|
|
CHEO CHA
MTUME MUHAMMAD (S.A.W) |
Bismillahi Rrahmani Rrahim. Baada ya
kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumtakiya rehma Bwana Mtume wetu Muhammad Salla
Llahu Alayhi Wasalam na Masahaba zake wote.
Shukurani zote ni kwa ALLAH mtukufu, na Rehma
na Amani ziwe kwa Mbora wa viumbe Mtume wetu Muhammad (s.a.w) pamoja na Aali
zake na Maswahaba wake na kila mfuasi wa Uadilifu wake mpaka siku ya malipo
(Amin).
Kwa hakika ALLAH mtukufu anamnyanyua katika
Daraja anayemtaka miongoni mwa Viumbe wake, basi amemtukuza na kumnyanyua
daraja ya juu kabisa Mtume wetu Muhammad (s.a.w), ni fadhila anaiweka ALLAH
mtukufu kwa anayemtaka. Amesema Mtume Muhammad (s.a.w): Mimi ni mbora wa
watoto wa Adam wala hakuna Fakhari" na anasema: Lau kua Ndugu yangu
Mussa yuko hai basi asingalipata nafasi isipokua ya kunifuata mimi";
inatosha kua ALLAH Mtukufu hakumukhutubia kwa jina lake lakini kwa Cheo
chake, tafauti na Mitume mengine -juu yao iko Rehma na Amani-, na akamsifu
kua ni Rehma kwa ajili ya Walimwengu wote: Wala hatujakutuma isipokua ni
Rehma kwa Walimwengu" vile vile amekhusishwa na ALLAH kwa safari
maalumu ya kufika mbinguni katika Usiku maalumu wa Miijar, hiyo ilikua ni
zawadi ya kumpeleka katika sehemu yenye cheo cha kukifikwa yeye (s.a.w)
ambacho hajakipata yeyote katika waliopita kabla yake, nacho ni Daraja ya
kua Mtume wetu Muhammad (s.a.w) ni Imamu, na Manabii wote wako nyuma yake
wakiongozwa na yeye. Pia ALLAH Mtukufu ameufanya Umma wa Muhammad (s.a.w)
kua ndio Umma bora kabisa baina ya Umma zote zilizopita: Mumekua Umma
bora uliotolewa kwa ajili ya Watu" na kesho Akhera ALLAH mtukufu
atamnyanyua Daraja Mtume wake Muhammad (s.a.w) kwa kumfanya kua ni Muombezi
wa watu wote katika kuanza Hesabu na Kuingia katika Pepo zilizoandaliwa:
Ili akunyanyue Mola wako Sehemu ya Kutukuzwa".
Na sisi tukiwa tumo katika kumbukumbu za
kuzaliwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w) hatuna budi kueleza kua ALLAH mtukufu
amejaalia Umma huu uwe ni Umma wa kati na kati, na kututaka -ALLAH- tuwe
sisi ni wenye matarajio kwa kuzipita sababu zake, na kama kawaida ALLAH
mtukufu anatuelezea Umma zilizopita kabla yetu ili tusije tukafuata nyayo
zao, na miongoni mwa nyayo zao zilizoelezewa katika Kitabu ni kupindukia
katika Mipaka katika Dini, Wakiristo wamepindukia mipaka katika cheo cha
Mtume Issa bin Marayam (a.s.w) hata wakamfanya kua ni Mungu, na wengine
wakafanya kua ni Mtoto wa Mungu, na kua yeye ni mmoja katika utatu, na
Mayahudi wakapindukia mipaka yao mpaka wakamfanya Uzairi kua ni Mtoto wa
Mungu, na Wakawafanya watukufu wao ni Mabwana wakamsahau ALLAH.
Yote hayo yameelezwa katika Qur-ani ili
tuzingatie tusije tukapindukia Mipaka ndani na Dini hasa katika Haki ya
Mtume wetu Muhammad (s.a.w); lakini Jee!! Tumezingatia katika hilo la
kupindukia mipaka katika Haki yake au tumalivamia?
