ya juu kabisa. Na ni kwa sifa hiyo ya elimu Mwenyezi Mungu S.W.T. akawatofautisha wanaadamu na viumbe wengine. Tunaambiwa katika Qur`aan, Mwenyezi Mungu S.W.T. alipotaka kumuumba Adam aliwajulisha Malaika wake kwamba Atamuumba Adam ambaye atakuwa na daraja bora na utukufu kuliko wao. Na akawaamuru wamsujudie. Aya hizi zinazoelezea kisa hiki zinabainisha wazi umuhimu wa Elimu katika Uisilamu. Amesema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Qur`aani, Suratil Baqaraha Aya ya (30 mpaka 32):
“(Wakumbushe watu habari hii) Wakati Mola wako alipowaambia Malaika, “Mimi nitaleta viumbe wengine kukaa katika ardhi (Nao ndio wanaadamu)”. Wakasema (Malaika), “Utaweka humo watakaofanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutukuza kwa sifa zako na kukutaja kwa utukufu wako?” Akasema (Mwenyezi Mungu), “Hakika mimi nayajua msiyoyajua”. Na (Mwenyezi Mungu) akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema (kuwaambia Malaika) “Niambieni majina ya vitu vyote, ikiwa mnasema kweli (kuwa nyinyi ndio wajuzi wa mambo). Wakasema (Malaika), “Utukufu ni Wako! Hatuna ilimu isipokuwa ile uliyotufundisha, bila shaka wewe ndiye Mjuzi na Ndiye Mwenye hikima”.
AKILI NI CHOMBO CHA ELIMU
Hapana shaka kila mwanaadamu anafahamu kwamba ana mwanzo na pia anafahamu kuwa ana mwisho. Na hapana shaka kwamba kila mmoja wetu anafahamu ya kuwa baina ya mwanzo na mwisho mwanaadamu anahitajika kufanya au kutimiza majukumu fulani na kupatwa na mashaka fulani, na hii ni kwa sababu ya ile tabia ya maumbile ya asili ya mwanaadamu inayotofautiana na viumbe wengine waliomo katika ulimwengu huu.
Ni kwa sababu hiyo, Mwenyezi Mungu S.W.T. akamtunukia binaadamu huyu akili ambayo akiitumia vizuri anaweza kuvimiliki na kuvitumia viumbe vingine vilivyomo ulimwenguni humu kwa manufaa na maslahi yake, na kuyafanya maisha yake yawe mepesi na yenye furaha. Lakini akili hii aliyopewa binaadamu siyo imuwezeshe tu kutimiza haja yake kwa muda huu mfupi atakaoishi, yaani baina ya mwanzo na mwisho wa maisha yake hapa duniani, lakini pia ni kwa sababu amechukua majukumu kwa maisha yote atakayoishi. Na kwa vile pia ataulizwa kesho akhera na atapata jazaa yake huko akhera kwa yale yote aliyoyatenda hapa duniani.
Hivyo basi, inampasa binaadamu afahamu kuwa baada ya maisha haya yapo maisha mengine na kuwa elimu hii iliyomo katika risala tofauti za Mwenyezi Mungu walizokuja nazo Mitume Wake ililetwa ili ije kutatua yale mafumbo na kuondoa shaka ambazo zingeshamiri na kuenea kila mahala katika akili na nafsi za huyu binaadamu.
Na pia ni wajibu wetu kufahamu kuwa maisha ya mwanaadamu ni tofauti na yale ya viumbe wengine kwani kimaumbile maisha ya mwanaadamu ni maisha ya kimaendeleo na ni maisha ya kijamii. Hivyo basi hana budi kimaisha binaadamu achanganyike na jamii ya jinsi yake.
MATATIZO YA WAKATI LAZIMA YATATULIWE CHINI YA SHERIA ZA KIISILAMU.
Matatizo mengi yamejitokeza kufuatana na kubadilika kwa wakati na maendeleo ya jamii. Mfano kuna matatizo mengi ya kinadharia kuhusu msimamo wa dini katika baadhi ya mambo yaliyojitokeza katika fani ya utibabu baada ya kukua na kuendelea kwake na ambayo yalikuwa hayapo kabla. Au matatizo ambayo yanayohusiana na teknolijia mpya kama inavyojulikana. Haya matatizo ni lazima yachunguzwe na kutatuliwa chini ya kivuli cha sheria za Kiisilamu, kupitia katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Sunna za Mtume wake S.A.W. na Kauli ya pamoja ya wanavyuoni wacha Mungu waliotangulia wa taifa la Kiisilamu. Ni wajibu wa Wanavyuoni wa Kiisilamu kuyatambua haya matatizo vizuri ili waweze kuyatatua, na ili waweze kuwabainishaia Waisilamu wengine kwa ufasaha na kwa kinaganaga yote yanayohusiana nayo pamoja na faida na madhara yake. Ili kusudi iwe kinga kwao na wasiweze kuchupa mipaka ya Mwenyezi Mungu na kuingia katika kutenda vitendo vilivyo haramishwa. Kufanya hivi kunahitajia kuisoma elimu ya Kiisilamu kwa makini na kwa undani sana, na inamaanisha kukisoma na kukifahamu kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa undani, na elimu yake imejumuisha mambo mengi ikiwemo elimu katika lugha, tafsiri, na sheria na kadhalika. Na pia kusoma Sunna za Mtume S.A.W ambayo pia zimejumuisha kusoma mambo mengi kama vile elimu ya hadithi, chimbuko lake, wasimulizi wake na mambo mengine kama hayo. Na pia inahitajia kusoma misingi ya sheria ili kusudi mtu aweze kuwa na uwezo wa kutoa ushahidi kamili katika misingi sahihi inapohitajiwa, yaani kutoka katika kitabu Qur`aani takatifu na Sunna za Mtume wake S.A.W.
GO PAGE NO 2
Rudi katika makala
Copyright ©2004 Uislam.net