Kwa hakika tumevuuka Mipaka katika Haki ya
Mtume wetu Muhammad (s.a.w), na hayo yako wazi katika Mambo yafuatayo:-
1. Shafaa
ya Mtume (s.a.w): Kuitakidi kwetu kua Mtume
(s.a.w) atakuja kuwaombea Waislamu wote waliokufa hali ya kua wameyavaa
Madhambi makubwa yasiyokua ya Kishirikina ni jambo linalokwenda kinyume
kabisa ya yaliyokuja katika Qur-ani, kwa sababu Qur-ani inatubainishia kwa
Uwazi kabisa kua Madhalimu hawatopata Uwombezi wala Rafiki: Hakuna kwa
Madhalimu fariki yoyote wala muombezi wa kutiiwa" na Udhalimu katika
Sharia ya ALLAH mtukufu unakusanya kila kosa kubwa, kwa hivyo mwenye kwenda
kwa ALLAH na yeye anao mzigo wa Kosa kubwa huyo anayo sifa hiyo ya Udhalimu
ajijue kua hana Uwombezi wala Rafiki. Na vipi apate uwombezi au Rafiki hali
ya kua yeye yumo katika hali ya Ufasiki, na fasiki haridhiwi mbele ya ALLAH
mtukufu: Basi ikiwa mutaridhia kwao; basi kwa hakika ALLAH haridhii watu
mafasiki". Hakika kuishi kwa Muislamu katika Maisha haya na huku amebeba
Fikra ya kua yeye hatodhurika na Maasi kwa sababu ya Mtume wake Muhammad
(s.a.w) ni kupindukia Mipaka (Ghuluwu) katika Dini. Naam Shafaa ya Mtume
(s.a.w) ipo lakini Shafaa hiyo inawakusanya Waumini walio safi kotokana na
makosa, wametubia kabla ya kuondoka hapa Duniani, hao ni Wachamungu, hawa
peke yao ndio wenye Haki na Shafaa ya Mtume (s.a.w) kwa kupandishwa Daraja
zao katika Pepo, na kufanyiwa haraka hesabu zao, na kukubaliwa Toba zao, na
kuwekwa mbali na Mabayaya waliyoyafanya kasha wakatubia, kama ilivyokuja
katika Surati Ghaafir: Ambao wanachukua Arshi na walio pembezoni mwake
wanatukuza kwa utukuzo wa Mola wao na wanamuamini yeye na wanaomba msamaha
kwa ajili ya walioamini; Mola wetu umekienea kila kitu kwa Rehma na Elimu;
basi samehe kwa wale ambao wametubia na wakafuata njia yako na uwaepushie
Adhabu ya Moto * Mola wetu; na uwaingize katika Pepo safi ambayo
umewaahidi, na aliyetengenea katika Baba zao na Wake zao na Vizazi vyao;
Hakika yako wewe ni Mwenye nguvu Mwenye hikima * Na uwaepushie
Mabaya, na ambaye unamuepushia Mabaya siku hiyo basi umemrehemu; na hayo
ndio Mafanikio Makuu" Basi tujihadhari na yale ya Batili yaliyozuliwa
katika Haki ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w), ambayo yanamjenga anayeyakubali
katika matarajio ya Uongo yasiyokua na Ahadi katika Kitabu cha ALLAH, na
yenye kwenda kinyume na Qur-ani.
2. Kutoka
Motoni: Katika mambo yaliyopo -nayo ni kupindukia
Mipaka katika Haki ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w)- ni kule kuitakidi kwetu
kua yeye hatoacha kwenda katika Moto wa Jahannam ili kuwatoa Waislamu
waliomo humo, mpaka wamalizike wote, ni Itikadi inayokwenda kinyume kabisa
na Kitabu cha ALLAH Mtukufu, kwa sababu kitabu cha ALLAH kinatuwekea Bayana
ya wazi, kua hakuna kutoka katika Moto milele; kwa atakayeingia humo
ataendelea ni kubakia bila ya kukosekana: Hakika Wema watakua katika
Neema * Na hakika Waovu watakua katika Moto mkali *
Wataufikia siku ya Malipo * Na haitokua kwao na huo wenye
kukosekana" Sasa vipi yanatufikia Mafundisho kua Waovu watatolewa Motoni
si uongo ni nini? Na hali ya kua hakuna hata Aya moja inayoeleza kua kuna
Mtu atatoka Motoni, basi Qur-ani inatueleza kua Itikadi hii ni katika
Kupindukia Mipaka ndani ya Dini: Basi Ole wao ambao
wanaandika Kitabu kwa mikono yao kisha wanasema: Haya ni kutoka kwa Allah"
ili wanunue kwa hayo thamani ndogo; Basi ole wao kwa hayo iliyoandika Mikono
yao; na ole wao kwa hayo waliochuma * Na wamesema: Hautotugusa
Moto isipokua siku zenye kuhesabika" Sema: Jee!! Mulichuka kwa ALLAH Ahadi;
basi hatoiendea kinyume ALLAH Ahadi yake; au munasema juu ya ALLAH yale
musiyoyajua?"
3. Kumuabudu
Mtume (s.a.w): Na hili ninaingia kwa wale Wajinga
wanaojinasibisha na Uislamu, wao wamepindukia Mipaka mpaka kumfanya Mtume
(s.a.w) kua ni kama Mungu wa Kuombwa, hali ya kua ALLAH Mtukufu amesema:
Hakika Misikiti ni ya ALLAH basi usiombe pamoja na ALLAH yoyote" Aya
iliyokua wazi kabisa kua yeye ALLAH hataki ushirikisho katika Dua, lakini
utawakuta wengine baada ya kumuelekea ALLAH mtukufu wanamuelekea Mtume
(s.a.w) na wanamuomba yeye, na hapa sikusudii Tawassuli inayokubalika ndani
ya Sheria, nayo ni kumuomba ALLAH Mtukufu kwa kumtaja Mtume (s.a.w) kua yeye
ni Haki na Rehma, kwa mfano: Ewe Mola kwa Haki ya Mtume wako Muhammad
(s.a.w) tuwezeshe tuwe Wachaungu" huku ni kumuomba ALLAH mtukufu na sio
Mtume (s.a.w) ifahamike vizuri, na Haki ya Mtume (s.a.w) ni ule Uongofu wake
wa Haki, kwa hivyo ni kutuwezesha kuifuata Sheria yake na Uongofu wake ili
tuwe Wachamungu; ama kulikusudia kaburi lake kwa kwenda kumlilia Mtume
(s.a.w) na huku unamuomba na kuyayatika, ni mambo maovu katika Uislamu nayo
ni katika mila za Kishirikina.
4. Kuvuka
mipaka katika cheo chake: Na haya ni Maradhi
waliyonayo baadhi ya Watu, kiasi cha kua akiambiwa kua ALLAH amesema kitu
Fulani, na maneno ya Qur-ani yako mbele yake anayaona; unamuona anayachuka
maneno ya ALLAH kua ni jambo la kawaida, na kuyarudi kwa Mapokezi ya Dhana
kua Mtume ameyasema, na kuyapa mapokezi hayo cheo kikubwa zaidi kuliko
maneno ya ALLAH mtukufu, ni maradhi mabaya kabisa, nako ni kuvuuka mipaka
katika Haki ya Mtume (s.a.w), kwa sababu Qur-ani ndio Hakimu wa juu kabisa,
na yeye sio wa kuhukumiwa, na yako Mengi ya Uzushi ambayo yalifanywa na
Wajinga dhidi ya Mtume (s.a.w); na hili ndio lililowaingiza baadhi ya
Wajinga katika kunyanyua vyeo vya Wanachuoni wao kuliko Vyeo vya ALLAH na
Mtume wake (s.a.w) na kusema: Hakuna kheri katika Kitabu cha ALLAH bila
ya Sunna; wala hakuna kheri katika Sunna bila ya ufahamu wa Wema wetu
waliotangulia" na wengine hawalisemi hilo kwa ulimi wa maneno, lakini
kwa ulimi wa hali zao. Na hawa zimegeuka Mezani kwao, ALLAH atuondoshee kila
fitna, na atujaalia katika anayoyaridhia. Na hili halina maana ya kua ni
kudharau Mapokezi na Juhudi za Wapokezi lakini ni kuilinda Dini na Uchafuzi
wa wachafuzi, na yaliyosahihi katika Mapokezi yanakubaliwa na yanafanyiwa
kazi lakini kwa Mezani ya Ushahidi; kwa sababu Mtume (s.a.w) hawezi kwenda
kinyume na Kitabu cha Qur-ani, kwani Mwenendo wake (s.a.w) ni Sheria kwa
mujibu wa Qur-ani, na hapa itakua matokeo yake ni kuivunja Qur-ani, na ndio
ALLAH akasema: Na lau atajisemea juu yetu baadi ya Majineno *
Kwa hakika tungalichukua kwake kwa Nguvu * Kisha kwa
hakika tungalikata kwake mshipa wa shingo * Basi hakuna yeyote
katika nyinyi kua kwake wazuizi" sasa vipi aseme au afanye au aridhie
kinyume na Qur-ani? Na ndio yakapokewa Mapokezi Sahihi kutoka kwake (s.a.w)
kua amesema: Hakika nyinyi mutatofautiana baada yangu; basi kitakachokuja
kwenu kutoka kwangu kiwekeni katika Kitabu cha ALLAH; basi
kitakachukubaliana nacho hicho kinatoka kwangu; na kitakachopingana nacho
hicho hakitoki kwangu" sasa kimebakia kile ambacho hakipingani na
Qur-ani wala hakimo katika Qur-ani, hicho kitakua katika Uhakikisho zaidi wa
Wanavyuoni, kwa sababu ALLAH mtukufu amesema: Basi waulizeni Wana
kumbukumbu ikiwa nyinyi hamujui * Kwa Ubainisho na Dalili..
.
5. Kutukuza
Watu wa mezani ya Mtume (s.a.w): Wako wengine
wamejiingiza katika kuzingatia Usharifu katika Dini ni sawa Usharifu wa
Kisuhuba au wa Kiukoo, na wengine wamepindukia mipaka zaidi katika Jamaa wa
Mtume Muhammad (s.a.w), hata ikafikia kwao kuwapa urithi wa Sheria, na
kuwapa Taathira katika Uhai, ni upotevu juu ya Upotevu, kwa hakika Dini ya
Uislamu haikuja kumnyanua mtu kwa sababu ya Ukoo wake, wala Utaifa wake,
wala Ukabila wake, wala Usuhuba wake, lakini Uislamu umekuja katika mezani
ya Uadilifu, ya kua watu wote ni Sawa mbele ya ALLAH mtukufu amesema ALLAH
mtukufu: Enyi watu,, Hakika sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na
mwanamuke, na tumekujaalieni Mataifa na Makabila ili mujuane; Hakika Mbora
wenu kwa ALLAH ni Mchamungu wenu zaidi; hakika ALLAH ni Mjuzi Mwenye
khabari" kwa hivyo Mezani ya Uadilifu mbele ya ALLAH ni Uchamungu, na
sio chengine chochote, basi amesema ALLAH: Hakika ayakubali ALLAH kutoka
kwa Wachamungu" na Baba wa Mtume Ibrahimu (a.s.w) ni Mtu wa Motoni
milele kwa Ubainisho wa Qur-ani, na Mtoto wa Mtume Nuuh (a.s.w) ni wa Motoni
milele kwa ubainisho wa Qur-ani, na Mke wa Mtume Nuuh na Mtume Luut (a.s.w)
-wake wao wote- ni Motoni milele kwa Maelezo ya Qur-ani, na waliokufuru
katika Bani Israaili -juu ya kua wao ni wato wa Manabii- wamelaaniwa katika
Ulimi wa Dauni na Issa mwana wa Mariyamu (a.s.w): hayo ni kwa sababu ya
kule Kuasi kwao na walikua wakifanya Uadui" kwa ubainisho wa Qur-ani, na
katika yaliyopokewa kutoka kwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w) aliwaambia watu
wake wa Karibu akiwemo Bibi Faatimah (r.a): ..Ifahamike ya kua Vipenzi
wangu katika nyinyi ni Wachamungu, wasije wakaja watu siku ya Kiama na Dini,
na nyinyi mukanijia na Dunia mumeichukua…" hiyo ndio Mezani ya Usawa kwa
ajili ya Watu wote, sasa vipi tena yaje mambo ya Kurithi kwa kutumia Nasabu?
Hali ya kua Qur-ani inatubainishia kua Kuangalia Asili ni sababu ya Kibri,
pale aliposema ALLAH akituelezea aliyoyasema Ibliisi Mal-uuni: Mimi ni
bora kuliko yeye umaniumba kutokana na Moto na umemuumba kutokana na Dongo"
aliangalia Asili yake akadharau Amri ya Mola wake.
Tunamuomba ALLAH mtukufu atuwezeshe katika
anayoyaridhia na atuepushe na anayoyakasirikia tuwe sababu ya Uongofu tusiwe
Wapotovu wala Wapotevu. Na anyanyue Bendera ya Waumini na aangushe Bendera
ya Makafiri, na awaondoshee ndugu zetu Udhalilifu popote pale walipo, na
aunganishe nyoyo za Vijana katika Utiifu wake. Na Rehma na Amani ziwe kwa
Aliyechaguliwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w) pamoja na Aali zake na Maswahaba
wake mpaka siku ya Malipo .
(Amin).
Wassalamu alaykum
warahmatullahi wabarakatuh
Ndugu yenu: Hafidh. H.
Seif Sawafiy
Imamu wa Msikiti wa
Ibadhi Bujumbura – Burundi.
sawafiy@yahoo.com
09/03/1426H – 18/04/2005M |